ILIPOISHIA IJUMAA:
Kama angejua kuwa sikuwa na gari hilo, angenisumbua kwa maswali na sikuwa na jibu la kumpa.
Kama atajua ni hapo kutakapokucha, nitajua jinsi ya kumueleza, nilijiambia.
Hata hivyo, nilikuwa na uhakika kwamba gari lile lingelala pale hadi asubuhi ambapo ningemtuma dereva wangu alifuate.
“Ndiyo unarudi kutoka ofisini kwako?” Mke wangu akaniuliza tulipokuwa sebuleni. Alikuwa akinitazama kwa shaka. SASA ENDELEA…
“Ndiyo narudi hivi,” nikamjibu.
“Mbona umechelewa sana? Ni saa ngapi sasa?”
“Inakaribia kuwa saa tisa.”
“Kazi gani mpaka saa tisa usiku?”
“Kuna kazi niliyokuwa ninaikamilisha.”
“Kazi gani?”
“Huwezi kujua. Ni taarifa ambayo inatakiwa kufikishwa kwa waziri mkuu kesho. Nilitaka niimalize leo. Kesho asubuhi iwe tayari.”
Nilipomjibu hivyo mke wangu akaniuliza.
“Utahitaji chakula au kinywaji?”
“Kama kuna kahawa ya maziwa nipatie.”
“Nafikiri ipo, ngoja nikuandalie.”
Mke wangu akaenda jikoni.
Baada ya dakika tatu hivi alirudi akaniletea kahawa ya maziwa kwenye kikombe.
“Karibu,” akaniambia huku akiketi kando yangu.
Nilipopokea kile kikombe nililipapasa tumbo lake.
“Nini?” akaniuliza huku akitabasamu.
“Naona mtoto wetu anazidi kukua,” nikamwambia huku nikimtazama kwa pembeni.
“Unawaza mtoto tu?”
Niliionja ile kahawa kisha nikamjibu.
“Si unajua mtoto wa kwanza…”
“Ana nini?”
“Anatia kiwewe. Kila siku naomba Mungu mtoto wetu azaliwe.”
Mke wangu akauweka mkono wake kwenye bega langu.
“Nataka nizae kwa mfululizo watoto wawili kisha ndiyo nipumzike,” akaniambia kwa sauti laini.
“Kumbe wewe una mawazo kama mimi. Mimi nataka iwe hivyohivyo.”
“Unajua ni vizuri uzae watoto wawili halafu unapumzika. Baadaye ukifikiria kupata mtoto mwingine inakuwa poa.”
“Ni kweli mke wangu. Tukishapata watoto wawili tunapumzika. Tutakapotaka tena mtoto, tunamtengeza mwingine au siyo?”
“Tunamtengeza mwingine kwa mashine au…?”
“Kwa mchakato maalum.”
“Upi?”
“Unaujua vizuri. Unauliza tu sijui kwa faida ya nani.”
“Umeanza upuuzi wako! Haya maliza kahawa twende tukalale.”
“Sawa mke wangu.”
***
Dakika chache kabla ya saa kumi na mbili alfajiri niliamshwa kwa mlio wa simu ya mezani iliyokuwa kwenye kimeza cha mchagoni mwa kitanda.
Niliinua mkono wangu nikakinyakua chombo cha kupokelea na kukiweka sikioni.
“Hello…Meshack hapa.”
“Hiki ni kituo kikuu cha polisi. Mheshimiwa unahitajika hapa kituoni. Kuna gari ambalo limekamatwa na polisi alfajiri hii ambalo limekutwa na kadi yenye jina lako.”
Wito huo ulinishtua. Nilishukuru kuwa mke wangu alikuwa bado amelala na hakusikia kwamba lile gari nilililoondoka nalo usiku limekamatwa na polisi. Nikajiambia kukamatwa kwa hilo gari kutafichua mengi ambayo nisingependa yajulikane.
Msemaji wa polisi alipoona nimenyamaza kimya akaongeza.
“Hilo gari lilifukuzwa usiku na polisi waliokuwa kwenye doria. Alfajiri hii lilikutwa limegeshwa sehemu likiwa halina mtu. Mlinzi mmoja wa eneo hilo aliwaambia polisi kuwa gari hilo lilifikishwa usiku mahali hapo na waliona mtu mmoja akishuka na kuvaa nguo kisha aliondoka na kuliacha hapohapo.”
Wakati polisi huyo akinielezea hivyo moyo wangu ulikuwa ukienda mbio. Hapohapo nikapata akili. Nikazua uongo huu.
“Kama mmelipata hilo gari ninashukuru sana. Gari langu liliibwa usiku na kunisababishia usumbufu mkubwa.”
“Liliibwa usiku?”
“Ndiyo. Kama saa tano usiku nilikuwa katika hoteli moja pamoja na mke wangu. Tulipotoka gari likawa halipo.”
“Uliripoti kituo gani?”
“Sikuwahi kuripoti kituo chochote.
Nilikuwa nije kuripoti asubuhi hii.”
“Sasa fika hapa kituoni, kuna maswali tunataka kukuhoji!”
“Kuhusu hilo gari au…?”
“Ndiyo kuhusu hili gari na kuhusu wewe mwenyewe. Ikiwezekana fika na mke wako.”