Faiza akatikisa kichwa.
Siwezi kukuacha peke yako. Kama Kaikush atakuja basi atuue sote.”
Nikatazama nyuma tena. Kwa upande wangu nilikuwa nimeshajitolea kuuawa lakini sikupenda yule msichana naye auawe ila alikuwa mbishi.
SASA ENDELEA…
Ingawa mpaka muda ule tulikuwa salama, nilikuwa na uhakika kwamba Kaikush atakapomaliza kumfyonza damu yule askari aliyemkamata atatufuata na sisi. Kwa vyovyote vile, nilijua, asingekubali Faiza atoroshwe.
Kizaazaa ningekuwa nacho mimi niliyekuwa nimefuatana na Faiza.
Niliendelea kuchechemea huku Faiza akinifuata kwa mwendo wa taratibu. Pengine akili yangu ilikuwa tofauti na ya Faiza, mimi nilikuwa nikiwaza kuwa safari yetu haitafika mbali tutakumbana na Kaikush.
Na nilivyokuwa nikiwaza vilikuwa sahihi kwani baada ya mwendo mfupi tu tukauona ule mwanga. Ulitokea ghafla kisha ukapotea hapohapo. Kutahamaki yule jini akawa mbele yetu.
Sikujua ilikuwa zamu ya nani kufa, mimi au Faiza?
Jinsi nilivyoshituka nilipepesuka kama mlevi nikaanguka chini chali. Sikutaka kuinuka kwa vile niliona muda wangu wa kuishi ulikuwa umekwisha. Kwa vyovyote vile, nilishuku jini hilo lisingemuua Faiza kwanza bali lingeniua mimi niliyekuwa naye.
Jini hilo liliniinamia pale chini huku likichanua mikono yake ili linikamate. Mkono wake mmoja ulishika kwenye goti langu lililokuwa linavuja damu na mkono mwingine ulinishika kwenye bega langu.
Ile mikono ilivyokuwa imenishika kwa umadhubuti nilihisi kama nilikuwa nimebanwa na koleo ya umeme.Pale kwenye goti langu palikuwa bado panavuja damu. Lile jini liliishika kisha likaondoa mkono wake haraka na kuutazama kuona jinsi ulivyoingia damu.
Baada ya kutazama mkono huo lilinitazama mimi kisha likamtazama Faiza. Liliona damu kwenye mkono wa Faiza na kwenye gauni alilovaa. Damu hiyo ilikuwa ni ile ambayo Faiza alinipangusa mimi.
Matokeo yake Jini hilo likatoa msonyo mkali na kupotea palepale.
Nilishituka kwa kitendo kile. Nikatupa macho yangu huku na huku, sikuliona. Faiza naye alitazama kila upande kisha akanigeukia mimi.
“Inuka haraka tondoke, limekwenda zake.”
Nikainuka. Sikuweza kujua ni kwa nini jini hilo limeondoka wakati lilikuwa limeshanishika ili linifyonze damu.
Faiza alinishika mkono tukaanza kutembea. Ingawa bado nilikuwa nachechemea nilikuwa nimeongeza kasi ya mwendo.
Kila mara tulikuwa tunatazama nyuma kwani bado nilikuwa na hofu kwamba jini hilo lingeweza kurudi tena. Tulipofika mbali kidogo nikamuuliza Faiza.
“Mbona liliondoka ghafla?”
“Nafikiri ni baada ya kuona damu yako.”
“Baada ya kuona damu yangu ndio limeondoka?”
“Siku moja aliwahi kuniambia kuwa yeye ni jini jamii ya chunusi wanaoishi chini ya bahari.”
Faiza aliendelea kunieleza kuwa majini hao wanaoishi chini ya bahari ndio wanaoua watu wanaoonekana wamekufa maji kwa kuwafyonza damu.
Akaniambia kama mtu anataka kusalimika nao, pale anapomtokea mtu ajikate sehemu ya mwili wake na kiwembe. Jini hilo likiona damu huondoka haraka.
“Nafikiri alipoona damu yako, tamaa ya kukufyonza damu ilimtoka,” Faiza aliendelea kuniambia.
“Kwa hiyo hii damu yangu ndiyo iliyonisaidia?”
“Nafikiri ni hiyo.”
“Kwa hiyo hatarudi tena?”
“Sijui.”
“Sasa kama ameniacha mimi baada ya kuona damu yangu, mbona amekuacha na wewe?”
Faiza akanionesha mkono wake.
“Damu yako si imeniingia na mimi. Imeingia pia kwenye gauni langu,” akaniambia.
“Inawezekana ikawa ni hivyo kwa sababu lilikutazama sana akatoa msonyo na kupotea.”
“Tuombe Mungu lisirudi.”
Faiza aliponiambia hivyo nikatazama nyuma.
“Linaweza lisirudi. Lakini nashangaa sana, yeye anafyonza damu halafu akiona damu anaondoka!”
“Yeye anataka akutoboe mwenyewe. Ukijitoa mwenyewe damu hataki. Aliwahi kuniambia hivyo siku moja.”
“Basi imekuwa nusura kwetu, tuombe Mungu tutoke salama.”
“Inshaallah tutatoka salama.”
Nilitazama tena nyuma kabla ya kuendelea na safari. Kila nilipotazama nyuma Faiza naye aliiga.
Licha ya kupata matumaini kutokana na maelezo ya Faiza, bado moyo wangu ulikuwa na chembe ya hofu. Nilikuwa nikijiambia tutakapofanikiwa kutoka salama ndani ya lile pango ndio ningeamini kuwa tumepona.
Safari ilikuwa bado ndefu. Lile pango lilikuwa na taswira ya kutisha hasa kutokana na yale mauaji ya wenzetu yaliyotokea.
Ghafla tukaanza kukutana na vitu vilivyotuongezea hofu.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.