×

Mkuki moyoni mwangu 06

WATOTO wawili (Kevin na Catarina) wapo katika mapenzi mazito lakini hakuna hata mmoja aliyefungua mdomo kumweleza mwenzake hisia zake, Kevin pamoja na kuwa mwanaume ana aibu nyingi, Catarina naye kwa upande wake anaamini mvulana ndiye anatakiwa awe wa kwanza kusema.

Kila siku wanazungumza wakiamini wao ni marafiki, lakini wote wanasubiri nani aanze! Mwisho wazazi wa Catarina wakaamua kumhamishia Kampala kimasomo walipogundua mtoto wao ameanza kuathiriwa na mapenzi katika umri mdogo.

Akiwa huko, Catarina anamkumbuka sana Kevin kiasi cha kuteseka, shule imefungwa na sasa amerejea Dar es Salaam, cha kwanza anachokitaka ni kumwona Kevin. Siku iliyofuata baada ya wazazi wake kuondoka kwenda kazini, aliamua kwenda Shule ya Sekondari ya St. Joseph kwa lengo la kumwona Kevin, akazuiliwa.

Badala ya kurejea nyumbani, aliamua kusubiri muda wa wanafunzi kutoka, akamwona Kevin ndani ya basi la shule na kumwita, hapo ndipo likatokea jambo ambalo hata yeye hakulitarajia; Kevin aliruka kupitia dirishani na kupiga kichwa kwenye barabara ya lami, damu zikaanza kumtoka puani, masikioni na mdomoni!

Catarina akakimbia mpaka eneo hilo na kumkumbatia, baadaye akaondolewa na Kevin akapakiwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Catarina akikodisha teksi.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

Kama ungekuwa ni usafiri wa kutumia gari la wagonjwa ingewachukua muda wa dakika tano tu kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakipitia maeneo ya Upanga, kwa sababu walikuwa na gari la kawaida na foleni za magari za Jiji la Dar es Salaam mchana huo zilivyokuwa kubwa, iliwachukua saa nzima, Kevin akivuja damu mfululizo ndani ya gari hilo, ndipo wakafika mbele ya jengo la Idara ya Magonjwa ya Dharura ama Emergency kwa Lugha ya Kiingereza.

Wazazi wote wawili wa Kevin walishafika kwa kutumia usafiri wa pikipiki, mama yake alikuwa akilia, akaanguka chini na kuzimia aliposhuhudia Kevin akishushwa garini na kulazwa juu ya machela, mwili wote ukiwa umetapakaa damu, akiwa hana fahamu, macho yake yamegeukia juu kama mtu aliyepoteza uhai.

Watu waliokuwa jirani wakisaidiana na wauguzi walimbeba mama Kevin na kumwingiza ndani ya jengo la wagonjwa mahututi ambako alianza kuhudumiwa akipewa huduma ya kwanza, Kevin akaingizwa chumba cha wagonjwa mahututi, kundi la madaktari bingwa likamzunguka.

“Oxygen! Oxygen!” Daktari mmoja alipiga kelele ili Kevin awekewe hewa safi ya Oksijeni haraka.

Daktari mwingine alikuwa akimpa moyo na alipomaliza alianza kumgandamiza kifuani upande wa moyo kufanya kile ambacho kwa Kiingereza huitwa Cardiac Massage ili kuushtua moyo wake ambao alidai ulikuwa ukielekea kusimama, baba yake Kevin aliyekuwa hapo alishindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka ingawa siku zote Kevin akiwa mtoto yeye ndiye alizoea kumwambia: “Wanaume huwa hawalii.”
“Monitor Vital Signs Urgently!”(Mpimeni vipimo muhimu vya mwili haraka!) daktari mwingine akatamka.

Wauguzi wakaanza kushughulika na kupima shinikizo la damu, mapigo ya moyo, kuhema na walipomaliza walikabidhi majibu ambayo yalionyesha shinikizo la damu lilikuwa 90/40, lilikuwa likishuka kwenda chini, huku mapigo ya moyo yakiwa 120 kwa dakika, ishara kwamba moyo ulikuwa ukifanya kazi kwa nguvu kubwa kupeleka hewa sehemu mbalimbali za mwili.

“Infuse with sodium chloride 500mls, 50drops per minute, do you understand?”(Muwekeeni dripu ya maji ya chumvi, mililita mia tano, matone hamsini kwa dakika, mnanielewa?) daktari alipiga kelele kama vile mtu aliyekuwa akiongea naye alikuwa mbali sana.

“Yes doctor!”(Ndiyo daktari!) wauguzi wakaitikia huku wakikimbia kufuata maji ya Sodium Chloride pamoja na mipira ya kuwekea, ndani ya dakika mbili tu tayari yalikuwa yakitirika kuingia kwenye mishipa ya Kevin.

“He seems to have Haemorrhagic anaemia, urgently we need to do blood grouping and cross matching, few blood pints of blood needed, call the Laboratory people right know!”(Anaonekana kuwa na upungufu wa damu unaotokana na damu nyingi kuvuja, kwa haraka tunahitaji kupima tujue kundi lake la damu na pia anaweza kuongezewa damu ya aina gani, chupa kadhaa za damu zinahitajika, wapigieni watu wa maabara haraka iwezekanavyo!)

“Yes doctor!” (Ndiyo daktari!) wauguzi wakaitikia na simu ikapigwa maabara, dakika chache tu walifika na kuchukua damu, majibu yalipotoka Kevin alikuwa na kundi O hasi la damu na kiasi chake cha damu mwilini kilikuwa kimebaki gramu tano, sawasawa na asilimia thelathini na tano, alihitaji damu haraka sana.

Dk. James Mabula aliyekuwa zamu siku hiyo idara ya wagonjwa wa dharura baada ya kupewa majibu hayo, aliwasiliana na watu wa benki ya damu ili baba yake Kevin atoe damu, lakini benki ya damu itoe damu haraka na Kevin awekewe wakati akiandaliwa kupelekwa chumba cha upasuaji.

“Adminster injection hydrocortisone 200mg stat to give him strength!” (Mchomeni sindano ya Hydrocortisone 200mg ili kumpa nguvu mwilini!)

Yote hayo yalifanyika madaktari wakimpima Kevin ambaye bado alikuwa hajitambui huku kichwa kikiendelea kuvimba, uamuzi uliofikiwa na madaktari ukawa ni kumfanyia kipimo cha Magnetic Resonance Imaging (MRI) ambacho hupiga picha kuonyesha sehemu gani ya ubongo ilikuwa imeharibika.

“MRI inafanya kazi kweli? Maana hapa Muhimbili napo…”
“Hebu cheki na jamaa mara moja!” Dk. Mabula alimweleza daktari mwenzake, simu ikapigwa, jibu lililopatikana ni kwamba mashine ya MRI ilikuwa imeharibika kwa mwezi mzima.

Hapakuwa na la kufanya zaidi ya kuchukua uamuzi wa kumbeba Kevin ndani ya gari la wagonjwa kumkimbiza hadi Aga-Khan, mita kama elfu mbili hivi kutoka Muhimbili ambako kipimo hicho kilifanyika na kurejeshwa tena Muhimbili, majibu yalikuwa yameonyesha upande wa kulia wa Ubongo ulikuwa umevuja damu nyingi kwa ndani ambayo ilihitajika kuondolewa kwa upasuaji.

Wakati wanarejea, mama yake Kevin alishazinduka na alikuwa mapokezi akiwa amekumbatiana na mume wake, wote wawili wakibubujikwa na machozi, mioyoni na akilini mwao walijua kabisa tayari mtoto pekee waliyekuwa naye hapa duniani alikuwa katika dakika zake za mwisho za maisha, walimu walishawaeleza kila kitu kilichotokea na jinsi msichana mdogo alivyosababisha Kevin kuruka kutoka garini.
“Vipi daktari?” baba yake Kevin alimuuliza Dk. Mabula.

“Mhh! Kijana aliangukia kichwa, mishipa kadhaa ya damu chini ya fuvu lake ikapasuka na imevuja damu nyingi sana ambayo imeugandamiza ubongo wake, lakini pia tumboni kwake kuna damu nyingi imevuja, bandama imepasuka.”

“Mtafanya nini daktari kumuokoa mwanangu? Ndiye mtoto pekee niliye naye.”
“Uamuzi tuliofikia ni kufanya upasuaji wa kichwa na kuiondoa hiyo damu.”
“Atapona?” Mama yake Kevin aliuliza.

“Mama naomba nisiongee kwa uhakika kwamba atapona, wote tumwombe Mungu, ninachoomba ni kwamba mmoja wenu asaini fomu ya kukubali mtoto afanyiwe upasuaji, tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu, mmenielewa?”
“Ndiyo.”

Fomu ikasainiwa, Kevin akaandaliwa kwa ajili ya upasuaji na kusukumwa akiwa juu ya machela kwenda chumba cha upasuaji ambako jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wakiongozwa na Dk. Walter Kweka pamoja na Dk. James Mabula wangefanya upasuaji huo mkubwa kujaribu kunusuru maisha ya Kevin.

Machela ikisukumwa kutoka wodini kwenda chumba cha upasuaji Kevin akiwa juu yake, wazazi wake wakiwa nyuma ya wauguzi, Catarina alikuwa amejificha kwenye moja ya kona ya majengo ya Hospitali ya Muhimbili akishuhudia kila kitu, huku mashavu yake yakiwa yamelowa kwa machozi, akashindwa kuvumilia na kutoka mafichoni akiwakimbilia wazazi wa Kevin.

“Shikamoo baba!” aliamkia baada ya kumgusa bwana Mdoe.
“Usiniguse! Nasema usiniguse! Umetusababishia matatizo makubwa sana na mwanangu akifa…”

“Baba Kevin, usiseme hivyo…” Mkewe alimzuia.
“Naomba mnisamehe, haikuwa makusudi yangu, ilitokea kwa sababu nilikuwa nimemkumbuka sana Kevin, sikujua angeruka, nimeshamwomba Mungu atamsaidia ili apone, nampenda mno mtoto wenu, kutoka moyoni mwangu kabisa, sipo tayari kuona anaondoka na kuniacha.”

“FUNGA MDOMO WAKO NA NINAKUOMBA UONDOKE MBELE YA MACHO YANGU SASA HIVI KABLA SIJAKUPIGA HALAFU NIKAGOMBANA NA WAZAZI WAKO, SIJUI KWA NINI MLIHAMIA PALE, MSINGEKUJA MWANANGU ASINGEKUJUA NA HAKIKA ASINGEKUWA NA MATATIZO ALIYONAYO, NASEMA ONDOKA…” alimaliza mzee huyo akivutwa na mke wake.

Catarina akaanza kuondoka taratibu, uso wake ukiwa umejawa na soni, moyoni alikuwa akiendelea kumwomba Mungu amsaidie Kevin ili asife chumba cha upasuaji.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

Leave a Comment