Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!
Hadi usiku ulipoingia watu walikuwa bado wakiingia na kutoka, zamu yangu ilipofika, nikaingia. Akaniuliza kwa nini kijana wangu hakupotea kama alivyosema?
Sasa endelea…
Mganga aliniangalia vizuri na kuniuliza kama katika mipango yangu nilimshirikisha mke wangu, nikasema hapana, sitaki kabisa ajue lolote kwa sababu nina wasiwasi anaweza kukataa na hivyo kunivurugia kabisa.
Basi akaniambia hiyo ndiyo sababu kubwa ya kushindwa kufanikiwa kwa jaribio langu kwa sababu mke wangu alikuwa amemkinga mtoto wake, hivyo kama bado nina nia hiyo, inabidi afanye kazi ya kutegua kwanza kinga zake ndipo afanye mambo yake.
Nikasema nilikuwa bado nina nia hiyo na nilitaka mipango hiyo ifanyike haraka ili nijue moja, akasema atarekebisha siku hiyo hiyo na nitakapofika nyumbani nitagundua kitu gani kimefanyika.
Basi akaniambia kesho asubuhi niendelee tu na safari yangu ya kurejea nyumbani au niende kazini kwangu na kwamba shughuli hiyo ilikuwa imeisha. Kesho yake niliondoka mapema kurejea Dar es Salaam ambako nililala siku moja tu na siku iliyofuata nikapanda basi kuelekea kazini kwangu Masuguri mkoani Ruvuma.
Nilipofika tu machimbo, simu ya mke wangu iliingia kwenye simu yangu, moyo ukapiga nikajua mambo yamejipa, basi nikapokea nikijifanya kumfahamisha kuwa nilikuwa nimefika salama. Lakini kabla sijasema lolote, akaniambia kijana wetu amepata matatizo na natakiwa nirudi Dar mara moja.
Nikamuuliza kitu gani kimetokea, hakutaka kuniambia zaidi ya kunisisitiza kuwa angependa niwe Dar hata siku hiyo hiyo usiku. Nikajua kitu kimekubali, nikawaaga marafiki zangu kuwa narudi Dar, wakashangaa sana lakini nilipowaeleza nimepata taarifa za ghafla kuhusu mtoto, wakanielewa.
Nikakodi pikipiki kutoka machimbo hadi njia panda ya Kitai, pale nikasubiri gari na nikapata nusu saa baadaye. Nilifika Songea mjini kama saa mbili hivi usiku, nikauliza kama ninaweza kupata gari usiku ule, nikaambiwa lipo moja ambalo linaishia Njombe. Nikapanda na saa sita kasoro robo tukaingia Njombe.
Pale nilipata gari lingine dogo lililoishia Makambako, pale nikapanda malori ambayo yalinifikisha Iringa saa kumi na mbili asubuhi, nikapata basi la kwanza na saa tisa alasiri tuliingia Dar.
Moja kwa moja hadi Tabata ambako sikumkuta mke wangu, nilipouliza kwa majirani wakaniambia aliondoka tangu jana usiku na hajarudi. Nikampigia simu, akaniambia alikuwa Mwananyamala kwa dada yake hivyo nimfuate mara moja.
Nikachukua bodaboda, ikanifikisha hadi Mwananyamala kwa dada yake. Niliwakuta wamekaa sebuleni, baada ya kuwasalimia nami nikajiunga nao na mara moja nikauliza alipo mtoto wetu.
“Kwani wewe unamhitaji mtoto au maiti yake?” mke wangu aliniuliza swali lililonishtua sana, sikutegemea kama angeweza kuhisi kitu. Mshtuko wangu hata wao waliuona, lakini cha ajabu dada mtu hakushtuka kusikia kauli ile kutoka kwa mdogo wake. Nikajikakamua na kumuuliza alikuwa na maana gani kuniambia vile.
Bila kupepesa macho, akaniambia kuwa anafahamu ninao mpango wa kumuua mtoto wake kwa sababu ya kusaka utajiri, kwa hiyo akanionya kuwa yeye hatakubali kumuona kiumbe aliyemuweka tumboni kwake miezi tisa anatoweka kirahisi kwa tamaa ya mali.
Akaniambia kuanzia siku ile niachane na mpango wa kumtoa kafara mtoto wake, kama ninataka utajiri, basi nimtafute mtu mwingine kwa sababu yeye alikuwa ameaga kwao na endapo nitarudia tena, atawaeleza nyumbani kwao na ole wangu kwa kitakachonitokea.
Kama niliyezinduka, nikajikaza na kujifanya kukasirika, nikamuuliza alikuwa na ujasiri gani kuniambia mambo ya ajabu kama yale mbele ya shemeji yangu, lakini tofauti na nilivyotegemea, wote wawili waliangua kicheko cha nguvu ambacho kilikuwa ni kama wananikebehi!
Je, nini kilitokea? Usikose katika toleo lijalo.
JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS


