The House of Favourite Newspapers

Chlamydia: Ugonjwa Hatari Wa Zinaa-2

Chlamydia trachomatis/ Wadudu wasababishao Chlamydia

TUMALIZIE makala yetu ambayo tulianza kueleza wiki iliyopita kuhusu ugonjwa hatari wa zinaa unaoitwa kitaalamu Chlamydia. Leo tueleze dalili kwa watu wazima na watoto na tiba pia ushauri.  

DALILI Dalili za ugonjwa huu kama umeathiri puru (rectum) kwa wanawake na wanaume ni kama ifuatavyo: Kuwashwa na kutokwa na damu kwenye puru, maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa na kutokwa na uchafu kama kamasi kutoka kwenye puru.

Iwapo vimelea vya chlamydia vitaathiri macho, wanawake na kwa upande wa wanaume huwa na dalili zifuatazo; Mwanamke huvimba kwenye macho au macho kuwa mekundu pia kuwasha na hata kutokwa na majimaji machoni.

Chlamydia inayoambukiza kwenye macho (Chlamydia Conjunctivitis or Trachoma) ndiyo inayoongoza kwa kusababisha upofu duniani, hivyo yatupasa kujihadhari sana.

VIPIMO NA UCHUNGUZI

Baada ya mtu kuhisi dalili hizo tulizozitaja hapo juu, hupaswa kwenda hospitalini au katika kituo cha afya ili kupimwa na kuthibitishwa kwamba ana ugonjwa huo ili apatiwe matibabu. Vipimo vya uchunguzi vya ugonjwa wa Chamydia ni Urethral Swab for Culture.

Katika kipimo hiki majimaji kutoka kwenye uume au uke huchukuliwa kwa kutumia kijiti chenye pamba au swab maalum ambayo hupelekwa maabara ili kuoteshwa na kuangalia aina ya uoto wa bakteria.

Pia huchukuliwa vipimo vya mkojo na pia kipimo cha PCR au Polymerase Chain Reaction, ambacho ni cha kuangalia vinasaba vya bakteria au DNA na hufanywa katika maabara.

Baada ya majibu kuonyesha kuwa mgonjwa ameambukizwa vimelea vya ugonjwa huo matibabu hufuata. MATIBABU YAKE Chlamydia ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayotibika na ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa aina ya antibiotiki zilizopo kwenye makundi ya Macrolides, Quinolones na Polyketides ambazo hutolewa chini ya maelekezo ya daktari.

MADHARA KWA WANAUME Lakini madhara ya ugonjwa huu ni yapi?

Mpenzi msomaji, madhara ya ugonjwa huu kwa wanaume ni kuwa huathiri korodani na kusababisha mwanamume kukosa uwezo wa kuwa na watoto au kuwa tasa na pia husababisha maambukizi kwenye tezi dume (Prostatitis).

MADHARA KWA WANAWAKE

Kwa wanawake, husababisha maambukizi kwenye mirija ya uzazi, mfuko wa uzazi, na mayai ya uzazi, kwa hivyo kusababisha ugonjwa wa uvimbe katika fupanyonga au Pelvic inflammatory disease (PID).

Pia huongeza uwezekano wa wanawake kupata mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi ambazo kitaalamu huitwa Ectopic pregnancy. Mbali na hilo, mwanamke hupata maumivu sugu kwenye nyonga na ugonjwa wa mifupa arthritis aina ya Reiters Syndrome. Vilevile, Chlamydia huweza kusababisha ugumba kwa mwanamke kama hatapata tiba.

Si hayo tu, kwa wanawake wajawazito, Chlamydia husababisha wajifungue kabla ya wakati wake. Pia mtoto anaweza kuzaliwa na maambukizi kwenye masikio, sehemu za siri, macho na kwenye mapafu yaani wakapata homa ya mapafu na kama mtoto hatapatiwa tiba ya haraka ya macho baada ya kuzaliwa basi anaweza kuwa kipofu.

DALILI WATOTO WACHANGA

Dalili za Chlamydia kwa watoto wachanga hutokea katika kipindi cha wiki mbili kwenye macho, na iwapo ni homa ya mapafu dalili zake hujitokeza katika kipindi cha wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.

WAJAWAZITO

Kwa wanawake wajawazito, ni vizuri kuhudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito na kupimwa vipimo mbalimbali ambapo kimojawapo ni cha kuangalia iwapo mama mjamzito ameathirika na ugonjwa huu na kupatiwa matibabu mapema.

USHAURI

Kwa wale wenye m a a m bukizi wanashauriwa kuchukua tahadhari ya kutowaambukiza wapenzi wao kwa kufanya ngono salama, pia kuepuka kushika macho kwa kutumia mikono na hata ikiwezekana kuwaepuka wapenzi wao ili kuwalinda na maambukizi.

Vilevile kwa wale ambao wapenzi wao wameambukizwa au wameonyesha dalili za ugonjwa huu, wanashauriwa na wao pia kupata tiba hata kama hawana dalili zozote. Kwa hakika kama wasemavyo wahenga kinga ni bora kuliko tiba, basi tujilinde na kujiepusha na magonjwa yote yakiwemo ya zinaa yanayoweza kuepukika, daima tuzilinde afya zetu!

KINGA

Nihitimishe kwa kuelezea jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa zinaa wa Chlamydia. Kwanza kabisa kama nilivyoeleza kwenye kipindi kilichopita, njia sahihi ya kujikinga na magonjwa ya zinaa ni kuacha au kuepuka kujamiiana au kufanya ngono zembe na zisizo salama.

Comments are closed.