The House of Social Media
gunners X

Umezalishwa, huna msaada? Hujui hatima yako? Jifunze!

0

baby1JUMAMOSI nyingine tulivu tunakutana katika uwanja wetu wa kufundishana masuala ya uhusiano na maisha ya wapendanao kwa ujumla.

Niwashukuru wale wote walionitumia ujumbe mfupi kuonesha wameguswa na mada ya wiki iliyopita ambayo ilihusu umuhimu wa kutengeneza historia katika uhusiano. Wengi wenu mlisema mlikuwa mkitaka njia za mkato kufikia kilele cha mafanikio. Mliishia kukata tamaa kila mlipoanzisha uhusiano.

Mlikiri kwamba mmejifunza, kuvumiliana ndiyo silaha ya maisha marefu. Mlijifunza kwamba mtu hupaswi kukata tamaa harakaharaka. Kwamba, unapaswa kushikilia ulipo mpaka dakika za mwisho. Kwamba ifike wakati mnasema; ‘ni Mungu tu katufikisha hapa, si kwa akili zetu.’

Mmepambana, mmetengeneza historia ya penzi lenu kutokana na majaribu mliyopitia. Mnapongezana kuonesha kwamba msingejitahidi, mngeahirisha safari mapema. Nilisema hilo ndilo penzi la kweli ambalo ni vyema kila mmoja wetu akajifunza.

Tukirudi katika mada ya leo kama inavyosomeka hapo juu.  Wengi tunaamini watoto ni baraka. Wanaletwa na Mungu. Wakifika duniani, Mungu anakufungulia milango ya kuwatunza hata kama huna uwezo wa kuwalea.

Utapambana kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu. Hakuna mama atakayekubali mwanaye akose mahitaji. Atapambana ili mwanaye ale, anywe, avae na akue vizuri.

Tatizo huwa linakuja, wengi wamekuwa wakijikuta tu wanapata watoto. Pasipo kuwa na maandalizi mazuri, mtoto anakosa mahitaji na mama na mtoto wanajikuta wakiteseka. Mama anakosa msaada, kuzaa kunageuka kuwa majuto.

Mama anajuta kuzaa. Anajuta kufanya kitendo ambacho kilimsababishia apate ujauzito. Tujifunze kupitia mfano huu:

“Anko habari mimi ni msichana ambaye nimebahatika kupata watoto wawili. Cha ajabu mwenzangu hanipi matumizi. Mimi mwenyewe sina kazi ya kufanya ni mama wa nyumbani. Kinachoniuma zaidi, mwenzangu anasema hanitaki, imefika wakati hadi watoto wake anawakana.

“Anasema nimembambikia. Hana imani na mimi, wakati ukweli hata Mungu anajua. Sijawahi kusaliti tangu nimeanzisha naye uhusiano. Sasa hivi anasema amepata mwanamke mwingine. Mimi hanitaki tena, eti ana mpango wa kufunga ndoa na huyo mwanamke. Nisimsumbue. Inaniuma maana sina msaada wa ndugu.

“Ndugu zake wako mbali, baadhi nimezungumza nao kwa simu nao wanasema hawana kitu. Mbaya zaidi wengine wamethubutu kusema hawanitambui maana tayari wametambulishwa mwanamke mwingine ambaye anataka kufunga ndoa na ndugu yao, mwenzenu nipo katika wakati mgumu kweli.”

Mfano huo utoshe kutufundisha juu ya umuhimu wa kujiandaa kuzaa. Kwanza unapaswa kumtathmini huyo unayepanga kuzaa naye. Ana mapenzi ya dhati? Ana nia ya kufika mbali na wewe? Hana tamaa tu za kupata mtoto ilimradi na yeye aitwe baba?

Historia yake ikoje? Hajawahi kuzalisha watoto halafu akakataa mwanamke? Ana hofu ya Mungu. Ukishamchunguza kwa makini mtu huyo, zungumzieni suala la kuzaa kwa kujua mahitaji yake. Hivyo kila kitu mtakachokifanya au matokeo mtakayoyapata muwe tayari na majibu yake.

Kama unaona mtu uliyenaye hana sifa nilizoziainisha hapo juu, ni vyema ukaanza kumuepuka kabla hamjafika mbali. Usikubali kuanzisha uhusiano na mtu ambaye huna imani naye. Mchunguze vya kutosha na kuona kweli ana msimamo wa kufika mbali.

Ukijiridhisha, jadilini kuhusu ndoa. Jadilini kuhusu mtoto. Vitu vyote hivyo vinahitaji maandalizi ya fedha za kujikimu. Ndoa inahitaji mahala pakuishi, mtoto anahitaji matumizi. Mna kipato cha kutosha? Kama bado anzeni kwanza kurekebisha kipato chenu.

Tengenezeni mazingira ambayo mtoto akija aweze kupata mahitaji muhimu. Mtoto ambaye mtaweza kumgharamia, aishi vizuri. Asome vizuri. Hilo litawezekana kama utakuwa umefanya chaguo sahihi, ukampata mtu sahihi ambaye mtafunga ndoa na kufurahia maisha ya ndoa pamoja na familia.

Leave A Reply