The House of Favourite Newspapers

Waliotaka Kumteka Tarimo, Mikononi Mwa Polisi, “Wanane Tumewakamata”-Muliro

0

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa  kukamata kundi la wahalifu wanane wanaotuhumiwa kula njama kwa pamoja na baadae kufanya tukio la kumteka Deogratius Tarimo.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema Novemba, 11/ 2024 eneo la Kiluvya Ubungo Dar es Salaam lilitokea tukio la  kutekwa kwa Bw. Deogratius Tarimo, mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani.

Kufuatia tukio hilo na mengine ya nyuma Polisi Dar es salaam imekuwa ikiendelea kuchunguza na kufuatilia taarifa mbalimbali  pia kukusanya ushahidi wa kisheria kuhusiana na matukio hayo ili kuyazuia.

Aidha amesema Watuhumiwa wa tukio hilo wamekamatwa kwa nyakati tofauti Dar es salaam, Songea Ruvuma  na eneo la Mbingu Mlimba Morogoro ambapo lilipatikana gari aina ya Toyota Raum ambayo ilitumiwa wakati wa tukio hilo huku ikitumia namba isiyo halisi T 237 EGE na baada ufuatiliaji namba halisi ya gari hiyo ni T237 ECF.

Amewataja Watuhumiwa hao kuwa ni Bato Bahati Tweve, Bondia, Miaka 32, Mkazi wa Kimara Bunyokwa na Songwe Mbozi, Yusuph Abdallah, Miaka 32, Mkazi wa Mbingu – Mlimba Morogoro, Fredrick Juma, Miaka 31, Mkazi wa Kibamba, Nelson Elimusa @ msela, Dereva Tax, Miaka 24, Mkazi wa Mbezi Luguluni, Benk Daniel Mwakalebela@tall , Miaka 40, Mkazi wa Mbezi Makabe na Kyela Ipinda Rusungo  Mbeya, Thomas Ephraim Mwakagile @ baba mage ,  Miaka 45, Mkazi wa Kinyerezi Bonyokwa na Kyela Ngonga Ndiali Mbeya, Anitha Alfred Temba,  Miaka 27, Mkazi wa Mbezi Mwisho, Isack Mwaifani, @ boxer , Mkazi wa Kimara Tembo Salanga na Bujonde Isanga Kyela Mbeya.

Amesema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linaendelea na kazi ya  kuzuia vitendo vya kihalifu lakini pia kuwakamata na kutokuwa na huruma kwa watuhumiwa wote wanaojihusisha na matukio ya kihalifu ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria kwa  kuwapeleka kwenye mamlaka zingine za haki.

Hata hivyo amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote  kuendelea kutoa taarifa za kweli ili Jeshi lichukuwe hatua za kisheria kwa watu wanaopanga kufanya  matukio ya kihalifu ili washughulikiwe mapema kabla ya matukio.

 

Leave A Reply