×

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni-47

ILIPOISHIA

Nikamueleza jinsi nilivyokutana na Faiza akiwa ameshakaa kwa miaka minne ndani ya mapango hayo. Nikamueleza na yale yaliyotokea hadi tukaweza kutoka ndani ya mapango hayo.

 “Ni simulizi ya ajabu sana. Kwa kweli umekutana na masaibu makubwa!”

“Lakini nashukuru kuwa tumesalimika, hivi sasa niko Bagamoyo.”

“Bagamoyo kwa nani?”

ITAENDELEA…

Bagamoyo kwa huyo msichana niliyekutana naye ndani ya hilo pango. Alinialika kwao na mimi ishaalah nitamualika kwetu.”

 “Sasa unatarajia  kuja lini huku, watu wanataka wakuone.”

 “Nitakuja hivi karibuni, labda kesho nitakwambia nitakuja  lini.”

 “Usichelewe sana, ile habari tuliyosoma kwenye gazeti imewapa wasiwasi watu wengi.”

 “Sitachelewa kwa sababu nahitaji kurudi haraka Uingereza.”

 Baada ya kuzungumza na kaka yangu nilirudisha simu niliyokuwa nimeazima.

 Nilikaa Bagamoyo kwa siku tatu. Katika mazungumzo yaliyokuwa yakizungumzwa pale nyumbani ni kuwa aliyekuwa mchumba wa Faiza kijana aliyetoka Mombasa alirudi kwao baada ya Faiza kupotea katika mazingira ya kutatanisha siku ya harusi yao.

 Taarifa ambayo ilimsikitisha Faiza ni kuwa yule mume alikuwa tayari ameshaoa mke mwingine wa huko huko kwao Mombasa.

 “Kila jambo linakwenda kwa riziki mwanangu,” mama yake Faiza alisema wakati tunazungumza ile habari.

 “Ni kweli mama, kila jambo linakwenda kwa riziki. Kama jambo halikupangwa na Mungu haliwezi kuwa,” Faiza akamwambia mama yake na kuongeza.

 “Jambo lilioko katika akili yangu kwa sasa si kufikiria mume aliyepita bali kila wakati nashukuru Mungu kuwa nimenusurika, vinginevyo ningekufa au ningebaki kule kule mapangoni na nisingejulikana niko wapi.”

 “Ni kweli Faiza, jambo kubwa ni kushukuru Mungu. Kule tulikokuwa nusu ni duniani na nusu ni kuzimu,” nikamwambia Faiza.

 Katika siku hizo tatu nilizokaa Bagamoyo, ndugu zake Faiza walinitembeza tembeza katika mji wao. Niliona maeneo mengi ya kitalii yakiwemo mahoteli ya gharama kubwa. Zilikuwa siku adimu za kupumzisha moyo wangu ambao kwa siku chache zilizopita ulikuwa ukihangaika.

 Nilishamwambia Faiza kuwa baada ya siku hizo tatu ningeondoka kwenda Pemba.

Faiza akanitazama kwa tabasamu kisha akaniuliza.

 “Utaniacha hapa Bagamoyo?”

Sikutegemea kama angeniuliza swali kama hilo. Nikajiuliza Faiza alikuwa akiniuliza kwa mzaha au aliniuliza kwa dhati. Nikachukulia kuwa aliniuliza kwa mzaha.

 “Twende pamoja,” nikamwambia.

 “Kama unaniambia kweli niko tayari. Naamini wazazi wangu wataniruhusu.”

“Wewe umekuja kunionesha ndugu zako ni wajibu wangu na mimi kukuonesha ndugu zangu.”

“Ni kweli, ngoja nikamwambie mama.”

Baada ya muda kidogo Faiza alikuja kuniambia.

 “Mama anakuita.”

 Nikaenda naye kwa mama yake.

 “Hivi kesho ndiyo unaondoka?” akaniuliza.

 “Ndiyo mama.”

 “Faiza ameniambia utaondoka naye kwenda Pemba.”

 “Nimemwambia twende sote kama atapata ruhusa yenu. Nataka ndugu zangu nao wakamuone.”

 “Ni sawa lakini mimi napenda uende pamoja na dada yake.”

 “Itakuwa vizuri zaidi.”

“Mtarudi lini?”

“Kule Pemba nimepanga tukae kwa siku mbili tu, siku ya tatu tunaondoka. Nikiwarudisha hapa Bagamoyo, mimi narudi Dar kwenda kufanya mipango ya kurudi Uingereza ninakofanya kazi.”

Baada ya mazungumzo mafupi na mama yake Faiza, nikamwambia Faiza na dada yake wajiandae kwa safari, siku iliyofuata tukaondoka, mimi na Faiza pamoja na dada yake.

 Tulipanda basi tukaenda Dar. Tulipofika Dar kabla ya kupanda boti niliomba simu kutoka kwa dada yake Faiza, nikampigia kaka kumjulisha kuwa niko bandarini Dar ninakwenda Pemba nikiwa na Faiza pamoja na dada yake.

 Kaka akafurahi kujua kuwa tulikuwa njiani tukielekea Pemba.

 Muda wa kujipakia kwenye boti ulipowadia tukajipakia kusubiri safari. Wakati wote nilikuwa nikizungumza sana na dada yake Faiza kuliko Faiza mwenyewe. Huyo msichana alikuwa mchangamfu sana.

 Safari yetu ya kwenda Pemba ilikuwa nzuri. Faiza aliniambia ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda boti. Alisumbuka kidogo tu kutokana na mawimbi lakini baadaye akazoea.

Tulipofika bandarini Pemba, baada ya kushuka kwenye boti nikamkuta kaka pamoja na ndugu wengine wawili wakisubiri kutupokea.

 Baada ya kusalimiana na kuwatambulisha kwa Faiza na dada yake, walitupakia kwenye teksi iliyotupeleka katika eneo tulilokuwa tunaishi.

Ilikuwa ni furaha kubwa kukutana na ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wazazi wangu.

 Baada ya kuwaelezea ndugu zangu masaibu yaliyonikuta huko Tanga, Faiza alionekana kioja kikubwa hasa kwa vile ambavyo nilimkuta katika lile pango akiwa amekaa kwa miaka minne.

 Watu walitupa pole na kututakia maisha mema. Faiza ndiyo walimpongeza sana. Baada ya mazungumzo marefu na ndugu zangu, kaka yangu akaniambia alikuwa akiwasiliana na mke wangu karibu siku zote tangu nilipokuwa sijulikani niko wapi.

 Nikaomba simu kwa kaka nikaingia chumbani na kumpigia mke wangu. Nilizungumza na mke wangu kwa karibu robo saa. Nikamfahamisha kuwa nilikuwa niko katika maandalizi ya kurudi Uingereza.

 Kama nilivyokuwa nimepanga, nilikaa Pemba kwa siku mbili. Siku ya tatu nikaondoka na wenzangu. Nilikuwa nimenunua simu mpya ambayo niliirudishia laini yenye namba yangu za zamani.

 Lakini wakati tumo kwenye boti tukirudi Dar, nilimuona Faiza alikuwa amechukia.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave a Comment