×

Wafungwa 68 Wauawa

Takriban wafungwa 68 wameuawa kwenye mapigano mapya katika gereza la Ecuador. Ghasia katika gereza la Litoral katika mji wa Guayaquil inasemekana zilianza Ijumaa jioni. Ripoti zinasema Polisi ambao wameingia kwenye majengo ya magereza wamekuta bunduki na vilipuzi.

 

Zaidi ya wafungwa 100 walikufa katika mapigano kati ya magenge hasimu mwezi Septemba, na takriban wafungwa 300 wamefariki kufikia sasa katika magereza ya nchi hiyo ndani ya mwaka huu. Vurugu za Septemba zinazohusiana na genge zilikuwa mbaya zaidi katika historia ya Ecuador.

 

Wakati huo, wafungwa kutoka upande mmoja wa gereza walitambaa kupitia shimo ili kufika upande mwingine ambapo walishambulia genge pinzani. Mamia ya maafisa na askari wa jeshi walitumwa kurejesha udhibiti wa eneo hilo.

 

Mapema mwezi huu, Rais Guillermo Lasso alisisitiza kuwa serikali yake inarejesha udhibiti sio tu wa magereza bali pia maeneo ya Ecuador ambako walanguzi wa dawa za kulevya wamejidhihirisha.

 

Maafisa wanasema Magereza ya Ecuador kwa sasa yanachukua wafungwa wapatao 9,000 zaidi ya idadi stahiki. Gereza la Litoral liliundwa kwa ajili ya wafungwa 5,300 lakini kwa sasa lina wafungwa 8,500.

Leave a Comment