Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas alipoeleza kwamba wakati akiwa kule kijijini alikuwa akienda kuhudhuria kliniki alikopimwa na kuelezwa mtoto alikuwa akiendelea vizuri na kupewa maelezo mengine yaliyohusiana na masuala ya uzazi. Je, kiliendelea nini? Songa mbele…
Hata hivyo, kitendo cha kutelekezwa na mama kule kijijini kilinifanya muda mwingi kuwa katika msongo wa mawazo na kujiuliza ilikuwaje mama aliyenishauri nikakae kule na aliyefahamu hali niliyokuwanayo anifanyie vile?
Kutokana na msongo wa mawazo niliokuwanao, yule mama wa kwanza kufika pale nyumbani kwa bibi alinigundua, mara kwa mara nikawa nakwenda kwake kwa ajili ya mazungumzo nk.
Licha ya kufanya hivyo, aliponiuliza kuhusu mwanaume aliyenipatia ujauzito sikuthubutu kumtaja Evance kama mama alivyoniomba nisimtaje kuhofia mwanaye kupata matatizo ya kisheria.
Niliishi kule kijijini hadi ujauzito wangu ulipofika miezi tisa bila mama wala mdogo wake kuja kuniona, siku moja usiku nilipatwa na uchungu lakini kwa kuwa kituo kikubwa cha afya ambacho kinatoa huduma za uzazi kilikuwa mbali, chupa ya uzazi ilipasuka nikiwa nyumbani.
Baada ya tukio hilo sikukaa muda mrefu kwa msaada wa bibi na jirani zake wawili nilijifungua mtoto wa kiume, kama inavyokuwa karibu kwa wanawake wote, licha maumivu kitendo cha kupata mtoto kilinifurahisha sana.
Akina bibi walinihudumia vizuri na kulipokucha tuliondoka pale kijijini kwa usafiri wa baiskeli mbili nikapelekwa katika kituo cha afya kilichotoa huduma ya uzazi.
Kwa kuwa nilijifungulia nyumbani, nilifanyiwa uchunguzi kama nilipata maambukizo yoyote lakini ilibainika nilikuwa salama mimi na mwanangu.
Hata hivyo, nilikaa pale hospitali kwa muda wa siku tatu ndipo niliruhusiwa kurudi nyumbani, bibi alinihudumia vizuri kama mzazi lakini tatizo sikuwa na nguo za kumvalisha mwanangu kwa sababu sikuwa na fedha.
Kutokana na hali hiyo, nilikuwa namfunga kanga zangu na za bibi, ila yule mama niliyekuwa napenda kwenda kwake aliniletea nguo kadhaa za mtoto.
Kwa kuwa nilihitaji sana kumuona mama na kuzungumza naye kuhusu hatima yangu na masomo, nilimuuliza bibi kama alimtumia ujumbe kwamba nilijifungua, alisema alifanya hivyo na angefika muda wowote.
Hata hivyo, nilikaa majuma matatu, si mama wala mama mdogo aliyetokea nikaendelea kuishi katika mazingira magumu na mwanangu hadi nilipomaliza mwezi.
Kwa kuwa afya ya mwanangu na yangu zilikuwa nzuri, nilizungumza na yule mama jirani wa bibi anikopeshe fedha ili niweze kwenda mjini ambazo angerudishiwa na mama.
Mama huyo aliyekuwa akitegemea kupata fedha kwa kuuza mazao wakati wa minada, akaniambia nisubiri kama angezipata angenipatia tena bila kunikopesha kwa sababu alikuwa ananionea huruma maisha niliyoishi kule kijijini na mwanangu.
Hata kabla ya kunipatia fedha hizo, nilimshukuru kwa ukarimu wake nikamwambia nitamsubiri mpaka atakapozipata, maisha yakaendelea.
Niliendelea kuishi huku nikisubiri kupewa nauli na yule mama na kufikisha mwezi mmoja na nusu, siku moja usiku mwanangu alipatwa na homa ya mapafu (Nimonia) akawa anashindwa kupumua vizuri.
Kwa kuwa ilikuwa usiku ilituwia vigumu kutoka kwenda hospitali tukaamua kusubiri kuche ndipo tumpeleke lakini ilipofika saa tisa kuelekea saa kumi alfajiri mwanangu alifariki dunia.
Awali sikufahamu kama mwanangu alifariki hadi bibi alipokwenda kuwaamsha majirani ambapo alikuja babu mmoja na mkewe, bwana mmoja aliyekuwa akipenda kuniita mjomba na yule mama aliyeniahidi kunipatia nauli ya kwenda mjini.
Baada ya kuzungumza na bibi ndipo yule mama aliniambia mwanangu alifariki dunia hivyo niwe jasiri kwa sababu ilikuwa bahati mbaya.
Taarifa hiyo ilinihuzunisha nikaanza kulia kwani licha ya changamoto nilizopitia nilimpenda sana mwanangu na sikuhitaji kumpoteza, akina bibi waliendelea kunifariji.
Hata hivyo, nilimchukia sana mama pamoja na Evance kwa vitendo walivyonifanyia, mama kunipeleka kijijini na kunitelekeza na kijana wake kunibaka na kunipa ujauzito.
Pamoja na chuki niliyokuwanayo, sikutaka kumuonesha mtu yeyote hali hiyo zaidi ya kusema siku moja Mungu angenilipia kwa ukatili niliofanyiwa, nilipomkumbuka mama maumivu yalizidi kuwa makali nikajikuta nalia kwa sauti.
Tangu muda alipofariki mwanangu, hatukulala kwani muda mwingi nilikuwa nikilia.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.