The House of Favourite Newspapers

Sibomana Atengeneza Mifumo Miwili Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera amepanga kutumia mifumo miwili atakayoitumia kwenye msimu ujao ambayo ni 3-4-3 na 4-5-1.

 

Mkongomani huyo tayari ameanza kuitumia mifumo hiyo kwenye michezo ya kirafiki waliyoicheza pamoja na wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

 

Kocha huyo kwenye msimu uliopita alikuwa akitumia mfumo wa 4-4-2 na 3-5-2, ambao ulifanikisha timu hiyo kumaliza Ligi Kuu Bara katika nafasi ya pili.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema amepanga kutumia mifumo hiyo kutokana na aina ya wachezaji wazuri wenye kasi aliowasajili baadhi ni Patrick Sibomana, Juma Balinya na Sadney Urikhob.

 

Zahera alisema kuwa ana matarajio makubwa ya timu hiyo kufanya vizuri kwenye msimu ujao kutokana na ubora wa kikosi chake kinachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Aliongeza kuwa mifumo hiyo itatoa nafasi kwa viungo akina Papy Tshishimbi, Mohammed Issa ‘Banka’, Mapinduzi Balama na Sibomana kumiliki mpira kwa dakika 90. “Msimu huu nina kikosi bora cha kufanya vizuri kwa kuanzia mashindano ya kitaifa na kimataifa ambacho ni tofauti na cha msimu uliopita.

 

“ Hii ndiyo sababu ya kufanya usajili wa wachezaji wengi na kikubwa kuwa na kikosi kipana ambacho kinanifanya mimi nimtumie mchezaji yeyote atakayeendana na mfumo husika nitakaoutumia kwenye mechi.

 

“Nafurahia kasi ya viungo wangu na mpira wanapopeleka mashambulizi kwenye goli la wapinzani wetu kwa kasi ambapo pia wakipoteza mpira wanakaba wote,” alisema Zahera.

Comments are closed.