×

Dunia Uliyoiacha Nyuma – 51

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.

Upelelezi unaendelea na tayari mke wa Magesa amepatikana na sasa anahojiwa kwa kina. Magesa na Grace wamewasili sehemu ambayo mwanaume huyo haijui.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Waliendelea kutembea mpaka walipofika nje ya uwanja ambapo Grace alinyoosha mkono kumuita mmoja kati ya madereva wengi wa pikipiki za matairi matatu waliokuwa nje ya uwanja huo wakisubiri abiria. Akawasha pikipiki yake na kuisogeza mpaka jirani na pale Grace na Magesa walipokuwa wamesimama.

Grace akazungumza naye kwa lugha ambayo Magesa hakuielewa kisha akampa ishara kwamba wapande. Wakapanda na kukaa kwenye siti zilizokuwa zimepambwa huku muziki mkubwa ukiwaburudisha.

“Huku hizi ndiyo kama teksi? Naona zilivyojaa barabarani.”

“Huu ndiyo usafiri mkubwa wa huku, wenyewe wanaita ‘tuk-tuk’,” alisema Grace huku akiachia tabasamu pana usoni kwake, safari ikaendelea huku Magesa akiwa bize kushangaa mandhari ya mji huo ambao mpaka muda huo hakuwa anajua unaitwaje.

Muda mfupi baadaye, pikipiki waliyopanda ilisimama mbele ya geti kubwa jeusi, Grace akafungua pochi yake ndogo na kutoa fedha, akamlipa yule dereva na kumpa ishara Magesa kwamba washuke.

Yule dereva wa pikipiki alipogeuza na kuondoka, Grace alifungua begi lake alilobeba na kutoa funguo, akafungua geti hilo na kumkaribisha ndani Magesa ambaye bado alikuwa anashangaa-shangaa.

“Whaoo! Pazuri sana hapa, halafu kuna upepo mzuri wa bahari,” alisema Magesa huku akishangaa bustani nzuri zilizokuwa ndani ya uzio wa nyumba hiyo. Grace hakumjibu kitu, akamuongoza kuelekea kwenye mlango mkubwa wa kuingilia ndani ya nyumba hiyo, akafungua na kuingia ndani.

Kama ilivyokuwa Mombasa, Kenya, nyumba hiyo ilikuwa imekamilika kwa kila kitu, ndani kukiwa na samani nyingi za kisasa huku picha kubwa ya Grace ikiwa imetundikwa ukutani.

“Tutakaa hapa kwa siku kadhaa wakati nikikamilisha kazi iliyonileta. Tupo kwenye Kisiwa cha Marie Louise, Shelisheli,” alisema Grace na kusababisha Magesa akodoe macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.

Kwa hiyo kumbe una makazi pia Shelisheli? Grace mbona una mambo makubwa kiasi hiki?”

“Kazi zangu ni za kimataifa, lazima niwe na makazi sehemu tofauti-tofauti, siyo kwa kupenda bali sheria za kazi yangu zinanilazimisha kufanya hivyo,” alisema Grace huku akifutafuta vumbi ndani ya nyumba hiyo kwani kwa kipindi chote ambacho hakuwepo, hakukuwa na mtu aliyekuwa anaishi.

“Pale uwanja wa ndege kuna jambo ulitaka kuniambia. Ni nini?”

“Kuna tatizo nyumbani Tanzania. Una kifua nikwambie?”

“Tatizo gani tena?”

“Kaburi lako limefukuliwa na sampuli zimechukuliwa kutoka kwenye mwili wako kwa ajili ya kwenda kupimwa DNA.”

“Mungu wangu, sasa si ukweli utafahamika?”

“Tayari wameshagundua kwamba aliyezikwa siyo wewe, sasa hivi wanafanya uchunguzi wa nguvu kubaini kilichotokea siku hiyo. Hivi tunavyozungumza, mkeo anahojiwa na maafisa wa polisi.”

“Mh! Anasemaje?”

“Anashangaa tu. Lakini hilo siyo kubwa, nikuulize kitu?”

“Uliza tu.”

“Mkeo ana uhusiano gani na waziri mkuu?”

“Kabla sijagundua kwamba mheshimiwa waziri mkuu anahusika katika njama za kutaka kuyakatisha maisha yangu, familia zetu zilikuwa marafiki, tukawa tunatembeleana, wao wanakuja kwetu na siku nyingine sisi tunaenda nyumbani kwao. Kimsingi tulikuwa tukiishi kama ndugu.”

“Unajua kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na mkeo?”

“Niniii? No! Haiwezekani, nasema haiwezekani. Haiwezi kuwa kweli, hawezi.”

“Hebu angalia hizi picha. Huyu ni nani? Na huyo aliyekumbatiana naye ni nani?” alisema Grace huku akimsogezea Magesa laptop yake, akawa anaitazama picha ile akiwa ni kama haamini. Mkewe alionekana akiwa amekumbatiana na mheshimiwa waziri mkuu, huku wakiwa wamegusanisha midomo yao, kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa.

“Hii ilikuwa ni siku ya ajali yako, wakati maiti yako ilipokuwa hospitalini mkeo alikuwa akila raha Bagamoyo kama unavyoona,” alisema Grace na kusababisha Magesa ashindwe kujizuia, akaanza kuangua kilio kama mtoto mdogo.

“Huna haja ya kulia Magesa, hiyo ndiyo dunia uliyoiacha nyuma yako,” alisema Grace na kumkumbatia Magesa, akawa anambusu huku akiendelea kumbembeleza lakini haikusaidia kitu. Uchungu aliokuwa anauhisi Magesa ndani ya moyo wake ulikuwa hauelezeki.

Kwa kuwa Grace alikuwa anajua namna ya kumtuliza, alimshika mkono na kumuinua pale alipokuwa amekaa, akamfuta machozi na kumuongoza kuelekea chumbani huku Magesa akiendelea kulia. Safari yao iliishia ndani ya chumba kizuri cha kulala, Grace akamsukumia Magesa juu ya kitanda kikubwa cha kisasa, harakaharaka akavua nguo alizokuwa amevaa na kubaki kama alivyotoka kwenye tumbo la mama yake.

Akamfuata Magesa na kumfanya vilevile, muda mfupi baadaye wote walikuwa wanafanana, taratibu wakaanza kupasha misuli yao kwa ajili ya kuingia kwenye mechi ya kirafiki, isiyo na refa wala jezi.

Kadiri Grace alivyokuwa anaongeza ufundi wa kugusa hapa na pale, ndivyo Magesa alivyokuwa anabadilika kihisia, kilio kikakatika juu kwa juu na badala yake ikaanza kusikika miguno ya hapa na pale.

“Ni jukumu langu kukufurahisha Magesa na kukusahaulisha mambo yote ya dunia uliyoiacha nyuma yako,” alisema Grace huku akiongeza kasi ya kuupasha moto mwili wa Magesa, muda mfupi baadaye, tayari wawili hao walikuwa wakielea kwenye bahari ya huba yenye kina kirefu.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

1 Comment

Leave a Comment