ILIPOISHIA
Baada ya kufukuzwa kwa muda mrefu na wanajeshi wa mpakani mwa Somalia na Kenya, Mtima na Abdulrahman wanajitosa kwenye mto Afmadow kujaribu kuokoa maisha yao, upande wa pili kutokana na mauaji ya Kundi la WAB, nchini Kenya mamia ya watu wanafanya maandamano wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe uliomtaka waziri wao wa usalama na ulinzi, Jenerali James Nkoyo kuhakikisha analiangamiza kundi hilo.SONGO NAYO…
MAANDAMANO hayo ndiyo yaliyosababisha ulinzi nchini humo kuimarishwa zaidi pia nchi zilizoizunguka Kenya na Somalia zilitoa tahadhari kwa wananchi wake kuzitembelea kutokana na sababu za kiusalama.
Maeneo ya mipakani, mashuleni, kwenye vituo vikubwa vya kibiashara, sehemu za ibada na kila kona kulipo na mikusanyiko ya watu vikundi vya askari jeshi vilikuwepo kuhakikisha watu wanaendelea na shughuli zao za kila siku.
Kazi ikawa moja tu, kulisaka kundi hilo kila walikosikia au kunusa kuwa lingefanya shambulio ili walitie nguvuni na kulifikisha kwenye mikono ya sheria.
* * *
Mtima na Abdulrahman walikuwa wameingia kwenye kumi na nane za wanajeshi wa Kenya waliokuwa wanawatafuta kwa udi na uvumba, ambapo baada ya mafukuzano ya muda mrefu na vijana hao kujitosa katika maporomoko ya Mto Afmadow, wanajeshi walishuka kwenye magari yao na kulizunguka eneo lote la mto huo wakiwa na mitutu ya bunduki mikononi!
Gari la vijana hao lilikwenda kwa kasi ya ajabu hadi chini kabisa lilikojipigiza kwenye miamba iliyopo kwenye sakafu ya mto huo kiasi kwamba kioo cha mbele kikapasuka na kuwajeruhi vibaya, lakini kutokana na mafunzo ya kikomando waliyopitia vijana hao walijitahidi kupambana na maumivu ya kuchanwa na vipande vya kioo wakachomoka ndani ya gari hilo kwa kupitia kwenye sehemu ya wazi kisha wakaanza kuchapa maji bila kuelewa kila kona wanajeshi wa Kenya walikuwa wametanda!
* * *
Upande wa pili nchini Marekani, Destiny alikuwa anaendelea na masomo ya uandishi wa habari, Jambo ambalo lilikuwa kivutio kwa wengi katika chuo alichokuwa anasoma lilikuwa ni umakini na kufanya kwake vizuri darasani, kila mtihani wa majaribio alikuwa anashika namba moja tu!
“Destiny wewe ni jiniazi.”
“Kwa nini Vicktoria?”
“Uwezo wako darasani si bure!”
“Hapana, nina jibidisha kwenye masomo tu.”
“Mh! Hivyo basi!”
“Ndiyo, hakuna zaidi.” Hayo ndiyo yalikuwa maelezo yake kwa mwanafunzi yeyote aliyejaribu kudadisi juu ya uwezo wake darasani.
Ukweli ni kwamba Destiny hakupoteza hata nukta moja ya muda wake akifanya au kushiriki katika masuala ambayo hayakuwa na faida kwake.
Muda mwingi akiwa chuoni hapo aliutumia kwa kujisomea na kila mara kupitia vyombo vya habari alikuwa anafuatilia matukio mbalimbali yaliyoendelea Afrika ambapo kwenye maombi yake siku zote alimuombea Mtima na Abdulrahman kunusurika katika mipango yote ya kuangamizwa iliyokuwa inapangwa kila kukicha na mataifa mbalimbali ili siku moja azma yake ya kumbadilisha Mtima ifanikiwe.
Siku zikazidi kusonga mbele, hatimaye baada ya miaka miwili kukatika Destiny na wenzake waliojiunga masomo pamoja wakatakiwa kutafuta vituo vya kupatia uzoefu (intership).
Kwa Destiny halikuwa jambo gumu, kutokana na kufanya kwake vizuri darasani pamoja na ukaribu aliokuwa nao na rais wa chuo hicho Profesa Chrstopher Aoun, alipatiwa nafasi katika kampuni kubwa la habari Marekani lililokuwa linamilikiwa na mtangazaji maarufu Wend Williams, liitwalo Wend Productions.
“Natumaini utakuwa mwandishi mzuri siku za usoni,” Profesa Aoun alimwambia Destiny siku wanaagana.
“Kwa nini?”
“Unaijua siri ya mafanikio?”
“Si kweli!”
“Niamini, kupenda unachokifanya ndiyo siri pekee itakayokufanya ufanikiwe kwenye taaluma yako.”
“Asante profesa.”
“Kila la kheri.”
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.