Serikali kukabiliana na wezi wa umeme
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud (kushoto), akizungumza jambo kwa wanahabari (hawapo pichani). Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa.
…Badra akisikiliza maswali yaliyokuwa yameulizwa na wanahabari.
Wanahabari wakichukua matukio katika hafla hiyo.
SERIKALI imeliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha linawabaini wezi wa umeme kupitia kikosi chake cha ukaguzi wa watumiaji wa umeme ili wateja wasio waaminifu wanachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza na wanahabari leo katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, amesema wizara yake inatarajia kuunda kikosi maalum kitakachojumuisha wataalam kutoka TANESCO na vyombo vya usalama kwa lengo la kukabiliana na tatizo hilo linaloikosesha mapato serikali kupitia TANESCO.
Amesema mbali na kulitaka shirika hilo kukabiliana na wezi wa umeme, pia amezitaka taasisi mbalimbali za serikali hata zisizo za serikali kuzingatia matumizi bora ya umeme ili kudhibiti upotevu wa nishati hiyo muhimu.
Masoud amefafanua kuwa hatua hiyo imekuja baada ya taasisi kuona kwamba, taasisi mbalimbali huwa zinaacha umeme ukiendelea kupotea bure baada ya muda wa kazi kuisha huku akivitaja baadhi ya vifaa vinavyoachwa vikiendelea kufanya kazi kuwa ni viyoyozi, taa, kompyuta na baadhi ya vifaa vingine vinavyotumia umeme.
Akizungumzia hali ya umeme hapa nchini, Masoud amesema hakuna mgawo wowote unaoendelea hivi sasa kwani hali ya uzalishaji ni nzuri pamoja na mabwawa ya maji ambayo hutumika kuzalisha umeme pia akitaja kiasi cha umeme kinachopatikana kwa sasa kuwa megawati 1500 matumizi ikiwa ni kati ya megawati 800 na 900 kwa siku.
NA DENIS MTIMA/GPL

