The House of Favourite Newspapers

Siku zote iwe Valentine yenu

0

Asalaam alaikum wapenzi wasomaji wangu, bila shaka ni wazima mnaendelea vema na ujenzi wa taifa letu, kwa wale wagonjwa niwaombee huko mlipo Mwenyezi Mungu atawajalia.

Wiki hii mdau wangu nimeona tuiongelee Valentine’s Day ambayo wengi wamezoea kuiita Siku ya Wapendanao. Imekuwa kawaida kila inapofikia siku kama hii kila mmoja anaongeza mapenzi kwa mwenzake na ikiisha basi mapenzi yanapungua.

Mazoea/kufuata mkumbo

Tabia kama hii naweza kuiita kama mazoea kwa baadhi ya wapendanao ama kufuata mkumbo. Wapenzi wengi wanapokaribia kufikia mwezi huu huwa hawabanduki pembeni ya watu wao. Kama mpenzi wake ni mfanyakazi atahakikisha anamsumbua mara kwa mara, kuleteana zawadi kila siku na vitu vingine, lakini inapokuja kupita siku hii taratibu mapenzi yao yanaaza kubadilika na kupungua tofauti na walivyokuwa.

Ahadi za uongo

Hapa nataka kuwapa somo kwa wale wapenzi ambao ikifika siku kama hii mengi hujitokeza hususan suala la kutoa ahadi ambazo ngumu kuzitekeleza. Wapo wanaoahidiana kufufua penzi lao na kwamba hakuna kitachowatenganisha labda kifo, pili wapo wanaoahidiana kufunga ndoa siku zijazo lakini mwisho wa siku wanaambulia patupu na kujutia.

Hivi jamani kwa nini umdanganye mtu unayempenda? Kwa nini umpe ahadi za uongo ambazo unajua kabisa huwezi kumtimizia? Niwaombe siku kama hii ya wapendanao si jambo zuri kuitumia kwa kutoa ahadi za uongo. Kama kweli unampenda na umeamua kumtoa siku hii basi mpe ahadi za kweli ambazo zinaweza kudumisha uhusiano wenu ukadumu milele na milele.

Isiwe tu Valentine

Kama kweli unampenda, hakikisha kila siku inakuwa Valentine yenu. Muoneshe upendo wa dhati, siku kama hii ni ya kutulia na kutafakari mustakabali wa mapenzi yenu yalipotokea na yanapoelekea, wapi mlikosea, wapi mlikwaruzana ili kuyaboresha.

Kwa leo niishie hapa na niwatakie wasomaji wangu wote heri ya Sikukuu ya Valentine, usikubali kuwa mchepuko!

Leave A Reply