visa

USIPIME! VITA YA GOLDEN BOOT ENGLAND MSIMU HUU

Sergio Leonel “Kun” Agüero Del Castillo ‘Sergio Agüero’.

BAADA ya mechi nne za Ligi Kuu England, tayari vita ya kuwania tuzo ya ufungaji bora ya Golden Boot imeanza kushika kasi mapema.

 

Katika usajili wa safari hii, timu nyingi za Ligi Kuu England ziliwekeza katika kupata wafungaji wazuri wa kuwafungia mabao mengi.

Dalili zinaonekana kutakuwa na vita kali ya kuwania tuzo ya mfungaji wa bora wa ligi kwa msimu huu wa 2019/20.

Zamani tuzo hii ilikuwa inashindaniwa zaidi na sentafowadi lakini katika miaka ya karibuni kuna mawinga wameonyesha ukali katika kufunga.

 

Pia kuna mafowadi kama Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, ambao siyo masentafowadi hasa lakini wapo moto katika kupachika mabao mara zote.

 

Timu safari hii zimejitahidi sana kuwekeza katika kusajili mafowadi mathalani West Ham wapo vizuri mbele.

Pia kuna Everton, ambayo ina safu nzuri ya ushambuliaji inayoundwa na Dominic Calvert-Lewin, Cenk Tosun na Omar Niasse.

 

Msimu uliopita kulikuwa na ushindani mkali sana wa kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu England, ambapo mastaa watatu walifungana, Mohamed Salah na Sadio Mane (Liverpool) na Pierre- Emerick Aubameyang wa Arsenal, ambao wote walipachika mabao 22 kila mmoja.

 

Kuna uwezekano mkubwa hali hiyo ikajitokeza tena katika msimu huu wa 2019/20.

Kuna mastaa watatu, ambao sasa wameanza kwa kasi mbio za kuwania ufungaji bora msimu huu.

 

SERGIO AGUERO (MANCHESTER CITY) – 6

Aguero ameonyesha dalili mapema kuwa anatengeneza mazingira ya kuwa mfungaji bora safari hii.

Staa huyo wa Argentina ndiye anaongoza akiwa tayari ametupia mabao sita.

Na rekodi zake za Ligi Kuu England zinamfanya awe ni mtu wa kuchungwa msimu huu.

Kwani staa huyo tangu ajiunge na Manchester City mwaka 2012 amekuwa moto likija suala la kupachika mabao.

Aguero sio mtu wa kumwachia nafasi ndani ya boksi kwani analijua goli vizuri.

 

Msimu huu akiendelea na kasi hii basi anaweza kufunga mabao 20 na zaidi kiasi cha kujiweka kuwa katika nafasi nzuri ya kuwa mfungaji bora.

 

 

Hata hivyo, ana mtihani wa kufikisha idadi hiyo kwani kocha wake, Pep Guardiola huwa ana tabia ya kuwabadilisha na sentafowadi mwenzake Gabriel Jesus,

Guardiola huwa hapendi kuwapanga katika kikosi kimoja Aguero na Jesus.

 

Bado Aguero atatupia mabao mengi kwani uzuri Manchester City ina wachezaji wa kiungo na mabeki wenye uwezo wa kutoa asisti nyingi.

Pia Aguero anapaswa kuombea asipatwe na majeruhi yatakayomfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

 

 

RAHEEM STERLING (MANCHESTER CITY) – 5

Winga Sterling naye ameanza kwa kasi msimu huu kwa kutupia mabao mengi.

Staa huyo, ambaye aliteuliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo wa England kama mwanasoka bora msimu uliopita, alikuwa amezoeleka kwa kutoa asisti nyingi.

 

Safari hii yupo moto, ambapo tayari ameshatupia mabao matano kwenye mechi za Ligi Kuu England kiasi cha kuchuana mapema na staa mwenzake wa City, Aguero.

Kiwango chake kimepanda kwa kasi kubwa katika miaka ya karibuni baada ya kushutumiwa vikali katika miaka ya nyuma.


Sterling kwa sasa yupo vizuri sana kiasi ambacho ni kati ya wachezaji ambao wanaaminika na Guardiola.

Winga huyo ni kati ya mastaa wa wachache waliokuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha Manchester City akiwa pamoja na Aymeric Laporte, Ederson, Kevin De Bruyne na Kyle Walker.

Sterling anatisha kutokana na kuwa na mbio, uwezo mkubwa wa kupiga  chenga na kujua kujiweka katika nafasi nzuri za kufunga.

Tayari anatisha msimu huu akiwa amepachika mabao matano katika mechi za ligi.


TEEMU PUKKI (NORWICH CITY) – 5

Straika wa Norwich City, Pukki ameanza kwa kishindo kwenye Ligi Kuu England baada ya kupanda daraja na timu yake,

Ameendeleza makali yake baada ya kutamba na Norwich City kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita.

Pukki mwenye umri wa miaka 29 naye amepachika mabao matano katika mechi nne za Ligi Kuu England,

Staa huyo wa Finland, miongoni mwa mabao yake ya ligi ni hat-trick aliyopiga kwenye mechi dhidi ya Newcastle.

Straika huyo ametajwa kwenye listi ya kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu England kwa mwezi wa Agosti.
Toa comment