Na Dk. Marise Richard | RISASI JUMATANO
LEO tunakwenda mbele zaidi kuzungumzia ugonjwa hatari wa homa ya ini au Hepatitis B ugonjwa ambao kwa bahati mbaya haujulikani na wengi licha ya kuwa madhara yake ni makubwa pengine hata kuliko saratani na Ukimwi.
Niwakumbushe waliokosa makala za nyuma ni kwamba Hepatitis B ni ugonjwa unaoshambulia ini au mfumo wa utoaji sumu mwilini unaosababishwa na virusi vya Hepatitis B (HBV).Ugonjwa huu umesababisha vifo vingi, kwa sababu tu ya kutojua. Kwa bahati nzuri ingawa hakuna tiba ya moja kwa moja ya ugonjwa huu lakini homa ya ini ina chanjo.
Pengine umewahi kusafiri nje ya nchi yako na kutakiwa kupata chanjo, miongoni mwa chanjo zinazotolewa pale mtu anaposafiri nchi za kigeni ni chanjo ya Hepatitis B. Kutokana na hatari ya ugonjwa wa homa ya ini sheria zimewekwa katika nchi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kila raia mgeni anayetaka kuingia katika nchi hizo kupata chanjo ya ugonjwa huu ili kuepusha maambukizi.
Kwa wengine, chanjo kwa ujumla ikiwamo ya homa ya ini huonekana kama usumbufu na udhia mtupu lakini yote hayo ni kutokana na kutoufahamu ugonjwa huu na madhara yake. Kwa wanaoujua wanafahamu kuwa madhara yake pengine ni makubwa zaidi kuliko hata saratani na Ukimwi na hasa kwa kuwa homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi, wenye madhara makubwa na wenye uwezo wa kuambukiza kwa wepesi kuliko Ukimwi.
Virusi vya HBV vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya ini vinaambukizwa kwa njia mbalimbali kupitia damu au majimaji ya aina yote yanayotoka mwilini zikiwemo mbegu za uzazi, mate na hata mkojo wa mgonjwa. Hali hii inaufanya ugonjwa huu uwe hatari zaidi kuliko Ukimwi kwa kuwa inatakiwa kuchukua tahadhari kubwa pale unapomhudumia mgonjwa wa Hepatitis B hali ambayo inatofautiana sana na ya mgonjwa wa Ukimwi.
HATARI KWA MJAMZITO
Maambukizi ya Hepatitis B wakati wa kujifungua ndiyo sababu kubwa ya watu wengi kupata ugonjwa huo katika nchi zinazoendelea, kwani mama mwenye homa ya ini anaweza kumuambukiza mwanaye wakati wa kujifungua. Ugonjwa huu pia huweza kuambukizwa kwa kujamiiana bila kinga au ngono zembe kama ulivyo Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa. Njia nyingine za maambukizi ya homa ya ini ni kunyonyana ndimi, kuwekewa damu isiyo salama, kuchangia vitu vyenye ncha kali kama sindano, wembe, vikata kucha na kadhalika na hata kuchangia miswaki.
HOMA YA INI KAMA UKIMWI
Homa ya ini aina ya B, inaweza kuingia mwilini mwa mtu kwa njia ya ngono, kama ilivyo Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa. Hivyo basi, majimaji katika mwili wa mwanadamu yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi. Kwa ajili hiyo kama ilivyo katika maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika ugonjwa wa Hepatitis B pia, watu wanatakiwa kuwa makini pale wanapoongezewa damu, wanapofanyiwa dialysis, tiba ya sindano au acupanture, na kuchorwa tattoo.
Kundi lingine lililoko kwenye hatari ya maambukizo ya ugonjwa huu ni wahudumu wa vituo vya afya, wauguzi, madaktari na wakunga. Hata hivyo, virusi vya homa ya ini na Hepatitis B haviwezi kuambukizwa kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kukohoa au kupiga chafya mgonjwa, mama kumnyonyesha maziwa mtoto na pia kuchangia vyombo vya kunyea na kulia chakula.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa kirusi cha homa ya ini kinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu kwa siku saba na kwa wakati huu, kirusi hiki kinaweza kusababisha maambukizi iwapo mtu hajapata chanjo ya kuuzuia. Kwa ajili hiyo watu wengi bila kujua wamekuwa wakiugua ugonjwa wa homa ya ini bila kufahamu hali ambayo husababisha ini kuathirika taratibu.
Homa ya ini aina ya B inaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote, huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Zinapoonekana, huenda tayari ini limenyauka au lina saratani na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na virusi vya HBV.
Ijapokuwa maambukizi ya awali hutokea katika ini lakini virusi vya HBV husambaa mwilini kupitia damu. Virusi vya Hepatitis B husababisha maambukizi ya haraka mara 50 hadi 100 zaidi kuliko Ukimwi.
DALILI
Dalili za ugonjwa huu huchukua muda mrefu kuonekana, na pindi zinapoonekana kwa kawaida zikionekana mgonjwa huwa tayari ameshaathirika sana na ni kama zifuatavyo; kuhisi uchovu, kichefuchefu, mwili kuwa dhaifu, homa kali, kupoteza hamu ya kula, kupungua uzito, maumivu makali ya tumbo upande wa ini, macho na ngozi kuwa njano na mkojo mweusi.
Ugonjwa sugu wa homa ya ini husababisha uharibifu mkubwa wa seli za ini au cirrhosis na pia kansa ya ini ugonjwa ambao ni vigumu kutibika. Pindi ugonjwa wa homa ya ini unapokuwa sugu mwilini na kuharibu sana mfumo wa utoaji sumu mgonjwa huweza kuhisi kuwashwa mwili.
Punde baada tu ya kuambukizwa virusi vya HPV, dalili pia huonekana lakini dalili hizo hupotea taratibu baada ya wiki kadhaa kwa watu wengi. Wachache kati ya walioambukizwa, virusi hivi hupata vidonda kwenye ini na matatizo makubwa ya ini ambayo husababisha kifo.
Lakini kwa baadhi ya waathiriwa virusi hubakia mwilini na mgonjwa kubakia bila dalili na matatizo yoyote. Maambukizi ya muda mrefu ya ugonjwa wa Hepatitis B huweza kuwa na dalili au bila dalili na baada ya miaka kadhaa kuambatana na uharibifu mkubwa wa seli za ini au kansa ya ini.
Magonjwa ya Hepatitis B na C yanakadiriwa kuwa ndiyo chanzo cha kansa ya ini kwa asilimia 50. Wagonjwa wenye virusi vya HBV mwilini vinavyosababisha ugonjwa wa ini ambao hawana dalili lakini wana uwezo wa kuambukiza wengine au chronic carries hushauriwa kutokunywa pombe kwani husababisha wawe kwenye hatari ya kupata cirrhosis na kansa ya ini.
Watu walio katika makundi ya hatari ya kupata Hepatitis B hushauriwa kupima ugonjwa huu ili kama watapatikana na virusi vya HBV mwilini waanze matibabu mapema na kubadilisha staili yao ya maisha ili kupunguza kasi ya kuharibika ini. Watu wanaoshauriwa kupima ugonjwa wa huo ni wale wanaoishi na watu walioambukiwa Hepatitis B,wale waliokuwa na mahusiano ya kimwili na mtu mwenye Hepatitis B na wale ambao vipimo vyao vya vimeng’enya vya ini au Liver Enzymes Tests vinatia wasiwasi.
Pia wengine ni wale wanaoishi au kutoka katika maeneo na nchi ambazo kuna maambukizo makubwa ya homa ya ini kama katika baadhi ya nchi za chini ya Jangwa la Sahara Barani Afrika, Asia na Ulaya Mashariki.Wanaojidunga dawa za kulevya, wajawazito na wale wanaotumia dawa za kudhoofisha mfumo wa kulinda mwilini.
Kwa bahati mbaya ugonjwa huo wa Hepatitis B unapewa uzito mdogo kwenye nchi nyingi zenye maambukizo makubwa licha ya kuwa ni wenye hatari kubwa. Inakadiriwa kuwa robo tatu ya watu ulimwenguni wameathiriwa kwa muda na homa ya ini lakini bila kuonesha dalili na wengine milioni 350 wako katika maambukizo ya muda mrefu hali ya kuwa ugonjwa huo hauwadhuru lakini ni wenye kuwaambukiza wengine hali ambayo kitaalamu tunaiita chronic carrier. Takwimu zinaonyesha kuwa homa ya ini huua watu 600,000 kila mwaka katika sehemu mbalimbali duniani, idadi ambayo ni sawa na ya wanaokufa kwa malaria.
Virusi vya HBV vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya ini vinaambukizwa kwa njia mbalimbali kupitia damu au majimaji ya aina yote yanayotoka mwilini zikiwemo mbegu za uzazi, mate na hata mkojo wa mgonjwa.
Hali hii inaufanya ugonjwa huu uwe hatari zaidi kuliko Ukimwi kwa kuwa inatakiwa kuchukua tahadhari kubwa pale unapomhudumia mgonjwa wa Hepatitis B hali ambayo inatofautiana sana na ya mgonjwa wa Ukimwi.
Itaendelea wiki ijayo.