×

Bosou aipa Yanga sare

Vicent-BosouSweetbert  Lukonge, Zanzibar

AZAM FC imejiweka katika nafasi ngumu ya kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya usiku wa kuamkia leo kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga kwenye Uwanja wa Amaan.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kuongoza katika Kundi B, ikiwa na pointi nne ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye pointi kama hizo ambayo jana jioni iliifunga Mafunzo bao 1-0. Azam ni ya tatu ikiwa na pointi mbili.

Katika mchezo huo wa Kundi B, uliotawalia na vituko na ubabe kwa wachezaji wa timu zote mbili ulihudhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki kutokana na upinzani wa timu hizo katika siku za hivi karibuni.

Kipindi cha kwanza, Azam ilionekana kulinda zaidi lango lake huku Yanga ikifanya mashambulizi kadhaa lakini washambuliaji wake hawakuwa makini na kushindwa kufunga.

Azam ilionekana kumudu mashambulizi ya Yanga huku yenyewe ikifanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hayakuwa na madhara. Hadi mapumziko timu hizo zilikwenda zikiwa sare.

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na straika Kipre Tchetche dakika ya 58, baada ya kuiwahi pasi aliyopenyezewa kutoka katikati ya uwanja na kupiga shuti kali akiwa katikati ya mabeki watatu wa Yanga na kufunga.

Yanga ilijitahidi kusawazisha bao hilo lakini safu ya ulinzi ya Azam ikiongozwa na beki wa kati Pascal Wawa ilikuwa makini kuondoa hatari zote zilizoelekezwa kwao.

Hata hivyo mchezo huo ulikuwa ukisimama mara kwa mara kutokana na vurugu za hapa na pale miongoni mwa wachezaji hali iliyosababisha nahodha wa Azam, John Bocco kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 65 kutokana na utovu wa nidhamu.

Baadaye Azam iliwatoa Tchetche na Ramadhan Singano na kuwaingiza Frank Domayo na Didier Kavumbagu, huku Yanga ikiwatoa Pato Ngonyani na Amissi Tambwe na kuwaingiza Vincent Bossou na Paul Nonga.

Yanga ndiyo iliyofaidika na mabadiliko hayo, kwani ilisawazisha dakika ya 83 kwa bao lililofungwa na Bossou akiunganisha mpira uliopigwa na Simon Msuva. Bao hilo kidogo lizue mzozo kwani beki wa Azam aliokoa mpira huo ukiwa umeshavuka mstari wa goli.

Leo katika michuano hiyo, Simba itacheza na JKU usiku saa 2:15 katika mchezo wa Kundi A, huku jioni saa 10:30, Jamhuri ikicheza na URA ya Uganda.

Uchawi watawala:

Kabla ya mchezo huo makomandoo wa timu zote mbili walitunishiana misuli katika lango la wachezaji la kuingilia na kutoka uwanjani kutokana na imani za kishirikina.

Mzozo wa kwanza uliibuka kabla ya kuanza kwa mchezo huo ambapo makomandoo hao walikunjana mashati kabla ya kutulizwa na polisi waliokuwepo uwanjani hapo.

Wakati timu hizo zikielekea mapumziko, mzozo uliibuka tena ambapo makomandoo wa timu zote mbili walishikana tena baada ya kutuhumiana kwa imani za kishirikina lakini kwa mara nyingine polisi waliwatuliza.

Morris azuiwa, asusa

Beki wa Azam, Aggrey Morris, jana alizuiwa kuingia uwanjani na maofisa wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi kwa sababu zisizojulikana na hata alipojitambulisha hakueleweka.

Maofisa walisema, Morris alipaswa kupanda basi la wachezaji wa Azam kuingia uwanjani hapo lakini naye alijibu kuwa, hayupo kambini kwa kuwa ni majeruhi na aliumia wakatia akiitumikia timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.

“Mnanizuia kwani hamnijui, mimi nimeumia nikiitumikia Zanzibar Heroes sasa sipo kambini mtaniambiaje nipande basi la Azam? Kama mnashindwa kunithamini basi sitaichezea timu ya taifa tena,” alisema Morris na kuondoka zake.

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Comment