×

The angel of darkness – 40

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari. Baadaye Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito na anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.

Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa ameanza kuchanganya bangi na Cocaine kwa lengo la kupunguza msongo wa mawazo.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Njia nzima Arianna alikuwa akiendelea kuhisi hali ambayo haijawahi kumtokea kutokana na matumizi ya mchanganyiko ule hatari wa madawa ya kulevya. Akawa anamhimiza dereva kuongeza mwendo wa bodaboda na hatimaye wakawasili kwenye jumba la Msuya.

Akamlipa dereva wa bodaboda na kuanza kujikongoja kuelekea ndani huku akijitahidi asionekane na mtu yeyote kwani kwa hali aliyokuwa nayo, ilikuwa aibu kubwa.
“Arianna! Unatoka wapi?” alishtuka kusikia swali hilo, akaanza kutetemeka kwani aljua hatimaye ukweli wake unaenda kujulikana, taratibu akageuza shingo yake kumtazama aliyekuwa akimuuliza.

Tofauti na alivyotegemea kwamba atakutana na Msuya akiwa amekunja sura, aligundua kuwa kumbe aliyekuwa anamuita hakuwa mumewe bali Diego.
“Unasemaje?” alimjibu kwa jeuri, mishipa ya kichwani ikiwa imesimama.
“Nakuuliza umetoka wapi muda huu?”

“Kwani wewe ni nani mpaka uniulize maswali hayo?”
“Haa! Arianna wewe ndiyo wa kunijibu hivi? Sitaki kuamini.”
“Utajijua,” alisema Arianna kisha akageuka na kutembea kuelekea ndani, Diego akabaki amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini kilichotokea. Tangu alipofahamiana na Arianna, hakuna siku aliyowahi kumjibu hovyo kiasi hicho, akaanza kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

“Au kwa sababu nimemwambia tutoroke? Halafu mbona leo macho yake yamekuwa mekundu kiasi hicho?” Diego aliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Mwisho akaamua kurudi chumbani kwake, huku mawazo mengi yakiendelea kukisumbua kichwa chake.

Baada ya kuingia ndani, Arianna alipitiliza moja kwa moja mpaka chumbani, akaenda kuficha ile misikoto aliyonunua, akavua nguo na kuelekea bafuni. Kila kitu alikuwa akikifanya harakaharaka kwani aliamini muda wowote mumewe atarudi na hakutaka amkute kwenye hali hiyo.

Alipoingia bafuni, alifungulia maji ya ‘bomba la mvua’ na kukaa kwa dakika kadhaa yakimmwagikia. Angalau ulevi ulipungua kidogo kichwani mwake, akapigwa mswaki na aliporidhika, alitoka mpaka chumbani, akavaa nguo za kulalia na kujipulizia manukato, akajitupa kitandani. Dakika chache baadaye, usingizi mzito ulimpitia tena.

Kwa jinsi alivyotengeneza mazingira ya chumbani humo, hata mumewe aliporudi kazini, aliamini mkewe atakuwa amelala kwa muda mrefu ndiyo maana hata hakuweza kula chakula cha mchana wala kutoka nje kutwa nzima.

“Mke wangu kipenzi,” alisema Msuya huku akimbusu mkewe kimahaba na kumtingisha ili aamke. Muda mfupi baadaye, Arianna alizinduka usingizini, kwa kumtazama, ilionesha kama amelala kwa muda mrefu kwani macho yake yalikuwa mekundu sana.

“Unajisikiaje mpenzi,” alisema Msuya huku akimkumbatia, kama kawaida yake Arianna akaanza ‘kumuektia’ kwamba alikuwa anajisikia vibaya sana na ndiyo maana kutwa nzima alishinda akiwa amelala.

“Pole sana mke wangu, huyu mtoto kwa nini anakutesa kiasi hiki?” alisema Msuya huku akilipapasa tumbo la Arianna ambalo lilishaanza kuonesha kwamba ana ujauzito. Arianna akaachia tabasamu hafifu, Msuya akamuomba waende pamoja sebuleni kupata chakula cha jioni.

Hata hivyo, Arianna alikataa kabisa kwenda kula, ikabidi Msuya awaambie wafanyakazi wake wa ndani wampelekee chakula chake na cha mkewe chumbani, jambo ambalo walilitii. Chakula kilipoandaliwa, Arianna alikula kidogo tu kisha akarudi kitandani kulala.

Msuya hakuwa na kipingamizi kwani aliamini kwamba kinachomsumbua mkewe ni ujauzito na hakuna kingine chochote. Akaendelea kula peke yake, alipomaliza wafanyakazi wake walitoa vyombo, akaenda kuoga na kurudi kitandani kupumzika na mkewe.

“Arianna.”
“Abee mume wangu,” aliitikia Arianna kwa sauti ya kichovu.
“Najua unajisikia vibaya mke wangu lakini tafadhali naomba tuzungumze kidogo,” alisema Msuya huku akimpapasa mkewe mgongoni, Arianna akageuka ili kumsikiliza mumewe.

Kwa lugha laini, iliyojaa maneno ya kubembeleza, Msuya alimwambia Arianna kwamba anaona huo ni muda muafaka wa kwenda kuwachukua watoto wake aliozaa na marehemu mke wake wa kwanza ili waishi pamoja na kuendeleza familia.

Arianna hakuwa na kipingamizi chochote, akamueleza na yeye atajisikia furaha zaidi ndani ya moyo wake akiishi na watoto hao na kupendekeza kwamba badala ya kuendelea kusoma shule za bweni (boarding), wawatafutie shule ya kutwa ili wapate muda wa kukaa nao zaidi, kauli ambayo ilimfurahisha sana Msuya. Akamkumbatia na kuendelea kumwagia mvua ya mabusu, wakalala pamoja.

Kesho yake, Msuya alijiandaa na kuelekea kazini kwake kama kawaida. Muda mfupi tu baada ya kuondoka, Arianna aliamka na kujifungia mlango kwa ndani, akapanda juu ya kabati la nguo alikoficha misokoto ya madawa ya kulevya na kuanza kuvuta.

Kwa kuwa chumba chao cha kulala kilikuwa ghorofani, hakuna mtu yeyote aliyesikia harufu ya bangi iliyochanganywa na Cocaine aliyokuwa anavuta Arianna. Baada ya kumaliza msokoto mmoja, Arianna alikuwa amelewa chakari, akajibwaga palepale chini alipokuwa amekaa na kupitiwa na usingizi mzito. Alikuja kuzinduka saa tisa za jioni baada ya kusikia mlango wa chumba chake ukigongwa, harakaharaka akaamka na kuficha ushahidi wote, akapulizia manukato maalum ya chumbani (air freshner) kisha akaenda kufungua mlango.

Alikuwa ni mfanyakazi wa ndani aliyekuwa amebeba sinia lililokuwa na chakula, akamruhusu kuingia na kwenda kuweka chakula hicho mezani. Harakaharaka Arianna akafunua sinia na kuanza kuangalia chakula hicho.

“Mbona hujaweka kipande cha ndimu?” alizungumza Arianna kwa kufoka, jambo ambalo hakuwahi kulifanya hata mara moja tangu aingie ndani ya nyumba hiyo. Yule mfanyakazi alimuomba radhi Arianna na kutoka kwenda kuchukua ndimu lakini Arianna hakuacha kufoka, akawa anaendelea kubwata kwa ukali utafikiri amefanyiwa kosa kubwa sana.

Muda mfupi baadaye, yule mfanyakazi alirejea akiwa na kipande cha ndimu na kukiweka pale mezani, akarudia tena kumuomba radhi Arianna lakini hakumjibu kitu zaidi ya kumtaka aondoke haraka chumbani kwake.

Harakaharaka akatoka huku akipatwa na mshangao mkubwa, hakuelewa amepatwa na nini mpaka awe mkali kiasi hicho. Hata alipoenda kumsimulia mfanyakazi mwenzake kilichotokea, wote walibaki wamepigwa na butwaa, hawakuelewa ni kwa sababu gani Arianna alikuwa mkali kiasi hicho, wakahisi hayupo sawa lakini atarudi kwenye hali yake ya kawaida akishatulia.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave a Comment