Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ameahirisha safari yake ya kwenda China kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nje taifa hilo, Wang Yi baada ya kuonekana kwa ‘puto’ ambalo Marekani imedai ni kifaa cha kijeshi kinachochunguza anga la Marekani.
Blinken amesema amemtaarifu Waziri Yi kuwa hatafanya ziara hiyo kufuatia kitendo chao cha kuvunja sheria za anga kwa kurusha kifaa hicho kwenye anga la Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imekanusha taarifa hiyo kwa kusema kuwa puto hilo siyo kifaa cha kijeshi bali ni kifaa cha kufanya utafiti wa hali ya hewa ambacho kiliingia kwa bahati mbaya kwenye anga la Marekani baada ya kupoteza mwelekeo.
Uamuzi wa kuahirisha ziara hiyo umefanywa baada kikao kizito kilichofanyika kati ya Rais Joe Biden na wakuu wa Idara za Usalama.
Rais Biden amekataa mpango wa jeshi kutungua puto hilo akihofia usalama wa watu.