Wananchi 18,674 Kunufaika na Mradi wa Maji Igawa Malinyi
Wananchi 18,674 kutoka vijiji vitatu vya Igawa, Ligala na Kiwale katika Kata ya Igawa wilayani Malinyi mkoani Morogoro wanatarajiwa kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi baada ya serikali kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 800.
Ukosefu wa huduma ya maji safi na salama ni changamoto kubwa kwa wakazi wa Kata ya Igawa, wengi wao wakilazimika kutumia maji ya mtoni kwa shughuli zao za kijamii ikiwemo kunywa na kupikia na kujikuta wakipata maradhi mbalimbali ikiwemo ya tumbo na kuhara.
Wakazi hao wanasema ni muda mrefu sasa huduma ya maji wameikosa, ombi lao kwa serikali ni kuharikisha mradi huo wa maji kwani ndiyo tegemeo lao kwa sasa.
Ili kuondokana na changamoto hiyo, tayari serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wameanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji kijijini hapo, lengo likiwa ni kuwafikia wakazi wote wa Kata ya Igawa.
Mhandisi Marco Chogero ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Malinyi ambapo amesema zoezi lililobaki ni kutandaza mabomba kuwawezesha wanachi kupata huduma ya maji safi na salama.
Juhudi hizo zinaisukuma Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (ССМ) Mkoa wa Morogoro kufika na kujionea namna mradi huu utakavyonufaisha wananchi.
Ujenzi wa mradi wa maji Igawa ulianza Januari 7, 2022 na unarajiwa kumalizika Oktoba 30, 2024 na kuwezesha kukamilisha kauli mbiu ya RUWASA ya Maji Bombani.