The House of Favourite Newspapers

YAJUE MAGONJWA YENYE UHUSIANO NA UKIMWI

WENGI tunajua tatizo la Ukimwi; kirefu chake ni Upungufu wa Kinga Mwilini, ni ugonjwa unaoshambulia na kuua chembe chembe nyeupe za damu zinazosaidia mwili kupambana na magonjwa.  Kutokana na upungufu huu wa kinga, magonjwa nyemelezi huanza kumpata muathirika wa Ukimwi sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo eneo la kinywa na uso. Ni vema leo tukaangazia juu ya magonjwa ya eneo la kinywa na uso.

MAGONJWA YA FIZI

Kwa kawaida magonjwa ya fizi huwapata watu wasiopiga mswaki au wanaopiga mswaki isivyopaswa. Mara nyingi mtu mwenye magonjwa haya hutokana na meno yakiwa na tando za uchafu na wadudu au hata ugaga uliojishikiza kwenye meno kama miamba. Lakini kwa mgonjwa wa ukimwi unaweza kukuta kinywa ni kisafi lakini fizi zimejaa vidonda ambavyo husambaa kwa kasi.

Magonjwa haya ya fizi hushambulia pia mifupa inayoshikilia mizizi ya meno hivyo kusababisha meno kulegea na hatimaye kutoka. Matibabu yake ni kusafisha meno na kutumia dawa za antibiotic za kusukutua na vidonge vya kumeza.

FANGASI MDOMONI

Ugonjwa huu hujidhihirisha kama utando mweupe kwenye ulimi, paa la kinywa au kuta za kinywa. Utando huu ni rahisi kukwanguliwa na kuacha ngozi laini yenye vipelevipele vyekundu. Wakati mwingine huonekana kama vipele vipele vyeupe kwenye kinywa.

TIBA YAKE

Ugonjwa huu hutibika kwa kutumia dawa za kawaida za fangasi ama za vidonge, za maji au za kumun’gunya katika hali ya gel.

KUVIMBA TEZI JIRANI NA SIKIO

Huku ni kuvimba hadi kuonekana kwa tezi la mate lililopo jirani ya sikio. Kwa kawaida tezi hili halionekani, hivyo ukiliona limevimba jua kuna tatizo. Ugonjwa huu huenda sambamba na kukauka kwa kinywa, kwani matezi haya ndiyo hutoa kiwango kikubwa cha mate mdomoni. Unaweza kuvimba tezi la upande mmoja au pande zote mbili. Ugonjwa huu huweza kujiponea wenyewe lakini wakati mwingine yaweza kuhitaji matibabu.

KUVIMBA MITOKI CHINI YA KIDEVU, SHINGO

Kama nilivyosema hapo juu, katika hali ya kawaida mitoki haionekani na wala huwezi kuihisi kwa kugusa. Ukiweza kuiona kwa macho kuwa imevimba au hata ukaweza kuihisi kwa kugusa hiyo ni dalili kwamba mitoki imevimba. Mbali ya majeraha na vidonda eneo la kinywa na uso mitoki hii pia huweza kushambuliwa na kansa ya karposi’s sarcoma au hata TB, lakini wakati mwingine inavimba tu bila sababu zilizo wazi. Mitoki hii huweza kupona bila matibabu, lakini wakati mwingine matibabu yanatakiwa.

Comments are closed.