The House of Favourite Newspapers

Serikali yatoa siku mbili kwa Wamiliki wa viwanda vya kubangua Korosho

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amewapa siku mbili wamiliki wa viwanda vya ubanguaji korosho kupitia mikataba waliyopewa na serikali ya Tanzania ili kuingia makubaliano ya kuanza ubanguaji.

 

Akizungumza mjini hapa jana, Jumamosi Desemba 15, 2018 amesema kwa sasa kiwanda kilichopewa korosho kwa ajili ya ubanguaji ni cha Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mtwara kwa majaribio na baadaye watasaini mkataba.

 

Amesema kwa upande wa kiwanda cha Buco kilichopo Lindi, wataalamu wanaendelea kukiboresha ili kiweze kuanza kazi rasmi na kuagiza mtambo mpya.

 

Kakunda amesema viwanda vyote 23 vilivyopo nchini kwa sasa vina uwezo wa kubangua tani 130,000 kwa mwaka, lakini vinavyofanya kazi ni vinane pekee.

 

“Lengo letu ni kuvifufua viwanda vilivyosimama vyote vifanye kazi. Vilivyopo uwezo wake ni kubangua tani 50,000. Tunafufua kiwanda cha Buco, Nachingwea na Newala, kwa hiyo uwezo utaongezeka kadri tutakapofufua viwanda zaidi, pia tunaagiza mitambo mipya,” amesema Kakunda.

 

Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema hadi Desemba 14, mwaka huu, vyama vya msingi (Amcos) 461 vya wakulima wa korosho katika msimu wa mwaka 2018/19 vimehakikiwa na kati ya hivyo, 451 vimeshalipwa.

Amesema hadi hadi tarehe hiyo, baadhi ya wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani walikuwa wameshalipwa Sh133.2 bilioni.

“Ni wazi kabisa fedha hizo tumezilipa vizuri na nina imani mambo yanakwenda vizuri,” amesema Hasunga.

Kuhusu kiasi cha korosho walichokusanya katika maghala husika awaziri huyo amesema tayari wamekusanya tani 178,049 na lengo ni kukusanya tani 275,191 ambazo zote zitabanguliwa nchini.

“Ninachoambiwa ni kwamba katika vyama vya msingi bado kuna korosho na wananchi bado wana korosho nyumbani, nitumie fursa hii kuviomba vyama vya msingi kupokea korosho zote kutoka kwa wananchi ili hali ya hewa ambayo inabadilika isije ikaathiri ubora wa korosho zilizo mikononi mwa wakulima,” amesema Hasunga

Kuhusu madaraja ya korosho, amesema hivi karibuni watawatangazia wakulima bei ya korosho za daraja la pili.

“Changamoto kubwa ambayo sasa ipo tumeanza kupokea korosho daraja la pili na hasa mkoani Pwani ambako korosho nyingi zinaangukia katika daraja hili, wanazo tani 20,000 kati ya hizo daraja la kwanza ni chache sana,” amesema Hasunga

Comments are closed.