×

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani – 6

ILIPOISHIA:

Sikutaka kujua pale amefikaje japo nammiliki lakini sidhani kama nilikuwa na haki ya kumuuliza pale amefuata nini. Lakini nilijikaza kike na kumuuliza kwa sauti ya ukali:
“Bantu huku umekuja kufanya nini?”
“Kabla sijakujibu, niambie huyu ni nani?” Bantu aliniuliza akiwa amekunja uso.

SASA ENDELEA…

“Bantu siku hizi huniheshimu yaani unatoka nyumbani bila idhini yangu,” nilijikakamua mtoto wa kike.“Bado hujanijibu huyu ni nani?” Bantu bado alinikalia kooni na kunifanya niwe kwenye wakati mgumu.

“Kwani dear huyu ni nani?” Abdul aliuliza.
“Abdul usiingilie we kaa pembeni,” nilimzuia Abdul asiingilie ugomvi wangu na Bantu.
“Hapana honey lazima nimjue huyu ni nani?” Abdul naye alitaka kumjua Bantu ni nani.
“Konso hapa ndiyo kwenye biashara? Ina maana kila siku unanila kisogo kwa kunidanganya kwa mtindo huu?” Maskini Bantu aliongea kwa sauti ya kilio, mmh! Nilijua nimeuvaa mkenge Bantu nitamueleza nini ili anielewe na Abdul nitamueleza nini ili anielewe.

Kimasilahi Abdul alikuwa mtu muhimu na kimapenzi Bantu alikuwa na umuhimu mkubwa. Swali lilikuja nitumie lugha gani wote wanielewe. Nilijikuta naongea lililokuja akilini.

“Bantu hebu njoo,” nilimshika mkono ili nimuondoe mbele ya Abdul.
“Konso unanipeleka wapi?” Bantu aligoma ili apate maelezo sahihi ya mimi kumuondoa pale.

“Hapana Bantu hebu njoo huku tuongee,” niliung’ang’ania mkono wake na kumuondoa pale.
“Honey huyu nani…kaka yako?” Abdul aliuliza akiwa amepigwa na bumbuwazi.
Nilijikuta nanyanyua kichwa kukubali kuwa Bantu ni kaka yangu bila kujibu neno. Kumbe Bantu ameona, Mungu wangu hapo ndipo Bantu alipokuja juu kama moto wa kifuu.

“Konso kweli umenichoka yaani mimi ni kaka yako?”
“Mbona sikuelewi…vipi bwana mdogo una tatizo gani kama dada yako ametoka bila ruksa ni kiasi cha kuelewana,” mmh! Makubwa, Abdul alimsogelea Bantu ili ampoze.
“Basi bwana shemeji hapa ni sehemu ya starehe hakuna haja ya kupigizana kelele na dada yak….”

He! Hakumalizia sentesi ngumi nzito ya mkono wa kushoto ya Bantu ilitua kwenye shavu la upande wa kulia kwa Abdul lililomtupa kwa nyuma. Nilijikuta napiga ukelele.
“Ha! Bantu unafanya niniii?”

Kumbe kipigo kile hakikuwa cha Abdul peke yake kiligeukia kwangu huku kikifuatia na matusi mazito juu yangu. Kwa kuitwa mwanamke malaya, fagio la chooni, jamvi la wageni basi kila aliloliona linanifaa kutukanwa Bantu alinitukana usiku ule.

Kipigo nilichopewa na Bantu kilinifanya nipoteze fahamu na kuzinduka siku ya pili na kujikuta nipo hospitali nimelazwa. Muuguzi alinieleza kuwa jana usiku tuliletwa na mume wangu tukiwa tumepoteza fahamu ila mume wangu ndiye mwenye hali mbaya kwa kuwa alikuwa na majeraha mengi.

Japokuwa nilijua Bantu ndiye aliyetoa kipigo nilishindwa kuelewa mume wangu gani aliyeletwa hospitali kati ya Bantu na Abdul. Kutokana na matibabu mazuri niliweza kunyanyuka mwenyewe na kuweza kutembea japo mwili ulikuwa ukiniiuma kwa mbali nilijua bila dawa za maumivu yangekuwa makubwa sana.

Nilikwenda ofisi ya wauguzi na kuwaomba wanioneshe bwana niliyeletwa naye usiku. Tuliongozana na yule muuguzi hadi kwenye wodi ya wanaume na kuingia. Mmh! Kumbe alikuwa ni Abdul ambaye alikuwa kwenye plasta ikionesha aliumizwa sana.

Nilikwenda hadi kwenye kitanda chake aliponiona alianza kulia na kunilaumu.
“Konso kosa langu nini mpaka utake kuniua?”
“Pole Abdul yule ni kaka yangu.”

“Muongo mkubwa, mwanamke mbaya wewe! Kwa nini Konso hukuniambia ukweli kuliko kunifanya hivi? Ona sasa mambo yangu yote yamevurugika…kwa nini hukuniambia ukweli kama una bwana?”

“Nisamehe Abdul,” nilijikuta nikipiga magoti kuomba msamaha.
“Siwezi kukusamehe wewe ni muuaji, yaani kila ulichotaka nilikupa matokeo yake unanifanya hivi? Hata sijui nitakuwa kwenye hali gani nikitoka nimeambiwa mbavu zimeteguka.”

“Lazima nimshtaki.”
“Haitasaidia nimeshaumia, ana haki kwa vile ni mumeo.”
“Abdul sijaolewa yule ni rafiki yangu wa zamani lakini tulikwisha achana,” nilijikuta nikichanganya maneno.

“Leo hivi kesho nitegemee mauti…kwa mtindo huo mimi na wewe basi.”
“Usiniache Abdul, usiniache bado nakupenda lazima mshenzi yule nitamshikisha adabu.”

“Haitasaidi kitu, kweli shukurani ya punda nimeiona, yote niliyokufanyia nimeambulia maumivu.”
“Abdul…Abdul.”

Nilianza kulia kwa kweli kumkosa Abdul kwa ajili ya kula kulala Bantu sikukubali, nilipanga lazima nimshtaki ikibidi nimfunge. Kilio changu kilimfanya Abdul awaite wauguzi ili wanirudishe chumbani kwangu. Niliondoka huku nikilia na kumchukia Bantu hata kama sikumuaga hakuwa na haki ya kunipiga kwa sababu maisha yake nayamiliki mimi hana tofauti na mwanamke. Na upande mwingine wanawake wengi wameamka kila mtu siku hizi anajitafutia.

Nilirudi hadi chumbani kwangu na kuanza kulia kwa hali aliyokuwa nayo Abdul, kama kweli angekuwa ameumia kama alivyonieleza basi lazima hakutakuwa na mapenzi na hawezi kunisamehe.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave a Comment