Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah Wa Namibia Awasili Nchini Tanzania Kwa Ziara ya Siku Mbili
Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amewasili nchini ambapo anatarajiwa kufanya ziara ya kiserikali ya siku mbili kuanzia Mei 20 hadi Mei 21, 2025, kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hii itakuwa ziara ya kwanza ya Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Namibia mnamo Machi 21, 2025, na inalenga kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika nyanja za biashara, uwekezaji na elimu.
Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kindugu na kidiplomasia, hivyo ziara hii inalenga kufungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowanufaisha wananchi wa nchi zote mbili kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atapokelewa Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Samia ambapo viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na baadaye kuongoza mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo mbili, kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Aidha, akiwa nchini Tanzania, Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atatembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama sehemu ya kuthamini mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi barani Afrika, sambamba na kukuza ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni kati ya Namibia na Tanzania.
Rais Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajiwa kuhitimisha ziara yake tarehe 21 Mei 2025.
Na: Elvan Stambuli – GPL


Comments are closed.