Twin Soul flame; tatizo sugu linalowatesa wapenzi wengi

NAKUKARIBISHA kwa moyo mkunjufu kwenye uwanja huu mzuri. Leo napenda kuzungumzia tatizo linalowatesa wapenzi na wanandoa wengi duniani kote, liitwalo Twin Soul Flame.  Yawezekana ndiyo mara ya kwanza kulisikia neno hili, lakini pengine maisha yako yote umekuwa ukiishi na tatizo hili. Ukifuatilia ndoa nyingi zinazovunjika na mapenzi yanayofika mwisho, huwa ni kwa sababu ya tatizo hili.

Kabla sijakupa tafsiri ya tatizo lenyewe, ngoja nikupe mifano kadhaa. Wiki iliyopita, nilipata bahati ya kuonana na msomaji wangu mmoja, alianza kwa kunitumia meseji akinieleza jinsi anavyoteseka ndani ya moyo wake kutokana na aina ya mapenzi aliyo nayo ndani yake.

Nilipozungumza naye kwa muda, nilimshauri tuonane na kweli akaja. Tatizo lake kubwa ni kwamba yupo kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa takriban miaka saba sasa. Lakini mwanaume aliyenaye, amekuwa akimsababishia maumivu makubwa mno ndaniya moyo wake.

Alinieleza kwamba katika kipindi chote hicho, wameshatengana zaidi ya mara nne na mwisho wakajikuta wakirudiana, wakiwa pamoja matatizo yaleyale yaliyosababisha wakatengana yanajirudia tena, mwisho wanatengana tena, wakikaa muda fulani, kila mmoja anammisi mwenzake, wakitafutana tu wanajikuta wamerudiana! Mchezo ndiyo huo kila siku.

Katika maelezo yake, alinieleza kwamba japokuwa mumewe amekuwa akimpa maumivu makali ndani ya moyo wake, wanapoelewana na kuwa pamoja, huwa anajihisi mkamilifu sana, moyo wake unatulia, ana-enjoy mapenzi kuliko kawaida. Yaani kuna muda wakikaa na kuelewana, anahisi anaimiliki dunia nzima, wanapeana mapenzi motomoto na mwenyewe anaeleza kwamba hiyo ndiyo sababu imefika mahali anajiona kama mtumwa wa mapenzi.

Tatizo ni kwamba wakianza kutofautiana, ugomvi unakuwa mkubwa mno hata kama chanzo kilikuwa ni kidogo tu, inafika mahali kunakuwa hakuna mtu anayeweza kuwasuluhisha, mwisho wanaishia kuachana.

Wanapotengana tu, dada huyu ameniambia kwamba huwa anaumia sana moyoni, anaona kama maisha yake yote yamepoteza thamani, ameshawahi kujaribu kuwa na uhusiano na watu wengine mara mbili, lakini wote aliwaona kama hawaendani naye, wanashindwa kufikia kiwango cha mapenzi anachopewa na huyu anayemsumbua, mwisho anaamua kumrudia.

Sikutaka kusikiliza upande mmoja, nilimuomba mawasiliano ya huyo mwanaume anayemsumbua na cha ajabu, naye alinieleza kitu kilekile. Kwamba anampenda sana mpenzi wake huyo na akiwa naye huwa anajiona kama dunia nzima anaimiliki yeye, lakini tatizo ni kwamba matatizo yanapoanza, huwa wanajikuta wakishindwa kuyahimili, hata kama chanzo chake kilikuwa kidogo.

Naye alinieleza kwamba amewahi kujaribu kuwa na wanawake kadhaa, lakini aliishia kuwaacha kwa sababu hawakuwa wakifikia kiwango cha mapenzi alichokuwa anapewa na huyu mpenzi wake wa siku zote. Anakiri kwamba hajawahi kupenda kama anavyompenda huyu dada, tatizo ni kwamba anamuumiza sana.

Bila shaka umeanza kupata picha aina ya uhusiano wanaoishi ndugu zetu hawa. Ukijaribu kufuatilia ni nini huwa kinawafanya watengane, hakuna sababu yoyote ya msingi, hawajawahi kufumaniana wala kufanyiana matukio makubwa! Ni mateso ya moyo tu mpaka inafika mahali wanaamua kuachana, lakini hakuna sababu yoyote kubwa.

Hili tatizo ndilo ambalo kitaalam huitwa Twin Soul Flame, unampenda sana mtu fulani, ukiwa naye unajihisi umekamilika, unamuona ndiye mtu wa ndoto zako, lakini ugomvi ukiibuka, unaumia mno ndani ya moyo wako hata kama tatizo ni dogo tu na mwisho unaamua kumpa mkono wa kwa heri.

Akienda mbali kidogo tu, unaanza kummisi sana, unajiona maisha yako hayana thamani tena na mwisho unafanya kila linalowezekana kurudiana naye. Hebu jichunguze na wewe, unaishi kwenye aina hii ya mapenzi? Wiki ijayo nitakuja kukufafanulia kwa kina, nini huwa kinasababisha hali hii na nini kifanyike ili udumu na mtu wa aina hii. Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii yenye elimu kubwa.


Loading...

Toa comment