KAMA kawaida kwenye kolamu hii tunawaletea mastaa mbalimbali na kuwabananisha kwa maswali kumi. Leo tunaye staa wa filamu Bongo Chuchu Hans ambaye anabanwa na Mwandishi Wetu Mayasa Mariwata, ikawa hivi;
Ijumaa: Ningependa kujua ukiwa nyumbani na mpenzi wako unapenda kumpikia vyakula gani?
Chuchu: Napenda sana mapishi kuliko chochote, nikiwa nyumbani napendelea kupika wali wa nazi na samaki. Ni chakula kinachonivutia zaidi mimi na mwandani wangu.
Ijumaa: Wasanii wengi wanapenda kujichubua wakiamini wanaongeza urembo, wewe ni miongoni mwao?
Chuchu: Mimi na mkorogo ni vitu viwili tofauti, nauchukia! Hao wanaojichubua hawajiamini, siri kubwa ya urembo wangu ni kula kwa mpangilio na kupata muda mzuri wa kupumzika.
Ijumaa: Kutokana na muonekano wako, ni mavazi gani ambayo unaamini ukivaa yatakufanya uwe amazing?
Chuchu: Nguo yoyote ile ambayo nikivaa nihakikishe imenipendeza, ila navutiwa zaidi na nguo ndefu.
Ijumaa: Kumekuwa na maneno yasiyochuja kuwa wasanii wengi wanatumia dawa za Kichina kuongeza shepu, likoje hilo na wewe hujawahi kufikiria kitu hicho?
Chuchu: Ninachojua wengi wanavaa zile taiti za Kichina ambazo mtu anaonekana kajazia. Mimi wala sifikirii hayo, najikubali nilivyo.
Ijumaa: Tunajua uko na Ray, kuna madai huwa unachepuka, hilo likoje?
Chuchu: (Kicheko) hapana bwana, najiheshimu sana kuliko watu wanavyofikiria.
Ijumaa: Ni changamoto gani uliyowahi kukutana nayo ukajikuta unajuta kuwa staa?
Chuchu: Changamoto zipo nyingi, ila kubwa kuliko ni kukosa uhuru katika maisha maana kuna mambo unalazimika kufanya hata kama hayaendani na uwezo wako.
Ijumaa: Unapenda kuwa na watoto wangapi katika maisha yako?
Chuchu: Siwezi kukadiria idadi ya watoto kwa kuwa kila jambo anapanga Mungu.
Ijumaa: Endapo ukiolewa na Ray, utapenda mapumziko yenu ‘honeymoon’ yawe nchi gani?
Chuchu: Hilo la kuolewa haliko akilini mwangu kwa sasa.
Ijumaa: Ni maungo gani ya mwili wako ukiguswa unadata zaidi ukiwa kwenye dimbwi la mahaba?
Chuchu: Hayo ni mambo ya siri siwezi kuyaanika ila zipo hizo sehemu ‘amazing’ sana.
Ijumaa: Kuna kipindi nilisikia umekorofishana na Ray tatizo lilikuwa nini?
Chuchu: Yalikuwa maneno ya watu tu, mkipishana kidogo ooo wamekorofishana, hakukuwa na ishu kubwa.
Ijumaa: Unazungumziaje haya mabifu ya mastaa kisa kuibiana wanaume?
Chuchu: Ni mambo ya kijinga tu na wanaofanya hivyo ni malimbukeni wa maisha.