
Wafanyakazi wa kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing nchini Marekani, wameendelea na maandamano wakipinga ongezeko dogo la mshahara kwa asilimia 35 katika kipindi cha miaka minne.
Imeshuhudiwa wafanyakazi zaidi ya 30,000 wakijiunga na maandamano hayo yaliyoanza tangu Septemba 13, huku bosi wa kampuni hiyo, Kelly Ortberg akionya kuwa maandamano hayo yamesababisha hasara ya dola bilioni 6 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 16.36 za Kitanzania.
Baadhi ya wafanyakazi wamelamikia kulipwa kiwango cha chini ya dola 28 za Kimarekani kwa saa ambacho ni sawa na shilingi 76,284 za Kitanzania wakidai hakiendani na kazi wanayofanya. Kwa mujibu wa BBC kampuni ya Boeing imekataa kutoa maoni kuhusu kukataliwa Kwa ofa yake ya hivi karibuni.

Hii ni mara ya pili kwa wafanyakazi wa Kampuni hiyo, kufikia hatua ya kugomea mpango uliopendekezwa katika kura rasmi. huku ofa ya awali ilikataliwa mwezi uliopita na asilimia 95 ya wafanyakazi.
Hapo awali Ortberg, ambaye alichukua nafasi ya afisa mkuu mtendaji mwezi Agosti, alisema amekuwa akifanya kazi kwa bidii sana ili kuimarisha kampuni hiyo, huku ikijaribu kurekebisha sifa yake, ambayo imeathiriwa na matatizo ya uzalishaji na usalama.
Mapema mwezi huu Kampuni hiyo ilitangaza mpango wa kupunguza takriban 10% ya wafanyakazi wake, huku maelfu ya wafanyakazi wengine tayari wako kwenye likizo kutokana na mgomo, ambao pia umeathiri shughuli za usambazaji.