×

Jamani Kaka Cheni …Ndiyo Nini Sasa?!-0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Na ikitokea umetoka kwa kuiba, ole wako,” alidakia mama ili asije akaonekana hana kauli kwa mtoto…
“Umenielewa?” alisema kwa kufoka baba.
“Nimekuelewa baba.”

“Hodi,” yaani ile kaka Cheni anamaliza kusema nimekuelewa baba, Chausiku, binti mmoja hivi, alikwendaga kujiuza Dodoma, alitokea akiwa amevaa nusu utupu.
SHUKA MWENYEWE SASA…

“Shikamoo baba…shikamoo mama,” aliamkia Chausiku. Bahati njema wazazi wote wanamfahamu, wakamwitikia, mama akadakia hapohapo…
“Umemfuata nani wewe Chausiku?”
“Huyu,” alisema akininyooshea mkono mimi.
“Hapo sawa. Nilidhani umemfuata Cheni. Cheni hana nafasi siku hizi, kazi nyingi. Hatakiwi kuondoka hapa nyumbani.”

Mama alipotoa kauli hiyo, Chausiku alimtazama kwa jicho lililosema ‘ukiwa na mama kama huyu ni shida’ kisha akasema;
“Najua mama!”
“Unaposema unajua nani kakuambia kwamba siku hizi Cheni ana kazi nyingi?” mama akamwuliza Chausiku.

“Najua tu!” Chausiku akamjibu mama.
“Haya kama unajua ndiyo hivyo, Cheni hawezi kutoka hapa, mambo ya kutokatoka ovyo nyumbani ilikuwa zamani, sawa Chausiku?” mama aliyekuwa anajua uhusiano uliokuwepo kati yake na Cheni alimpasha.

Kutokana na mama kutoa kauli hiyo, niligundua Chausiku ambaye kwa sehemu alikuwa fyatu angemjibu mama halafu ingekuwa balaa, nikampa ishara anifuate.

Nilitoka na Chausiku hadi nje huku wazazi wakimwangalia kwa masikitiko…
“Hivi nikwambie pale limenishuka. Sikutarajia kama nitawakuta wazazi wako wakiwa na Cheni. Kwa heri mwaya, mwambie Cheni anitafute baadaye,” alisema Chausiku na kuondoka, nikamwambia sawa.

“Mh! Leo kaka Cheni kapatikana, kwa ninavyomuelewa roho inamuuma sana kumkosa Chausiku aliyejileta mwenyewe, na hivi hakuwepo huko chumbani kwake ingekuwa kasheshe,” nilijisemea moyoni.

Sikuishia hapo, nikakumbuka siku aliyokuwa na demu wake chumbani kwake alivyoniweka katika wakati mgumu mpaka nami nikafika mwisho wa safari, nikaishia kutabasamu.

Baada ya kurudi ndani, baba akaniambia kuanzia siku hiyo ananipiga marufuku kuondoka nyumbani bila ruhusa na ikitokea akagundua, itakula kwangu…
“Sawa baba, nimekusikia,” nilikubali.
“Halafu urafiki na wasichana wahuni kama hawa sitaki,” alidakia mama…
“Sawa mama, nimesikia.”

“Wewe sema umesikia halafu nije nikufume bado unaendelea na urafiki wenu, utatambua kama mimi ndiye nilikuweka tumboni miezi tisa…”
“Mama sitafanya hivyo, nimekuelewa.”
***
Ilipita wiki moja tangu wazazi wampige marufuku kaka Cheni kutoka nyumbani. Siku hiyo, mama na baba walikwenda kijiji cha mbali kidogo, kulikuwa na harusi ya mtoto wa mjomba wangu.
Nyumbani nikabaki mimi na kaka Cheni…
“Sista,” aliniita kaka…
“Niambie…”

“Mimi nataka kuleta mgeni wangu hapa, sasa ole wako uje kumwambia baba au mama…utanijua mimi ni nani hapa duniani…”
“Usinitwishe mzigo kaka Cheni. Kila unalolifanya lifanye kwa binafsi yako. Ukijulikana msala ni wako, mimi sihusiki kwa lolote lile,” nilimwambia.
“Je, ukija kuulizwa kama nilitoka utajibuje?”
“Nitasema ukweli.”

“Upi?”
“Kwani wewe unataka kufanyaje sasa hivi?”
“Nataka kutoka…”
“Sasa huujui ni ukweli gani nitakaousema?”

Nilimwona kaka Cheni anakuwa mpole. Ukweli ni kwamba, tulikuwa tukimwogopa sana baba. Ndiyo maana hakuna aliyekuwa na uwezo wa kwenda kinyume na maagizo yake. Sasa alichokuwa anataka kukifanya kaka Cheni ni kujiingiza yeye kwenye songombingo na baba pia kuniingiza na mimi kama itatokea atajulikana…

“Poa tu bwana…baba anaweza akaja ghafla halafu kikaninukia,” alisema…
“Sasa wewe kaka Cheni kumbe unajua, unataka kimnukie nani?” nilimuuliza kwa ukweli kutoka moyoni.

Aliniangalia kwa hasira sana, macho yalimtoka…
“Kwanza we unaonekana hata nikileta demu utasema…”
“Itategemea…mademu wenyewe kama akina Chausiku hawa, nitasema tu.”
Ghafla nikamwona kaka Cheni akinifuata kwa macho juu, akanishika na kunisukumia ukutani. Nilianguka, akanikaba huku akiniambia…

“We ni mjinga. Wasichana wenzako wote wanawapenda mawifi zao wewe unamchukia Chausiku. Dada gani wewe?”
“Niache kaka Cheni…nimesema niache.”

Nilimsukuma, akaangukia huko, nikasimama na kukimbilia chumbani kwangu. Akanifuata. Nilijitupa kitandani, akaja na kuniminya huku akinishika mikono yote. Nikamkumbatia kwa nguvu, akaachia tabasamu.

Je, unajua nini kiliendelea huko? Usikose kusoma kwenye gazeti hilihili, wiki ijayo.

Leave a Comment