The House of Favourite Newspapers

WALIPOJIFICHA WAPINZANI WA TAIFA STARS

FAINALI za Afcon msimu huu zinaanza Juni 21, mwaka huu, kuanzia sasa kwenye miji mbalimbali ya Misri ikiwemo hapa Cairo tayari timu mbalimbali zimshaanza kuwasili. Tanzania na Zanzibar zitawakilishwa na Taifa Stars iliyopo kundi C.

 

Ndani ya kundi hilo wamo Algeria, Senegal na Kenya ambao wanajinoa kwelikweli. Stars imeanza maandalizi tayari imeshafika kambini nchini Misri kwa kujinoa zaidi na kucheza mechi kadhaa za kirafi ki ikiwemo dhidi ya mwenyeji ambaye hayuko nae kundi moja.

 

Mechi zote za Stars kwenye fainali hizo za Afcon zitachezwa usiku kwa muda wa saa za Tanzania. Mechi ya kwanza na Juni 23, ni saa 1 usiku, inayofuata na Kenya saa 3 usiku na ile ya mwisho ya makundi na Algeria saa 4 usiku. Mechi zote zikipigwa hapa Cairo.

 

Spoti Xtra ambalo ndilo Gazeti linalouzika zaidi kila Alhamisi na Jumapili, linakuonyesha walikojifi cha wapinzani wa Stars na wanachokifanya;

 

KENYA

Hawa ni majirani zetu, wao wako nchini Ufaransa wakijinoa kwenye Uwanja wa Shirikisho la Ragby la Ufaransa. Mastaa wao sita wanaocheza nje tayari wameshawasili.

 

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imeteua wachezaji 27 na watu 12 wa benchi la ufundi na viongozi saba na watakuwa kambini wiki tatu. Miongoni mwa majina makubwa yaliyoko kwenye kambi ya Kenya ni Eric Johanna, Ovella Ochieng, Eric Ouma na Victor Wanyama.

 

Itacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Madagascar kesho Ijumaa jijini Paris na DR Congo watachuana nayo Juni 15 huko Madrid, Hispania. Watatua Cairo, Juni 19. Mechi zao za Afcon watachezea kwenye Uwanja wa 30 June. Kenya itaanza na Algeria Juni 23, dhidi ya Stars Juni 27, kabla ya kumalizana na Senegal Julai 1.

 

SENEGAL

Achana na bajeti yao, wametenga mabilioni ya shilingi. Wako kambini nchini Hispania na watakaa hapo kwa siku 17.
Kocha wao Aliou Cisse, ametaja majina 25 yakijumuisha risasi yake ambayo ni straika wa Liverpool, Sadio Mane. Watacheza mechi ya kirafi ki dhidi ya Nigeria Juni 16 kwenye Uwanja wa Ismailia.

 

ALGERIA

Walikuwa wanajinoa Jijini Algiers lakini Jumamosi walitua kambini Qatar tayari kuweka sawa nondo zao. Senegal na Algeria ndio timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kuchukua nafasi mbili za juu kwenye kundi huku Stars ikitabiriwa ya tatu ingawa Mbwana Samatta amesema tutashangaza.

 

Algeria ina mchezaji mmoja tu anayecheza ligi ya ndani kwenye kikosi hicho ambaye ni Hicham Boudaoui. Wana watu kama kina Riyad Mahrez (Manchester City, England) na Islam Slimani (Fenerbahce, Uturuki).

Comments are closed.