The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 49

ILIPOISHIA:

Ilibidi asimame kidete kuhakikisha yeye ndiye atakayesimamia kila kitu. Baada ya mama yake kupata nafuu alitolewa hospitali na kufanyika taratibu zote na baba yake alizikwa.

SASA ENDELEA…
Baada ya mazishi alibakia na maswali yasiyo na majibu kuhusu mzazi mwenzie Ambe ndiye mhusika wa kifo cha baba yake japo alimuahidi angefanya kitu kama kile

***
Baada ya kumaliza kazi ya kumuua mzee Mtoe kwa njia nyepesi tofauti na walivyotarajia walirudi kijijini kwao na kujipanga kwa ajili ya maisha mapya.
“Nina imani kazi imekwisha,” Mabina alimwambia Ambe aliyekuwa amejilaza kwenye mkeka.
“Ni kweli rafiki yangu, nashukuru kwa msaada wako.”
“Kwa upande wangu sikufurahi kumuua yule mzee kistaarabu namna ile.”
“Sasa tungefanyaje?”
“Yule mzee alitakiwa kumuua kwa zaidi ya risasi zote zilizokuwa kwenye magazini.”
“Hatukuwa na jinsi tungefanyaje kwani Koleta angesikia.”
“Ningekuwa nimepanga mimi Koleta angeshuhudia kifo cha baba yake cha risasi nyingi ambacho asingekisahau.”
“Lakini kumbuka Koleta naye alikuwa na mpango wa kutaka kumuua baba yake.”
“Tungemtegemea angetuchelewesha watoto wa kike wana huruma sana, angeweza kubadili mawazo na kuwa upande wa baba yake.”
“Asingeweza, Koleta namjua mimi.”
“Nafikiri la muhimu tumemaliza tunatakiwa tujipanga kwa maisha mapya.”
“Kwa hiyo itakuwaje lazima niwe karibu na mpenzi wangu.”
“Sikiliza mpaka sasa hivi wewe ndiye unayetafutwa mwenzako nimekwishakufa hakuna wa kunitafuta.”
“Kwa hiyo?”
“Tutakaa shamba kutembea kwetu usiku kwa muda wa miezi sita ili wanaokutafuta wakate tamaa. Nina imani wataendelea kuweka mitego kwa Koleta ili kukunasa lakini wakikukosa watakata tamaa na kutupa nafasi ya kurudi tena wakiamini tumekimbia.”
“Siwezi kuwasiliana na Koleta hata kujua hali ya mwanangu?”
“Ambe sasa hivi kwanza tunaokoa nafsi zetu hatutakiwi tujulikane tupo ikiwa ni pamoja na kumchanganya mpenzi wako asijue nani amefanya tukio lile.”
“Lazima atajua ni sisi kwa vile tulimuuliza alipolazwa baba yake.”
“Hata akiwa na wasiwasi na sisi kupotea kwetu kutamchanganya, kwa muda tutakaopotea utamchanya sana.”
“Kwa hiyo unanishauri tusiwasiliane naye kwa miezi sita.”
“Ndiyo.”
“Basi mimi nipo tayari.” Walikubaliana kutoonekana mchana kwa miezi sita wala kuwasiliana na Koleta.

***
Mwezi moja baada ya kifo cha mzee Mtoe, Koleta alikuwa akijiuliza Ambe atakuwa wapi na kwa nini toka alipoulizia hospitali aliyolala baba yake hajaonekana tena. Swali lingine lilikuwa nani aliyemuua baba yake aliamini kabisa kifo cha baba yake kilifanywa na mtu anayemfahamu tena kwa kisasi. Swali likabaki nani aliyefanya vile? Alijiuliza Ambe atakuwa wapi na kwa nini muda wote huo hajampigia simu. Muda nao uliyoyoma akiamini atapata taarifa zozote za mpenzi wake, lakini muda uliyoyoma bila kupata taarifa zake. Baada ya arobaini ya baba yake alianza kazi kwenye duka lake akitegemea kuna siku moja Ambe angeonekana lakini miezi ilikatika na kuamini huenda alikufa siku ya tukio la kuzimwa taa.Akiwa na msichana wake wa kazi dukani alijikuta akijiuliza maswali mengi juu ya kupotea kwa mpenzi wake Ambe. “Ester nina wasiwasi baba Junior amefariki.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Huu mwezi wa ngapi, si kawaida yake huenda alipigwa risasi na polisi.”
“Dada Ambe amekufa lini ikiwa siku moja kabla ya kifo cha baba alipiga simu?”
“Ester lazima baba Junior atakuwa amekufa, kama yupo hai yupo wapi?”
“Kama amekufa simu ile alipiga nani?”
“Ni ya muuaji aliyeigiza sauti ya Ambe ili tumpe siri sehemu alipolazwa baba.”
“Na namba yako nani kampa?”
“Hapo ndipo ninapochanganyikiwa.”
“Dada yule ni baba Junior kabisa.”
“Kama ni yeye sasa yupo wapi?”
“Labda baada ya kulipa kisasi amekwenda kutafuta maisha mbele kwa kukuhofia kumpeleka polisi.”
“Japo kifo cha baba yangu kinaniuma lakini nisingethubutu kumtenda kwa vile yeye kwangu ni kila kitu.”
“Kama amekufa utafanya nini? Japo naamini ni mzima wa afya njema.”
“Naapa sitaolewa na mwanaume mwingine nitamtunza mwanangu kama mwanangu baba na ndiye atakayekuwa mume wangu.”
“Dada kwa nini ujitese hivyo kwa nini usimpe nafasi nyingine yule mchumba wako?”
“Ester siwezi nina imani nina dhambi kubwa kuchangia kifo cha Ambe, alikataa lakini nilimhakikishia usalama wake na matokeo yake yakamtokea yale.”
“Dada kwa nini unamuua Ambe wakati tumezungumza naye, ile ni sauti yake wala si ya mtu mwingine.”
“Kama yake sasa yupo wapi?”
“Huenda bado hakuamini hivyo inawezekana usimuone kabisa kwa kweli kama mlikubaliana na kitendo mlichomtendea kilikuwa kibaya.”
“Ester, mimi au baba mzee yule alikuwa mbishi sana.”

***
Baada ya miezi sita kukatika Koleta aliamini kabisa aliyepiga simu kuulizia habari za baba yake hakuwa Ambe bali mtu mwingine aliyeigiza sauti kama yake ili kujua marehemu baba yake yupo wapi lakini mwenyewe ameshakufa. Pamoja na kutiwa moyo na Ester kuwa Ambe mzima hata ile sauti haikuwa ya kuigiza bali ya kwake kweli bado hakukubaliana naye kwa kuamini kama angekuwepo lazima angemtafuta hasa baada ya kutafutana kwa muda mrefu huku wakipeana ahadi za kutenganishwa na kifo.
“Ester unabisha tu, lakini Ambe amekufa,” Koleta alishikilia msimamo wake.
“Dada acha kumuua mpenzi wako nina imani bado yupo hai ipo siku ataonekana akiwa hai.”
“Siku gani hebu angalia huu mwezi wa ngapi tangu kifo cha baba, nina imani baada ya kifo cha baba hakukuwa na kipingamizi kingine zaidi ya kujitokeza ili tuishi maisha mapya ya mke na mume mama hana pingamizi.”
“Da’ Koleta nina imani huenda Ambe hakuamini tena na kukuona wewe na familia yako lenu moja la kumpoteza.”
“Ester usiseme hivyo, nafikiri unajua kiasi gani ninavyompenda Ambe hata nilikuwa radhi kumuua baba yangu.”
“Tena kweli Da’ Koleta, wewe hukumuua baba?”
“Nimuue ili?”
“Kwani ulipoapa utamuua ulitaka kumuua ili iweje?”
“Kutimiza kile nilichomuahidi kama akinigeuka, lakini yale yalishapita ilikuwa ni hasira tu, lakini baba yangu nilikuwa nampenda sana pamoja na ubishi wake.”
“Unampenda vipi nawe uliapa utamuua kwa mkono wako?”
“Kwa hiyo unataka kuniambia mawazo yako yamekutuma mi ndiye muuaji?”
“Kwa mawazo yangu japo Mungu atanisamehe kukuwazia hivyo.”
“Kwa nini Ester umeniwazia hivyo?”
“Da’ Koleta unakumbuka siku chache baada ya kusema utamuua baba, kilitokea kifo cha baba kibaya zaidi wewe ndiye uliyekuwepo hospitali. Baada ya kujua kuwa wewe ndiye uliyempokea mama na siku hiyohiyo kifo cha baba moja kwa moja nilijua umetimiza dhamira yako.
“Kwa kweli pamoja na kulia sana niliamini moyoni unachekelea kumuua baba yako kwa ajili ya mwanaume ambaye anaweza kukugeuka wakati wowote.”

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.