The House of Favourite Newspapers

UCHUMBA WA SHILOLE WACHOKONOLEWA!

0
Zuwena Mohamed ‘Shilole.

RAHA ya ubuyu ni umpate mtu wa kumung’unya naye bwana! Iko hivi, ubuyu wa mjini ‘unaotrendi’ kwa sasa unanyetisha kuwa, baada ya staa wa Bongo Fleva na sinema za Kibongo, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ au ‘Shishi Baby’ kutangaza kwamba ametolewa posa, ni kwamba aliyemtolea posa hiyo ni mume wa mtu.

 

MCHUMBA’KE NI MUME WA MTU?

Chanzo makini kililimwagia ubuyu Ijumaa Wikienda kwamba, mwanaume huyo aliyemtolea posa Shilole ni mume wa mtu na inasemekana kwamba mwanamama huyo ndiye aliyemtaka jamaa huyo kwanza aachane na mkewe ndiyo waingie kwenye ndoa. “Kilichofuata, baada ya jamaa kuambiwa aamue kusuka au kunyoa, ndipo akakubaliana na Shishi, akamwacha mkewe ambaye kiukweli wametoka mbali na maisha haya. Kwa hiyo baada ya hapo ndipo wakaanza harakati za mipango yao kabambe ya ndoa,” alinyetisha mtoa ubuyu huyo.

 

NDIYO MAANA HATAKI KUMWANIKA

Chanzo hicho kiliendelea kutiririka kuwa, kudhihirisha kwamba jamaa huyo ni mume wa mtu, ndiyo maana Shilole hadi leo hajawahi kumwanika wala kutaja jina lake kwa kuogopa msala mkubwa utatokea. “Jamani si mnajua Shilole akiwa kwenye uhusiano huwa hajifichi? Huwa anapenda kuwaanika wapenzi wake kwenye ‘midia’ na mitandao ya kijamii lakini safari hii amekuwa kimya, hali inayotia shaka au kusherehesha ubuyu huu. “Ndiyo maana katika mahojiano yote aliyofanya juu ya ishu ya kupata mchumba, amekuwa akisema tu ana mchumba, lakini hataki hata kumtambulisha kwa marafiki zake wa karibu ndiyo mjue kuna kitu kinafichwa nyuma ya pazia. “Katika wapenzi wote aliowahi kuwa nao Shishi, wengi aliwaanika na majina yao yakajulikana, lakini kwa huyu imekuwa ni ngumu sana kwa sababu anadaiwa ni mume wa mtu hivyo anaogopa kuibuka kwa timbwili ikawa aibu,” alimalizia kunyetisha mtoa ubuyu wetu.

 

SHILOLE AJA JUU

Baada ya kupata ubuyu huo, Ijumaa Wikienda lilizama mzigoni, likamtafuta Shilole ambaye alikuja juu na kukanusha vikali habari hizo kwa kusema siyo kweli bali watu wamekuwa wakizungumza maneno tu wasiyoyajua na kwamba huko ni kumchokonoa na kumtafuta ubaya ambapo mambo yalikuwa hivi;

 

Ijumaa Wikienda: Shilole kuna habari kwamba mchumba wako ni mume wa mtu ndiyo maana hutaki kumwanika, hili likoje? Shilole: Jamani eeeh… naomba niseme kabisa kwamba watu wananichokonoa maana hakuna ukweli wowote juu ya hilo. Ijumaa Wikienda: Watu wanahoji kama siyo mume wa mtu ni kwa nini hutaki kumwanika? Shilole: Nasema hivi, mchumba au mume wangu siyo wa matangazo, nimebadilisha mfumo wangu wa maisha ila ipo siku nitamuonesha tu au watamuona siku ya ndoa. Ijumaa Wikienda: Wanasema mbona wapenzi wako waliopita ulikuwa unawaanika kwenye midia na mitandao ya kijamii? Kulikoni huyu wa sasa? Shilole: Ni uamuzi na mipango tu. Ijumaa Wikienda: Au uliwahi kuibiwa bwana baada ya kumwanika ndiyo maana unaogopa kumweka wazi? Shilole: Jamani, mbona watu wambeya kiasi hiki? Nimeshasema haya ni maisha yangu mapya.

 

ATUPIA PICHA, AITOA

Hata hivyo, muda mfupi baada ya mahojiano na Ijumaa Wikienda, Shilole alitupia picha ya jamaa huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo haikukaa muda mrefu kabla ya kuitoa, lakini wapenda ubuyu wakawa wameshaidaka.

 

NENO LA MHARIRI

Kama ubuyu ndiyo huo na maelezo ya Shilole tumeyasikia. Kama kweli mchumba’ke huyo ni mume wa mtu, hakuna siri chini ya jua hivyo mambo yatakuwa wazi muda si mrefu.

 

UBUYU: GLADNESS MALLYA| DAR ES SALAAM

===

Usipitwe na Matukio, Download na Install ==> Global Publishers App

Leave A Reply