×

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 44

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Baada ya kuzungumza kwa kirefu, Faiza aliwaleta ndugu zake katika wodi niliyokuwa nimelazwa.Faiza aliwatambulisha kwangu na wote wakanikumbatia na kunipa pole.

SASA ENDELEA

Faiza aliwaeleza kuwa kama si mimi na wenzangu kuingia ndani ya pango lile na kwenda kumgundua huko alikokuwa amewekwa, angeendelea kuishi humo humo hadi kifo kingemkuta.

Akawatoa ndugu zake machozi alipowaeleza jinsi wenzangu walivyouawa mmoja baada ya mwingine wakati mimi na yeye tukiwa katika harakati za kutoroka ndani ya lile pango.

Na kwa upande wangu nilimsifu Faiza kwa ujasiri aliokuwa nao, si tu kwa kuishi ndani ya lile pango kwa muda wote aliokuwamo bali pia kwa kunipa moyo na ushirikiano hadi tukafanikiwa kutoka.

Wakati tunazungumza na ndugu zake Faiza, waandishi wa habari wakaingia ghafla. Sikuweza kujua ni nani aliwapigia simu na kuwajulisha kuwa ndugu wa Faiza walikuwa wamefika hapo hospitalini kutoka Bagamoyo.

Walitupiga picha na kuzungumza na ndugu zake Faiza pamoja na Faiza mwenyewe.
Baada ya kutosheka na maelezo waliyopata, wakazungumza na mimi.
Waliniuliza kama ndugu zangu walipata habari na kuja kuniona hapo hospitali. Nikawajibu kuwa mpaka muda ule sijamuona ndugu yangu yeyote na sikuwa na uhakika kwamba wamesoma habari zangu kwenye magazeti.

Waandishi hao walipoondoka, ndugu zake Faiza waliniambia kwamba hawataondoka Tanga mpaka Faiza aruhusiwe na waondoke naye kurudi Bagamoyo.
“Hatujui tutaruhusiwa lini,” nikawaambia.

“Lakini tunaona mko vizuri, mnaweza kuruhusiwa kama mtaomba ruhusa,” dada yake Faiza aliyekuwa akiitwa Latifa aliniambia.

“Tutawauliza madaktari kama wataturuhusu itakuwa bora. Sasa mtakwenda kulala wapi leo, au mna wenyeweji hapa Tanga?”
“Tutalala gesti,” Latifa akaniambia.

“Kwani tutakapotoka hapa hospitali, wewe utakwenda wapi?” Faiza akaniuliza.
“Nitakwenda nyumbani Pemba nipumzike kwa wiki moja kabla ya kurudi Uingreza.”
“Kama huna ndugu hapa Tanga tungeondoka pamoja twende Bagamoyo ukawaone ndugu zangu wengine.”

“Sawa,” nikamkubalia Faiza.
Asubuhi ya siku ya pili yake tukaruhusiwa kutoka hospitalini lakini tuliambiwa tusiondoke hadi polisi wafike kwani walikuwa wameshaarifiwa kuwa tumepewa ruhusa.
Mganga mkuu wa hospitali ya Bombo alituambia kuwa baada ya wao kuwaarifu polisi kuwa tumepewa ruhusa, polisi walimwambia tuwasubiri.

Wakati huo ndugu zake Faiza walikuwa wameshafika. Tukasubiri hadi saa nne ambapo mkuu wa polisi wa wilaya ya Tanga pamoja na msaidizi wake walifika.

Msaidizi wa mkuu wa polisi wa wilaya alitupiga picha mimi na Faiza. Sikuweza kujua walitupiga picha za nini. Kila mmoja wetu akatakiwa aache anuani yake na pia aeleze anakwenda mji gani.

Maelezo yetu yaliandikishwa. Tulipomaliza kutoa maelezo hayo tukaruhusiwa kuondoka.
Tulipoondoka hospitali ya Bombo tulipanda teksi iliyotufikisha stendi ya mabasi ya Tanga, tukapanda basi la kuelekea Dar.

Basi hilo liliondoka saa sita mchana likawasili Mkoa wa Pwani saa kumi. Tukapanda basi jingine lililotupeleka Bagamoyo.
Tulipofika kwa kina Faiza jua lilikuwa limeshakuchwa. Kwa vile Latifa alikuwa amewajulisha wazazi wao kuwa tunakuja, tulikuta watu wakitusubiri nje ya nyumba yao kama wageni wa shani.

Kukafanyika kitu cha ajabu ambacho sikuweza kujua maana yake wakati ule.
Wakati tunafika pale nyumbani, Faiza aliambiwa asiingie ndani kwa mlango wa mbele bali aingie kwa kutumia mlango wa uani.

Lakini kabla ya kuingia kwa mlango huo, pale mbele ya mlango palikuwa na watu wanachinja mbuzi mweusi.
Mbuzi alipochinjwa, Faiza aliambiwa aruke ile damu ndipo aingie ndani. Faiza akaruka damu ya mbuzi kisha akaingia ndani. Sisi wengine tuliambiwa tuingie kwa kutumia mlango wa kawaida.

Tukaingia. Pale sebuleni nako nikaona mambo mengine yanafanyika. Faiza alipoingia alikalishwa chini. Alipokaa ikawekwa sinia ya chakula juu ya kichwa chake. Chakula chenyewe kilikuwa ni wali kwa maziwa ya mgando.

Kulikuwa na watoto wasiopungua saba wakaambiwa wasimame na kula kile chakula kilichokuwa juu ya kichwa cha Faiza. Watoto hao walikula hadi wakaumaliza wali wote.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave a Comment