Rais Samia: Acheni Kuvamia Maeneo Ya Hifadhi – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kuacha kuvunja sheria kwa kuvamia maeneo ya hifadhi na badala yake kutunza mazingira hayo.
Kauli hiyo imekuja kutokana na maombi ya Mbunge wa Mlele, Isack Kamwelwe aliyeomba kumegewa ardhi katika maeneo ya hifadhi ya mapori yaliyopo jimboni kwake. Rais ameyasema hayo leo Julai 13,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi katika Wilaya ya Mlele, Kata ya Inyonga Mkoani Katavi ambapo pamoja na kumuahidi Mbunge huyo maombi ya wananchi kushughulikiwa na Wizara husika kisha yatafika kwake.

“Tunajua kuna uhaba wa ardhi na kuna maeneo ya hifadhi mnayatamani lakini hayaendani na kuvunja sheria tukae tuzungumze tuangalie namna ya kuyamega na si kuvamia” amesisitiza Mhe. Rais Samia.
Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu ombi la Kamwelwe la kuongezewa hekta elfu 15 katika Pori la Akiba Inyonga,Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea maombi hayo na inaendelea kufanya tathimini kuangalia uhitaji halisi na kuyawasilisha kwa mamlaka kwa hatua zaidi.