The House of Favourite Newspapers

Salah Afukuzia Kuweka Rekodi Mpya Ligi Kuu England

BAADA ya kung’ara kwenye mechi dhidi ya Arsenal, wikiendi iliyopita, straika wa Liverpool, Mohamed Salah sasa anafukuzia kuweka rekodi mpya. Salah alipachika mabao mawili wakati Liverpool ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Arsenal kwenye mechi ya Ligi Kuu England, wikiendi iliyopita.

 

Alipachika bao moja la penalti katika mchezo huo huku lingine akilifunga baada ya kumlamba chenga na kumtoka beki wa Arsenal, David Luiz.

 

Salah inasemekana amewaambia watu wake wa karibu kuwa anataka kujitahidi kadiri awezavyo avunje rekodi ya kupachika mabao mengi aliyoweka katika msimu wa 2017/18. Staa huyo wa timu ya taifa ya Misri alipachika mabao 44 kwenye msimu huo na kuingia katika orodha ya mastaa waliowahi kuifungia timu hiyo mabao mengi katika msimu.

Salah kwa sasa ana mabao matatu kwenye Ligi Kuu England na ana nafasi ya kuongeza mabao zaidi
yakianza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Carabao na FA.

 

Straika huyo, hata hivyo, anataka rekodi hiyo ya mabao mengi iwe pia chachu ya kusaidia timu hiyo kumaliza kiu yao ya ubingwa wa England, ambao mara ya mwisho waliupata msimu wa 1989/90.

 

Salah alipachika mabao 27 tu, katika msimu uliopita wa 2018/19, ingawa alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England akiwa na mabao 22 sawa na straika mwenzake wa Liverpool, Sadio Mane na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal

Comments are closed.