WIZARA ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia (WyEST) kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imesaini mkataba wa hati ya makubaliano (MoU) ya utekelezaji wa mradi wa “Korea e-Learning Improvement Cooporation (KLIC)” na Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan (GMOE) kupitia Global Education and Research Information Service (GERIS) ya nchini Korea Kusini wenye lengo la kuboresha elimu nchini katika eneo la TEHAMA.
Tukio hilo limefanyika leo tarehe 7/11/2023 makao makuu ya TET jijini Dar es salaam ambapo, Naibu Katibu Mkuu wa WyEST Prof. James Mdoe amesema kuwa kusainiwa kwa hati hiyo inaashiria azma thabiti ya kuboresha elimu na kuwaimarisha walimu na wanafunzi nchini katika matumizi bora na sahihi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.
“ Ushirikiano huu umekuja wakati muafaka tunapoanza kutekeleza mabadiliko ya mitaala inayotarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2024.
Mabadiliko haya yamesisitiza matumizi ya teknolojia na ni wazi kuwa mafunzo ya walimu na vifaa vya TEHAMA vinavyotolewa kupitia mradi huu yatawezesha wanafunzi kupata umahiri uliokusudiwa” amesema Prof. Mdoe
Kwa upande wake Gavana wa Gwangju Metropolitan, Mhe. Lee Jeong seon amesema kuwa, wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha matumizi ya TEHAMA kwenye eneo la ufundishaji na ujifunzaji yanazingatiwa jambo litakalosaidia kwenye suala la maendeleo .
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema kuwa ushirikiano huo mpaka sasa umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uelewa wa walimu juu ya matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji .
Pia, ameeleza kuwa kwa awamu hii ya mradi shule mbili zitanufaika na mradi huo ambapo Shule hizo zipo Halmashauri ya Mji wa Njombe katika Mkoa wa Njombe. Shule hizo ni shule ya Msingi Mkombozi na Shule ya Sekondari Mabatini ambapo vifaa vya TEHAMA vinavyokwenda katika shule hizo vimeshapokelewa kutoka Korea Kusini .
Aidha, kama ilivyo kuwa katika makubaliano ya awali walimu wa shule hizi pia watapatiwa mafunzo ya masafa na baadaye watapata nafasi ya kuhudhuria mafunzo ya ana kwa ana nchini Korea Kusini.
Aidha, kwa sasa mpango huo unaendelea katika shule za Tegeta A na Kimbiji ambapo wanafunzi wanaendelea kujifunza masuala mbalimbali ya tehama.