Msanii wa vichekesho, Musa Kitele
KATIKA kolamu hii tunayowaletea wasanii mbalimbali wa filamu, leo hii tunaye msanii wa vichekesho, Musa Kitele ambaye amefunguka kama ifuatavyo kutokana na maswali aliyoulizwa katika kolamu hii wiki iliyopita.
Msomaji: Habari yako kaka Kitale, navutiwa sana na uimbaji wako lakini mbona upo kimya kwenye fani ya muziki sikusikii kabisa au umeamua kuacha?
Kitale: Siyo kwamba nimeacha muziki tegemea makubwa zaidi, kwa sababu nina vipaji vingi inategemea akili yangu inavyonituma kwa kila ninachotaka kukifanya.
Msomaji: Kaka vipi bado upo na mkeo na mmebahatika kupata watoto wangapi mpaka sasa?
Kitale: Ndoa yangu bado ipo na tumebahatika kupata mtoto mmoja anaitwa Ahmed.
Msomaji: Wasanii wengi wenye mafanikio wanahusishwa na imani za Freemason, vipi na wewe upo miongoni mwao na unazungumziaje hiyo Freemason ni kweli inawapa watu utajiri?
Kitale: Kwanza mimi sipo katika Freemason, ninavyofahamu Freemason ni binadamu anayempinga Mungu, sasa kwa maana hii inamaanisha kwamba watu wote wanaomkiuka Mungu kwa kufanya mambo aliyowakataza ni Freemason na mbona kuna wengi wanafanya maasi na siyo matajiri?
Msomaji: Nakukubali sana Mkude Simba, ningependa kujua familia yako inakuchukuliaje hususan mke wako kwa jinsi unavyoigiza haikushushii hadhi?
Kitale: Ukinichukulia Kitale kutokana na kazi zangu utaniona hivyo lakini ukichukulia kutokana na uhalisia wa maisha yangu ya kawaida ni mtu mwingine kabisa, tofauti na unavyoweza kufikiria.
Msomaji: Napenda sana kazi zako na Stan Bakora, nilisikia una kampuni inayohusiana na maswala ya sanaa, bado ipo hai au imekufa maana siisikii?
Kitale: Kampuni ipo inaitwa Macho Media na siku chache sijazo nitakuja na filamu yangu ya Shobo Dundo, nimecheza na Yobnesh Yusuph ‘Batuli,’ Stan Bakora na wasanii wengine.