Simba yapanda hadi nafasi ya pili msimamo wa Ligi Kuu
Klabu ya Simba SC imefanikiwa kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania bara baada ya kupata ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Namungo FC na kujikusanyia alama zote 3.
Simba sasa wamefikisha alama 19 katika michezo 8 msimu huu, wakiwa nyuma ya vinara Singida Black Stars wenye alama 22 katika michezo 8 huku nafasi ya 3 ikishikiliwa na Klabu ya Yanga wenye alama 18 katika michezo 6.
Magoli ya Simba yamefungwa na nyota wa mchezo huo, Shomari Kapombe aliyefunga goli la kwanza katika dakika ya nne ya mchezo, huku kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Steven Mukwala dakika ya 33 na kuiandikia timu yake bao la pili kabla ya Deborah Mavambo kupigilia msumari mwa mwisho dakika ya 85.
Simba wanatarajia kushuka dimbani tena Oktoba 29 dhidi ya JKT Tanzania, huku klabu ya Namungo ikitarajiwa kucheza mchezo wake mwingine dhidi ya Pamba Jiji Oktoba 28.