The House of Favourite Newspapers
gunners X

Polisi Wafunguka Ukweli wa Ajali ya Shilole Kigoma, Watoa Wito kwa Madereva

0
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Shilole

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limetolea ufafanuzi taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hususan TikTok, zikidai kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Shilole, amepata ajali mbaya ya gari mkoani humo.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa mnamo Januari 3, 2026, Jeshi la Polisi limefafanua kuwa taarifa hiyi inayoashiria msanii huyo kuumia akiwa safarini kuelekea Dodoma haujathibitishwa kituoni.

“Ukweli ni kwamba taarifa hiyo ya ajali haijaripotiwa kituo chochote cha Polisi Mkoa wa Kigoma,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ACP Philemon Makungu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ACP Philemon Makungu

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa mujibu wa uvumi huo, gari aina ya Toyota Alphard lilikuwa likitumiwa na msanii huyo na kudaiwa kugonga ng’ombe katika eneo la Maragalasi, Wilayani Uvinza. Licha ya maelezo hayo ya kina mtandaoni, Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa hakuna kumbukumbu rasmi ya tukio hilo.

Akizungumzia utaratibu wa kisheria, Kamanda wa Polisi kupitia taarifa hiyo ametoa wito kwa msanii huyo: “Endapo tukio hilo la ajali lilitokea, tunatoa wito kwa Shilole kufika kituo chochote cha Polisi kuripoti ajali hiyo, ili uchunguzi uweze kufanyika na hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mtuhumiwa aliyesababisha ajali hiyo.”

Aidha, Polisi imewakumbusha madereva wote mkoani humo umuhimu wa kufuata sheria ili kuepuka majanga. “Tunashauri dereva yeyote anapopata ajali akiwa safarini… anawajibika kutoa taarifa Kituo cha Polisi ili aweze kupata msaada wa matibabu, kuchunguza chanzo cha ajali na kuchukua hatua stahiki.”

Leave A Reply