Vijana 1,000 Kunufaika Na Ajira Zitokanazo Na Utekelezaji Wa Mradi Wa Ujenzi
Zaidi ya vijana 1,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira zitokanazo na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha- Kibaya – Kongwa yenye urefu wa kilometa 453.42, inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia utaratibu wa Engineering Procurement Construction plus Financing (EPC+F).
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Mbaraka Batenga ameeleza hayo hivi karibuni alipozungumza na wananchi pamoja na timu ya watalaam wa barabara kutoka TANROADS Makao Makuu wakiongozwa na Meneja wa Miradi ya PPP na EPC +F Mhandisi Harold Kitainda walipotembelea mradi huo ikiwa ni hatua za awali za kuanza rasmi ujenzi wa mradi huo.
Amesema mbali na ajira hizo faida nyingine za mradi huo utakapokamilika utaondoa changamoto ya Usafiri wa barabara na hivyo kuwasaidia Wananchi kuchochea shughuli za kilimo na ufugaji kwa kuwa na usafiri wa haraka hasa kwa kuzingatia kuwa Wilaya hiyo inazalisha zaidi ya tani 150,000 za Alizeti, mahindi zaidi ya tani 250,000, Ngombe zaidi ya 500,000, mbuzi 480,000 na Kondoo idadi hiyo hiyo, uzalishaji ambao unahudumia mikoa mbalimbali hapa nchini pamoja na nchi za jirani.