The House of Favourite Newspapers

Twaweza: Asilimia 80 ya Wananchi Waamini Taarifa Itapunguza Rushwa

0
Taarifa kwa waandishi wa habari
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi D. Mukajanga (Katikati) akifafanua jambo.

Taarifa kwa waandishi wa habari
Septemba 13 2017
Wadau waitaka serikali kutekeleza Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa
Duniani kote, sheria za upatikanaji wa taarifa zimebadilisha uhusiano uliopo kati ya wananchi na serikali.
Wananchi wanapoelewa serikari yao inafanya nini, huweza kuchagiza maendeleo na wao wenyewe
kunufaika. Wananchi wakiwa na taarifa za kutosha huweza kuchangia ipasavyo jitihada mbali mbali za
maendeleo zenye kuleta maboresho ya jamii. Wakati mwingine, wanaweza kusaidia kufichua vitendo
vya rushwa na uovu katika jamii zao. Mara nyingi upatikanaji wa taarifa huiwezesha serikali kuhakikisha
mipango yake inaendana na hali halisi ya jamii. Pia taarifa huwasaidia watafiti kuchunguza zaidi na kutoa
ufumbuzi wa matatizo sugu yanayozikabili jamii.

Wananchi huweza kuuona umuhimu wao pale wanapoweza kufuatilia yale yanayoendelea katika jamii
zao, na kuyachukulia hatua. Jamii bora ni ile inayoendesha shughuli zake kwa uwazi, ushirikishwaji na
uwajibikaji; na yenye mifumo ya kuwapatia wananchi taarifa kwa uharaka. Jamii kama hiyo huwapa
wananchi nafasi ya kushiriki kwenye masuala ya kijamii na huwapa nafasi za kutoa mawazo yao kwa
uhuru, na demokrasia ya kuchagua viongozi wao na kuwawajibisha.

Sisi, wanachama wa umoja wa AZAKI zinazojishughulisha na masuala yahusuyo haki ya kupata taarifa,
(Coalition on the Right to Information) tunaipongeza serikali kwa mara nyingine kwa kupitisha Sheria ya
Upatikanaji wa Taarifa (2016), hususani kwa kuthamini mawazo na maoni ya baadhi ya wadau kabla ya
sheria hiyo haijapitishwa.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa kanuni zinazoratibu utekelezaji sheria hii bado hazijaandaliwa, na pia
kwamba sheria hii bado haijatangazwa rasmi katika gazeti la serikali. Sheria hii ilipitishwa mwaka mmoja
uliopita lakini mpaka sasa bado haijaanza kutumika.

Katika kuelekea Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa (Septemba 28), tunaiomba serikali ianze
hatua ya majadiliano ya kuandaa kanuni ili zikamilishwe mapema iwezekanavyo. Kwa sasa, tunaomba
serikali itangaze sheria hii kwenye gazeti la serikali wakati mchakato wa kuaandaa kanuni unaendelea.
Kwa sasa, kuna uwezekano mkubwa kwamba wananchi hawapati taarifa pindi wanapozihitaji. Mwezi
Januari/Februari mwaka 2016, watafiti, wakiwa kama wananchi wa kawaida, walitembelea ofisi 131 za
serikali. Ofisi hizi zilikuwa katika wilaya 26 na takwimu zilizokusanywa zina uwakilishi wa kitaifa.
Nia ya ziara hizi ilikuwa kutafuta taarifa fulani na watafiti hao walifanikiwa kupata taarifa za suala 1 kati
ya masuala 3 (asilimia 33) waliyokuwa wanayahitaji. Hii inamaanisha kuwa, wananchi hawapati taarifa
juu ya masuala mawili kati ya matatu wanayoyahitaji, kutoka katika ofisi za serikali. Japokuwa takwimu
hizi zilikusanywa kabla ya kupitishwa kwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, hakuna sababu ya kudhani
kuwa matokeo haya yamebadilika kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na utafiti uliopita, tungependa kujikita kwenye maeneo yafuatayo:
1. Asilimia 84 ya wananchi waliunga mkono mswada wa upatikanaji wa taarifa bungeni kabla
haujapitishwa kuwa sheria, hii inaonesha kuwa wananchi wangependa kupata taarifa za serikali.

2. Asilimia 77 ya wananchi wanaamini kuwa wananchi wa kawaida wanapaswa kupata taarifa
zinazomilikiwa na serikali.

3. Asilimia 80 ya wananchi wanaamini kuwa rushwa na matendo mengine maovu yatapungua
iwapo wananchi watakuwa na uwezo wa kupata taarifa.

Asilimia 42 ya wananchi wangependa kupata taarifa zaidi zinazohusu sekta mbalimbali kutoka
serikalini.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, anasema “Sote tunafahamu
nguvu ya taarifa. Upatikanaji wa taarifa ni muhimu sana na huwawezesha wananchi kujenga jamii ya
kidemokrasia na yenye nguvu ambapo wananchi wanaweza kuzungumza kuhusu hatma ya maisha yao.
Vyombo vya habari ni muhimu sana katika kuhakikisha suala hili linawezekana na serikali ina wajibu wa
kuweka mifumo ya sheria na sera ili kufikia lengo hili.”

“Japokuwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, 2016 ilipitishwa mwaka uliopita” anaongeza, “hakuna kitu
kikubwa kilichofanyika kuifanya sheria hiyo ianze kutumika na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa
kwa uhuru kutoka serikalini. Ni wakati sasa wa sheria hii kuanza kutumika, hususani kwa kutengeneza
kanuni muhimu kupitia njia ya mashauriano. Tofauti na hapo tunaweza kuhitimisha kwa kusema sheria
hii ni kama danganya toto tu.”

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, anasema “Upatikanaji wa taarifa ni msingi imara
katika ujenzi wa jamii ya kidemokrasia na yenye mafanikio endelevu. Kupitishwa kwa Sheria ya
Upatikanaji wa Taarifa ni moja kati ya mambo yaliyoainishwa kuwa ya muhimu mwaka 2016 na Asasi za
kiraia, vyombo vya habari na wananchi. Tunaiomba serikali ishirikiane na wadau katika kuandaa kanuni
zinazoratibu utekelezaji wa sheria hii, na pia kutangaza rasmi matumizi ya sheria hii katika gazeti la
serikali. Vilevile tunawakaribisha wananchi kuanza kuitumia sheria hii kujaribu kupata taarifa.”

Mkurugenzi wa Misa‐TAN Gasirigwa Sengiyumva, anasema, “Njia pekee ambayo nchi inaweza kutarajia
kuwa na wananchi wanaowajibika na wanaoshiriki vema katika mipango ya maendeleo ni kwa
kuhakikisha wanapata taarifa. Wananchi wenye taarifa mara zote hufanya maamuzi yenye tija.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu, Dkt. Helen Kijo‐Bisimba alihitimisha kwa
kusema, “Kila Mtanzania ana haki ya kupata taarifa za serikali. Serikali wazi na inayowajibika lazima
iwahakikishie wananchi wake uhuru wa kupata taarifa. Mwaka 2016 serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ilipitisha Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa lakini sheria hii imeacha mambo mengi yasiyo ya
kawaida ambayo yanahatarisha haki ya kupata taarifa. Kwa mantiki hii tunaiomba serikali kupitia na
kuanisha mambo hayo kuhusu Sheria ya Kupata Taarifa kabla sheria hiyo haijaanza kutumika. Baadhi ya
mambo hayo ni muda wa kusubiri kabla maombi ya taarifa kujibiwa, wananchi wa Tanzania pekee
kuruhusiwa kupata taarifa, wigo mdogo wa taarifa zinazopaswa kutangazwa, utata katika kuzuia
baadhi ya taarifa, ada kwa ajili ya kupata taarifa na mambo mengine mengi yanahitajika kupitiwa.”

‐‐‐ Mwisho ‐‐‐
Kwa taarifa zaidi wasiliana na:
Annastazia Rugaba | [email protected] | 0687 222 197
Taarifa kwa wahariri
Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa huadhimishwa duniani kila tarehe 28 Septemba. Ilianzishwa
mwaka 2003.

Leave A Reply