The House of Social Media
gunners X

Penzi Kabla Ya Kifo

ILIPOISHIA

Hakutaka kuchelewa, hata hakutaka kumpa taarifa Candy, kwa kuwa alikuwa amekwishaoga asubuhi hiyo, alichokifanya ni kuanza kuelekea huko Ubungo kwa ajili ya kuonana na Edson tu.

SONGA NAYO..

Hakuchukua muda mrefu akafika katika jengo hilo, akapanda lifti na kwenda mpaka kwenye ofisi ya Edson, alipofika, moja kwa moja akaruhusiwa na kuingia ndani. Alipoyakutanisha macho yake na Edson tu, hapohapo mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, kwa siku hiyo, alijipanga vilivyo, hakutaka kushindwa hata mara moja, alihitaji kumwambia ukweli mwanaume huyo.

“Umependeza sana,” alisema Edson huku akimpa mkono.

“Asante sana.”

Walizungumza mawili matatu na kisha Elizabeth kuchukua kitabu kile kilichokuwa na picha kadhaa za mavazi na kumsogelea Edson kule alipokuwa, kuizunguka meza na kusimama karibu yake kisha kukiweka kitabu kile mezani, kwa jinsi mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakidunda, hata Edson aliyasikia kwa mbali.

“Elizabeth! Upo sawa?”

“Kwa nini?”

“Hapana! Nimeuliza tu!”

“Nipo sawa!”

“Basi hakuna tatizo! Haya nioneshe sasa,” alisema Edson, wakati huo, mawazo ya Elizabeth hayakuwa hapo kabisa, alikuwa akijifikiria namna ya kumuingia mwanaume huyo. Walikuwa wawili tu ofisini, tena karibukaribu mno. Hiyo akaiona kuwa nafasi yake kumaliza mchezo.

“Edson…..”

“Naam.”

“Unanukia vizuri kweli!”

“Asante!”

“Unatumia pafyumu gani?”

“The Prince…”

“Waooo! Ya kiume?”

“Ndiyo! Nililetewa na mke wangu kutoka Uholanzi! Naipenda sana, hata ikiisha, huwa ananiagizia,” alisema Edson.

Elizabeth akabaki kimya kwa muda, mapigo ya moyo wake yalikuwa yakidunda kwa nguvu mno, Edson alibaki akikiangalia kitabu kile lakini uwepo wa msichana yule pembeni yake, tena kwa ukaribu kabisa kulimnyima amani.

Alitamani kumwambia atoke lakini aliuona mdomo wake kuwa mzito kufanya hivyo, alichokifanya ni kubaki kimya tu huku macho yake yakikiangalia kitabu kile.

Kulikuwa na picha za mavazi mengi yaliyomvutia, aliyoamini kwamba kwa namna moja ama nyingine mkewe angeyapenda sana, alichokifanya ni kuchagua moja kisha kumwambia Elizabeth kwamba lingekuwa jambo zuri sana kama angeshona vazi hilo.

“Umelipenda?”

“Yeah!”

“Nashukuru! Nitakufanyia kazi hiyo! Ila kuna lingine.”

“Lipi?”

“Naweza kuonana nawe baadaye?”

“Baadaye?”

“Ndiyo!”

“Kuna nini?”

“Haujanijibu swali langu!”

“Inategemea na muda!”

“Jioni, hata saa kumi na mbili.”

“Mmmh!”

“Nini?”

“Nitaangalia, ila sidhani, nitahitaji kurudi nyumbani kukaa na familia yangu!” alisema Edson huku akionekana kumaanisha alichokisema.

Moyo wa Elizabeth ulikuwa na wasiwasi mno, alitamani sana kumwambia mwanaume huyo juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kwamba alimpenda sana lakini hakujua ni wapi alitakiwa kuanzia.

Alibaki kimya huku akionekana kama kuna jambo kubwa alikuwa akilifikiria mahali hapo. Edson alibaki kimya akimwangalia msichana huyo. Ni kweli alikuwa mrembo, alivutia kwa kila mwanaume ambaye angebahatika kumuona lakini kwake yeye, alimuona kuwa msichana wa kawaida, mawazo yake yote yalikuwa kwa mkewe tu.

Elizabeth alipoona ameshindwa kabisa, akaamua kuondoka ofisini hapo na kurudi nyumbani kwake. Huko, aliendelea kujuta, alipata nafasi hiyo kwa mara ya pili lakini bado hakumwambia mwanaume huyo ukweli wa moyo wake.

Alichokifanya ilipofika jioni ni kumpigia simu na kumwambia kwamba walitakiwa kuonana, kitu kilichomuuma sana ni pale alipomwambia kwamba alitakiwa kurudi nyumbani haraka kwani alihitaji kukaa na famiia yake, baada ya hapo, simu ikakatwa.

Je, nini kiliendelea kati ya Elizabeth na Edson? Usikose simulizi hii wiki ijayo.

“Edson….Edson…nakupenda Edson…nahitaji uwe wangu Edson…” alisema Elizabeth huku machozi ya uchungu yaliyojaa mapenzi yakianza kumbubujika mashavuni mwake.

 Je, nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.

Comments are closed.