Mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe.
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
WIKI iliyopita, Yanga ilifunga dirisha dogo la usajili kwa kumsajili, aliyekuwa mshambuliaji wa Mwadui FC ya Shinyanga, Paul Nonga na kumpa mkataba wa miaka miwili.
Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba, mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amedai kuwa hamjui kabisa mchezaji huyo zaidi ya kumsikia tu baada ya kusajiliwa na klabu hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Tambwe alisema kuwa siyo kwamba anafanya makusudi ila ni kweli kabisa hamjui Nonga kwa sababu huwa hana tabia ya kumfuatilia mtu uwanjani zaidi ya kuipigania timu yake kuhakikisha inaibuka na ushindi.
“Kusema kweli Nonga simjui ila nimemsikia tu baada ya kusajiliwa na Yanga hivi karibuni na hata tukikutana njiani, labda yeye ndiye aanze kuniita.
“Hata hivyo, kesho (leo) kama atakuja mazoezini basi hiyo ndiyo itakuwa nafasi yangu ya kumjua,” alisema Tambwe ambaye juzi Jumamosi alipiga hat-trick yake ya tano tangu alipotua hapa nchini akitokea Vital’O ya Burundi.
Katika hatua nyingi, Tambwe alisema kuwa licha ya kutomjua Nonga lakini haogopeshwi na ujio wake klabuni hapo kwani anajiamini kuwa yupo vizuri.
“Mimi nipo vizuri, najiamini, hivyo yeye aje tuweze kushirikiana kuhakikisha Yanga inatetea ubingwa wake, kuhusu kucheza au kutocheza anayejua hilo ni kocha, hivyo binafsi nitahakikisha najifua vilivyo ili kulinda kiwango changu,” alisema.
Hadi leo hii, Simba wengi wamekuwa wakijutia kitendo cha kuachana na Tambwe na kila anavyozidi kufanya mambo makubwa uwanjani, wamekuwa wakiumia.