×

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 42

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Kikosi kingine cha askari kikaingizwa ndani ya pango hilo kuhakikisha kama wale watu tuliosema wameuawa, wameuawa kweli. Askari hao waliambiwa kama watakuta maiti zao watoke nazo.

Baada ya mawasilino kufanyika, gari la hospitali likawasili, Waandishi wa habari na wananchi walikuwa wametuzonga wakituhoji maswali lakini polisi waliwaondoa.
Tukapakiwa kwenye gari la hospitali na kupelekwa Hospitali ya Bombo ya jijini Tanga.
SASA ENDELEA…

Wakati tunafikishwa katika Hospitali ya Bombo tulikuta makundi ya watu ambayo tulielezwa kuwa walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kutuona sisi baada ya taarifa za kutolewa kwetu katika mapango kuwafikia watu.

Kumbe wakati tukiwa mle mapangoni tayari habari zilikuwa zimeenea jijini juu ya kukwama kwetu ndani ya mapango hayo.

Hivyo taarifa za kuokolewa kwetu zilienea haraka jijini na watu wakaona mahali pekee ambapo wanaweza kutuona ni katika Hospitali ya Bombo.

Gari tulilopakiwa liliposimama kwenye geti, watu walikimbilia kwenye madirisha kutuchungulia. Faiza alikuwa akiwapungia mkono.

Mara tu baada ya kuingizwa hospitalini humo, Faiza alipelekwa katika wodi ya wananawake na mimi nilipelekwa katika wodi ya wanaume.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya zetu, tuliwekewa maji kwa vile tulionekana tulikuwa dhaifu mno. Watu hawakuruhusiwa kuja kututazama. Ilionekana kungetokea fujo ndani ya wodi kwa vile watu hao walikuwa ni wengi.

Licha ya kuwekewa maji, nililetewa chakula pamoja na maji safi. Wakati ninakula viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Tanga kuanzia mkuu wa wilaya walikuja hospitali kutujulia hali.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga ambaye alikuwa ni mwanamke alishangaa nilipomueleza kuwa nilikaa katika mapango ya Amboni kwa siku kadhaa ambapo nilimkuta mwanamke aliyekaa kwa miaka minne.

“Mimi nilidhani ni habari ya uongo, kumbe ni kweli! Nini kilitokea mpaka ukakwama ndani ya hilo pango?” akaniuliza.Nikamueleza mheshimiwa huyo kilichotutokea. Wakati wote alikuwa akitikisa kichwa kwa mshangao huku akisikitika.

Ile habari ya jini aliyekuwa ndani ya pango ndiyo iliyomshangaza zaidi. Kwanza alionekana kutotaka kuonesha kuwa anaamini habari za majini kwa vile alikuwa mwanasiasa lakini baadaye habari hizo zilimuingia akaacha mdomo wazi.

“Kwa hiyo imethibitishwa kuwa hao watu wote wamekufa?’ Mkuu huyo wa wilaya akaniuliza.
“Wamekufa wote.”

“Wewe ulimuona huyo jini kwa macho yako akiwafyonza damu hao watu?’
“Nilimuona kwa sababu nilikuwemo ndani ya hilo pango.”
“Yesu wangu!”
Baada ya kimya kifupi mkuu huyo wa wilaya akaniambia.
“Poleni sana jamani.”

“Asante, tumeshapoa.”
“Ngoja twende kwa huyo mwenzako uliyekuwa naye.”
Wakaondoka na maafisa wake aliokuja nao.

Baadaye alifika kamanda wa polisi wa mkoa. Naye aliniuliza maswali yake. Alipoondoka akaja afisa upelelezi na timu yake ya makachero.
Walinipiga picha kisha wakachukua maelezo yangu. Nilihojiwa kwa karibu saa mbili.
Kitu ambacho walikuwa hawataki kukiamini ni maelezo yangu ya jinsi nilivyoishi katika pango lile kwa siku kadhaa.

“Kuna hewa ya kutosha ya kukufanya uweze kuishi kwa siku zote hizo?” Kachero mmoja akaniuliza.
“Hewa inapatikana na ndiyo maana nimeweza kuishi.”
“Ni ajabu.”

“Acha mimi, kuna msichana ambaye amenieleza kuwa ameishi kwa miaka minne.”
“Tunataka maelezo yako wewe binafsi, yeye naye tutakwenda kumhoji tupate ukweli wake.”
“Sawa.”
“Kwa hiyo umesema kwamba wenzako uliopotea nao ndani ya hilo pango waliuawa?’
“Ndiyo waliuawa.”

“Na wale watu walioingia kuwatoa pia waliuawa?’
“Ndiyo waliuawa.”
“Waliuawa na nani?”
“Waliuawa na jini.”

“Unaposema jini una maana gani?”
“Nina maana ya jini. Mimi nadhani hakuna mtu asiyejua jini.”
“Mimi simjui kwa sababu sijakutana naye.”
“Sasa sijui nitakueleza nini!”
“Utueleze aliyewaua wale watu.”
“Ni jini!”

“Jini ni nani?”
“Yule msichana niliyekuwa naye anaweza kuwaeleza vizuri kuhusu huyo jini kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akiishi naye ndani ya lile pango.”
“Wewe ulimuona kwa macho yako huyo jini?”
“Ndiyo nilimuona”

“Yukoje?”
“Ni kama binadamu lakini anatisha.”
“Unajua ninakuuliza maswali mengi kwa sababu tukio lenu limehusisha vifo vya watu wengi. Kwa hiyo ni lazima tupate maelezo ya kina.”
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave a Comment