The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-6

4

ILIPOISHIA..
Kipindi chote sekretari yule alibaki akimwangalia Elizabeth, alikutana na msichana aliyekuwa supastaa, aliyependwa na wanawake wengi, kila alipomtazama, alijisikia raha moyoni mwake.

SONGA NAYO..

“Karibuni sana,” alisema sekretari huku akitoa tabasamu pana.
“Asante. Tunaweza kumuona meneja?”
“Hakuna tatizo.”

Alichokifanya sekretari ni kuchukua ile simu ya mezani kisha kumpigia meneja wake, wala simu haikuita kwa kipidi kirefu, ikapokelewa na Edson ambapo alimwambia kwamba awaruhusu wageni hao waingie ndani.

Walipoingia tu, kitendo cha Elizabeth kumuona Edson, mapigo ya moyo wake yakaongeza kasi ya kudunda, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kila alipomwangalia Edson ambaye uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, uzuri aliokuwa nao ukazidi kuongezeka huku Elizabeth akahisi kama yupo ndotoni, kukukutana na mwanaume mzuri kama alivyokuwa Edson, ilikuwa moja ya tukio lisiloaminika machoni mwake.

“Karibu,” aliwakaribisha Edson, kitendo cha Elizabeth kuisikia sauti ya Edson tu, akahisi ngoma za masikio yake zikianza kucheza. Alifarijika kupita kawaida.

Alitamani kupata nafasi zaidi ya kuzungumza naye, amwambie ukweli juu ya alivyokuwa akijisikia, hata kama atakataliwa, ajue lakini si kuona mwanaume huyo akipita huku mwanamke mwingine ambaye kwake alionekana kutokuwa na hadhi ya kutembea naye akiwa ameolewa na kuwekwa ndani kabisa.

“Huyu namfahamu, anaitwa Elizabeth! Sijui wewe unaitwa nani?’ aliuliza Edson, muda wote uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.
“Naitwa Candy!”
“Oke! Karibu sana!”
“Asante. “

Wote wakanyamaza, walikuwa kama watu waliosakiziana kuzungumza. Japokuwa Elizabeth alikuwa na hamu kubwa ya kumwambia Edson alivyokuwa akijisikia moyoni mwake lakini kwa wakati huo, kila kitu kikasahaulika moyoni mwake.

“Mnazionaje huduma zetu?” aliuliza Edson baada ya kuona ukimya wa muda mrefu.
“Ni nzuri mno, ninapenda kusafiri na ndege zetu, ninazipenda sana, ni safi, zina uwezo, nawapongeza sana,” alisema Elizabeth, hakuwahi kupanda ndege za shirika hilo la ndege lakini aliamua tu kusifia.

“Asante sana Elizabeth, pia ninapenda ubunifu wako, ni mzuri sana, u mwanamke wa tofauti sana, unajitoa sana kwenye kutafuta chapaa, hakika kila mwanaume anatamani kuwa na mwanamke kama wewe,” alisema Edson na kumalizia kwa tabasamu pana.
Wakati wakizungumza hayo, mawazo ya Elizabeth yalihama kabisa, alichokiona ndani ya moyo wake ni kwamba alikuwa na Edson sehemu fulani, ndani ya chumba huku wakiwa wamelala na kufanya kila kitu usiku huo huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha mno.

“Elizabeth…” aliita Candy baada ya kumuona rafiki yake akiwa kimya, tena kwenye rundo la mawazo.
“Abeee!”

Edson hakuzungumza kitu zaidi ya kucheka tu, kufuatia kumuona msichana huyo alivyoshtuka kutoka katika lindi la mawazo. Hata yeye alimkubali sana Elizabeth, alikuwa msichana mrembo lakini kamwe hakutaka kumsaliti mke wake.
“Nitahitaji unibunie vazi moja zuri la kike, vazi ambalo halijawahi kubuniwa nchini Tanzania, ninataka iwe zawadi kwa mke wangu,” alisema Edson.

“Hakuna tatizo, nitafanya hivyo, nakuahidi utalipenda,” alisema Elizabeth.
Japokuwa naye alirudisha jibu kwa tabasamu pana lakini moyo wake haukuwa na furaha hata kidogo, kile alichokuwa amejiuliza, alipata jibu la uhakika, achana na wale vijana waliokuwa ufukweni, kitendo cha kujua kwamba mwanaume huyo alikuwa ameoa, kilimuumiza sana, akahisi kama kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.

“Naombeni niende uani kwanza,” alisema Candy, Elizabeth akashtuka.
“Ooh! Hakuna tatizo, mwambie dada hapo akuelekeze,” alisema Edson.

Je, nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.

4 Comments
  1. ahady kidehele says

    usomaji umeboreshwaaa twashukuruu global

    1. Global Publishers says

      asante, tunakushukuru pia kwa kulitambua hilo na kuendelea kusoma habari zetu, Mungu akubariki sana.

  2. Majoy says

    Jamani Global muwe mnamalizia hadithi mpk mwisho nyingi sana mnazikatisha cjui kwa nini.

  3. carter joseph donnie says

    muwe mnaweka na ratiba za mechi kuboresha huduma zaidi

Leave A Reply