Mkurugenzi wa Miradi ya Uchumi na Utafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. Beatus Alois (kushoto wa kwanza) akiwasilisha rasimu yake kupitia projekta iliyokuwa ikimulika ukutani.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja (wakwanza kulia) akiwa na maofisa wengine kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Mtaalamu wa masuala ya Kilimo (aliyesimama) akitoa mapendekezo yake namna ya kuboresha rasimu hiyo iliyohusu masuala ya kilimo cha kisasa.
Maofisa wa magereza wakifuatilia kwa makini mkutano huo.
Maofisa wa Jeshi la Magereza wakiongozwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Casmir Minja, leo wamekutana kujadili rasimu ya mpango wa kuongeza chakula wanachotumia wafungwa na mahabusu magerezani.
Makamishna hao wamekutana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Magereza jijini Dar es Salaam, chini ya uenyekiti Kamishna Jenerali Minja ambaye ndiye alikuwa mwongozaji wa mkutano huo.
Wakati akifungua mkutano huo wa kujadili rasimu ya Bajeti iliyokuwa imewasilishwa na Mkurugenzi wa Miradi ya Uchumi na Utafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. Beatus Alois Kundi, Minja amesema kuwa jukumu la kuwahudumia chakula wafungwa na mahabusu magerezani ni la serikali na kwa muda mrefu jeshi la magereza limekuwa likikabiliwa na changamoto ya upungufu wa chakula cha wafungwa kutokana na ufinyu wa bajeti.
Kamishna Jenerali, Minja amesema kuwa gharama ya kumhudumia mfungwa mmoja kwa siku ni Tshs. 3,670.
Alisema mahitaji ya fedha kwa kugharamia wafungwa ni shilingi 51 bilioni kwa mwaka lakini kiasi kinachotolewa ni Tshs. 20.9 bilioni kwa wafungwa waliopo magerezani kwa kiwango cha shilingi 1,500 kwa siku.
Alifafanua kuwa mahitaji kwa sasa ya chakula cha wafungwa yanayohitajika ni mahindi tani 8,450.5, mpunga tani 1,976, maharage tani 1,308.7, nyama tani 592,800 na mafuta ya kupikia lita 416.1
Aliendelea kusema kiasi kwa sasa kinachozalishwa kupitia jeshi la magereza kwa chakula ni mahindi tani 2,501.1 ikiwa ni sawa na asilimia 24.3, mpunga tani 317.1 sawa na asilimia 16.1, maharage tani 14.7 ambayo ni sawa na asilimia 1.1, nyama kilo 165,750 sawa na asilimia 27 pamoja na mafuta ya kupikia lita 416.1 sawa na asilimia 100.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa kutambua hilo jeshi la magereza limeandaa mkakati wa kujitosheleza wa chakula na hivyo kuipunguzia serikali gharama ambapo sasa walijadilia andiko la bajeti walilojadili kwa pamoja na wataalamu wa uchumi na huku mapendekezo na maboresho yakitolewa ili kupata maoni ya maboresho ya rasimu itakayopelekwa kujadiliwa Bungeni kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017 wa bajeti ya serikali.
NA DENIS MTIMA/GPL