Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi na viongozi wa juu wa usalama, wamepeana saa 72 kuhakikisha ukweli unafahamika kuhusu kilichojificha nyuma ya mauaji hayo na tayari kuna kila dalili ya siri kufichuka.
Grace na Magesa bado wapo mafichoni Mombasa nchini Kenya na tayari Grace ameshaanza maandalizi ya wawili hao kuondoka nchini humo na kuelekea sehemu nyingine tofauti.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Wakati wakiendelea kuhangaika huku na kule, Mandiba aliwapigia simu vijana wake wengine waliotumwa kuifuatilia laptop ya marehemu Mwampashi ambapo GPS (Global Positioning System) ilikuwa inaonesha kwamba ipo Mwenge.
“That is the only chance which we have right now! Don’t mess up you guys!” (Hiyo ndiyo nafasi pekee tuliyonayo kwa sasa, msije mkafanya uzembe vijana) alisema Mandiba kwa msisitizo wakati akizungumza na vijana wake hao kwa simu.
Kwa bahati nzuri, vijana hao walifanikiwa kufika kwenye duka lililokuwa likiuza kompyuta, laptop na simu zilizotumika la Planet Link Used Computers and Accesories ambapo baada ya kujitambulisha na kuonesha vitambulisho vyao, wahudumu wa duka hilo waliwakutanisha na bosi wao, Barick Mmbaga ambaye aliwasikiliza kwa makini na kuwaahidi ushirikiano wa kutosha.
“Huwa mnanunua wapi hizi kompyuta zenu?”
“Huwa tunaagiza kutoka nje ya nchi hususan Thailand, China na Taiwan. Wakati mwingine huwa tunanunua kutoka kwa watumiaji wa hapa nchini ambao wanakuwa wamechoka kutumia kompyuta au laptop zao na kuhitaji kubadilisha nyingine za kisasa zaidi.”
“Huwa mnafuata sheria za nchi kwa kiasi gani katika biashara zenu?”
“Huwa tunafuata sheria zote mkuu, kuanzia kulipia leseni halali ya biashara, kulipia kodi na ushuru mizigo inayoingia bandarini.”
“Huwa mnahakikisha vipi kama mali mnazonunua zimepatikana kihalali na si za wizi?” Mmbaga aliulizwa swali ambalo lilimfanya ababaike kidogo. Hata hivyo, kwa kuwa kilichowaleta hapo hakikuwa hicho na walishapewa tahadhari na bosi wao, Mandiba kuhakikisha hawafanyi uzembe wowote, waliamua kumueleza Mmbaga kilichowapeleka dukani kwake.
“Kuna laptop iliibwa kwenye tukio la mauaji ya raia mmoja na katika uchunguzi wetu inaonekana ipo humu ndani kwenye duka lako, tunaihitaji haraka.”
“Lakini wakuu, humu ndani kuna zaidi ya laptop themanini, mtaijuaje?”
“Hiyo siyo kazi yako,” alisema mmoja kati ya wale vijana, kazi ya kuzipangua ikaanza mara moja huku wakiwasiliana na wenzao waliokuwa makao makuu kupitia vifaa maalum vya mawasiliano.
Baada ya kupekuapekua kwa muda, hatimaye walifanikiwa kuipata laptop hiyo, wakawasiliana tena na makao makuu ambapo baada ya kuridhika kwamba ndiyo yenyewe, waliondoka huku wakimtaka Mmbaga kuwa tayari kutoa msaada muda wowote atakaotakiwa kufanya hivyo.
Kwa kasi ya kimbunga wakaondoka na laptop hiyo na kurejea makao makuu ambako waliwakuta wenzao, akiwemo Mandiba wakiwasubiri kwa shauku kubwa. Harakaharaka laptop hiyo ikachomekwa kwenye umeme na kuwashwa. Kwa kuwa nayo ilikuwa na ‘password’ kama ile ya mwanzo, ilibidi mbinu zilizotumika mara ya kwanza zitumike pia kuifungua.
Programu maalum za kompyuta ziitwazo PowerISO na Password Cracker zikatumika na muda mfupi baadaye, tayari laptop ilikuwa imewaka.
“All the data in hard disc drive has been formated, we need a recovery softaware and Recuva Pro is the best,” (Taarifa zote kwenye kompyuta zimefutwa, tunahitaji programu maalum ya kuzirejesha na Recuva Pro ndiyo bora zaidi) alisema mtaalamu mmoja kutoka tume ya mawasiliano aliyekuwa akishirikiana nao.
Bila kupoteza muda wakaianza kazi ya kurudisha taarifa zote kwenye laptop hiyo huku pia wakiwa makini kuhakikisha hakuna udukuzi (hacking) inayotokea kama ilivyokuwa mwanzo. Kila mtu ndani ya ofisi hiyo alikuwa bize na ndani ya dakika zisizozidi thelathini, zaidi ya asilimia tisini ya taarifa zote zilizokuwa zimefutwa kwenye laptop hiyo zilirejeshwa.
Wakaanza kazi ya kuzihamisha kutoka kwenye laptop hiyo kwenda kwenye ‘server’ maalum ili isiwe rahisi kuharibiwa tena kama ilivyokuwa mwanzo. Kama walivyobaini awali kwenye laptop ya Magesa kabla taarifa zake hazijaharibiwa na mitambo ya kisasa, mawasiliano ya mwisho kati ya wawili hao yalikuwa ni kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa bahati nzuri zaidi, kwa kutumia laptop hiyo ya marehemu Mwampashi walifanikiwa kuipata ripoti kamili ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo tayari Mandiba alishahisi kwamba ndiyo iliyokuwa na siri ya kifo cha Mwampashi.
* * *
“Hatutakuwa na muda wa kuendelea kukaa sana hapa, kuna sehemu nyingine tutakwenda, mbali kabisa na hapa,” alisema Grace baada ya kuhakikisha ameweza kudhibiti taarifa zilizokuwa kwenye laptop ya Magesa.
“Kwa nini tuondoke wakati hii inaonekana ni sehemu salama?”
“Ni sehemu salama ndiyo lakini masharti ya kazi zetu hutakiwi kukaa sehemu moja kwa muda mrefu, isitoshe nimepangiwa kazi nyingine sehemu nyingine tofauti,” alisema Grace, Magesa akabaki na maswali mengi lakini mwanamke huyo mrembo hakuwa tayari kumfafanulia kila kitu.
Siku tatu baadaye, Grace alimshtukiza Magesa na kumwambia ajiandae kwa sababu siku ya safari ilikuwa imeshawadia. Magesa akabaki amepigwa na butwaa kwa sababu hakuona sababu yoyote ya kuishi kwenye ulimwengu usiotabirika kiasi hicho.
“Nivaeje?”
“Nimeshakuandalia nguo, hebu fungua kabati,” alisema mwanamke huyo huku akikusanya vitu vyake harakaharaka, Magesa akafungua kabati na kukutana na mavazi kama yale wavaayo wanaume wa Pwani, kanzu fupi, suruari, baraghashia na kikoi. Harakaharaka akavaa na kujitazama nyuma ya kioo, alikuwa amebadilika mno kiasi kwamba isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kumtambua.
Dakika kadhaa baadaye, walitoka huku Grace akiwa amebeba begi dogo lililokuwa na vifaa vyake muhimu, akiwa amevalia nikabu na baibui vilivyoacha wazi sehemu ya macho tu. Wakatoka mpaka nje ya jengo hilo na kuita teksi, Grace akamuelekeza kuwapeleka kwenye Uwanja wa Ndege wa Mombasa, jambo alilolitii.
Safari ikaanza na dakika kadhaa baadaye, tayari walikuwa Uwanja wa Ndege wa Mombasa, wakateremka na kumlipa dereva fedha zake, Grace akamuongoza Magesa kuelekea ndani ya uwanja huo huku muda wote Magesa akigeuka huku na kule kushangaa mazingira.
“Hebu acha kushangaashangaa, utasababisha tushtukiwe sasa hivi, kama huwezi ni bora utazame chini,” alisema Grace kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na hata chembe ya masihara, ikabidi Magesa atii na kujikaza kiume.
“Vitambulisho vyenu na hati za kusafiria tafadhali,” askari wa uhamiaji aliyekuwa pale mapokezi alisema kwa sauti iliyosikika vyema baada ya zamu ya Magesa na Grace kuwadia. Harakaharaka Grace akatoa vyote na kuviweka juu ya meza, yule askari akavichukua na kuvitazama kwa makini, kimoja baada ya kingine kisha akawakazia macho Magesa na Grace.
“Hebu ingieni ndani,” alisema askari huyo huku akiinua mkonga wa simu na kuanza kuzungumza na upande wa pili, Magesa na Grace wakabaki wakitazamana.