Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 15, 2021 amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Sera za Maendeleo na Ubia wa Benki ya Dunia (WB), Prof. Mari Pangestu Ikulu Jijini, Dar es Salaam.
Mhe. Rais Samia amemshukuru Prof. Pangestu kwa ushirikiano mkubwa na wa kimkakati katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametumia mazungumzo hayo kumueleza Mkurugenzi huyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule, vituo vya afya, ufanisi katika matumizi ya TEHAMA na miradi ya kikanda.
Kwa upande wake Prof. Pangestu amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kutekeleza miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kiwango cha juu na kusema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano.
Aidha, Prof. Pangestu amesema Benki ya Dunia inaunga mkono uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuendeleza elimu mbadala kwa wanafunzi wote walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali.
Prof. Pangestu ameonyesha utayari wa Benki ya Dunia kusaidia Mfumo wa Ekolojia ya kidijitali kuleta ufanisi katika matumizi ya TEHAMA.