Amani James a.k.a Chiba akifanya yake
Makala: IMELDA MTEMA
Kama umeshamuona jamaa mlemavu wa mguu ambaye ni bonge la dansa katika Kundi la Muziki wa Dansi la Yamoto Band na kujiuliza ni nani, leo unapata jibu kupitia Risasi Jumamosi.
Ukweli ni kwamba jamaa huyo ni kijana machachari ambaye amezidi kuongeza ladha kwenye kundi hilo kutokana na umahiri wake wa kucheza huku akitumia mguu mmoja tu anapokuwa stejini lakini nje ya jukwaa hawezi kutembea bila gongo (fimbo).
Mkali huyo anakwenda kwa jina la Amani James a.k.a Chiba. Kwenye spesho intavyu na gazeti hili, Chiba amefunguka kuwa hakuna kitu anachojivunia kama sanaa yake japokuwa ni mlemavu huku baadhi ya watu wakiamini kuwa hawezi kufanya chochote zaidi kuomba.

ALIINGIAJE YAMOTO BAND?
“Nilikuwa nipo nyumbani kwetu Lindi. Kuna kipindi alikuja Mkubwa Fella (Said Fella), akaniona na kipaji changu (cha kuimba), akanikubali na kuniahidi kuwa atakaporudi atanichukua nikajiunge na kundi hilo hivyo tuliachiana mawasiliano. Mkubwa alikuwa akinipigia mara kwa mara ndipo aliporudi tena na kunichukua kunileta huku Dar.
ALIKUWA AKIIMBA TANGU ZAMANI?
“Nakumbuka ilikuwa baada tu ya kumaliza darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo. Baba yangu aliniambia nikae naye pale Lindi Mjini. Nilijifunza ufundi wa magari na kila ilipofika jioni nilikuwa nakwenda kwenye mazoezi ya kucheza muziki kwani tulikuwa tukicheza kwenye maharusi mbalimbali na hata sherehe ndogondogo.
VIPI KUHUSU MGUU WAKE, ALIZALIWA HIVYO AU?
“Hapana. Sikuzaliwa hivi. Nilizaliwa mzima kabisa ila nilipata ajali ya gari ndipo nilipokatwa mguu wangu (anasikitika). Siyo muda mrefu sana. Ni miaka mitatu tu iliyopita.
“Nilipopona niliendelea na kazi yangu ya muziki, tena kwa kasi ya ajabu kwa kuwa niliona nikikata tamaa ndiyo utakuwa mwisho wangu. Pia sikupenda niwe ombaomba katika maisha yangu.
ANAWEZAJE KUCHEZA JUKWAANI BILA MAGONGO?
“Dah! Mungu ni mkubwa sana. Anaweza akakunyima hiki akakupa kile. Kama ulivyosema, kweli mimi jukwaani huwa situmii magongo kabisa lakini katika kutembea kawaida lazima nitumie magongo. Hapo ndipo uone maajabu yake na hata nilivyokatwa mguu huko kwetu ndiyo nilizidi kuwa maarufu kwa maana watu walikuwa wananipenda sana.
VIPI KUHUSU FAMILIA, AMEOA?
“Bado sijaoa ila nina mtoto mmoja na bado natafuta maisha kwanza ndipo nifikirie jinsi ya kuoa na kuwa na familia yangu mwenyewe ambayo nitaweza kuimudu bila tatizo lolote.
ILIKUWAJE MPAKA AKAPATA SAFARI YA AFRIKA KUSINI ‘SAUZ’?
“Tayari mimi ni memba wa Yamoto Band hivyo kutokana na bidii yangu, wakati wanaondoka kwenda Sauz tuliondoka wote kwa pamoja. Aisee nilifurahi sana kwa sababu nilijua nathaminika na nilizidi kujituma siku hadi siku.
ANAPELEKA SHUKURANI ZAKE KWA NANI?
“Baada ya Mungu, kwa kweli hakuna mwingine zaidi ya kiongozi wetu, Mkubwa Fella. Yaani amebadilisha kabisa maisha yangu. Nimekuwa wa tofauti kabisa na ninapendwa sana kila kona na watu wote. Kimsingi na mimi nawapenda mashabiki wangu na nawaomba wazidi kunisapoti kwani sitawaangusha.”