Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.
Wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari. Baadaye Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito na anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.
Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa ameanza kuchanganya bangi na Cocaine kwa lengo la kupunguza msongo wa mawazo, jambo linalosababisha mabadiliko makubwa kwenye tabia yake. Diego naye bado hajakata tamaa, anaendelea kumshawishi wamuibie Msuya na kutoroka. Safari hii anatumia vitisho.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
“Ninachotaka mimi unakijua. Nataka tutoroke hapa kwa Msuya, twende mbali tukailee pamoja hiyo mimba kwa sababu mimi ndiye baba wa mtoto. Tumuibie Msuya fedha za kutosha na vitu vingine ambavyo vitatusaidia kuanza maisha huko tuendako.
“Tukiendelea kukaa hapa, siku ukijifungua Msuya atagundua ukweli na tutapoteza kila kitu, hebu amka usingizini,” alisema Diego kwa sauti ya chini lakini kwa msisitizo mkubwa.
Arianna alishusha pumzi ndefu na kumtazama Diego usoni, macho yao yakagongana.
“Lakini Diego?”
“Lakini nini Arianna? Kinachokufanya uwe unasitasita kila mara ni nini?”
“Lakini Msuya hajatufanyia jambo lolote baya, kwa nini tumlipe mabaya?”
“Hatumlipi mabaya, tunachukua tunachostahili kuchukua Arianna, au umesahau lengo la kukubali kuja kuishi na Msuya?” Diego alisema kwa msisitizo, Arianna akashusha pumzi ndefu na kugeukia pembeni.
Ni kweli walikubaliana tangu mwanzo kwamba Arianna akubali kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Msuya na hata ikiwezekana kufunga naye ndoa kama ilivyotokea lakini kwa lengo moja tu; kupata pesa kwa njia ya mkato.
“Halafu siku hizi kuna vitu unatumia unajifanya ni siri yako. Mimi nakujua tangu ukiwa msichana mdogo, huwezi kunificha chochote. Unafikiri Msuya akijua tabia zako halisi atakufanya nini zaidi ya kukuacha na kutufukuza hapa kwake? Unataka tukarudie maisha yetu ya zamani ya kuhangaika mitaani?” alisema Diego, kauli iliyomfanya msichana huyo ashushe tena pumzi kwa mara nyingine.
“Kwa hiyo unataka iweje?” alihoji Arianna, kauli iliyomfanya Diego aachie tabasamu pana, akamsogelea na kumnong’oneza sikioni.
“Hatuwezi kuzungumzia hapa, twende chumbani kwangu, mi natangulia,” alisema Diego kwa sauti ya kunong’ona na bila kusubiri majibu ya Arianna, aliondoka na kuelekea chumbani kwake.
Arianna alibaki amesimama palepale walipokuwa wakizungumzia kwa dakika kadhaa kama anayetafakari kitu. Ili kuwapoteza maboya wafanyakazi wa ndani wa Msuya, alirudi chumbani kwake kwanza na kwenda kujimwagia maji huku akiendelea kutafakari.
Baadaye akatoka na kuelekea chumbani kwa Diego huku akiwa makini kuhakikisha hakuna anayemuona. Alipoingia tu, Diego alienda kufunga mlango kwa funguo kisha akarudi mpaka kitandani, Arianna alipokuwa amekaa akionesha kuwa na mawazo mengi.
Baada ya kulikosa penzi la Arianna kwa muda mrefu, Diego aliona huo ndiyo muda muafaka wa kukata kiu yake. Kwa kuwa tayari alishaelewa ni madawa gani Arianna aliyokuwa anayatumia yaliyomfanya abadilike kiasi hicho, Diego alisokota Cocaine iliyochanganywa na bangi kisha akawasha na kumpa Arianna.
“Umejuaje?”
“Nilishakwambia mimi nakujua tangu ukiwa msichana mdogo, utawadanganya watu wote lakini siyo mimi,” alisema Diego, Arianna akaachia tabasamu hafifu na kuanza kuvuta kwa pupa. Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa akielea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa, Diego akatumia nafasi hiyo kutimiza haja zake.
Baada ya hapo, wote wawili walipitiwa na usingizi mzito, walipokuja kuzinduka tayari ilikuwa ni saa tisa alasiri, wakaamka na kuendelea na mjadala wao huku kila mmoja akionesha bado kuwa na madawa kichwani.
“Fanya kila kinachowezekana kuhakikisha unazijua namba za siri za kadi za ATM za mumeo, kesho inabidi tukaangalie kuna kiasi gani cha fedha benki na tuone kama zitatutosha kwenda kuanzisha maisha mapya. Pia chunguza kama kuna fedha na madini chumbani kwenu, si unajua watu kama hawa hawakosi kuwa na akiba ndani,” alisema Diego, Arianna akawa anakubali kila anachoambiwa.
Baada ya kuwa wamefikia muafaka, Arianna alitoka chumbani kwa Diego na kuingia ndani huku akiwa makini kuhakikisha hakuna anayemuona.
Akafanikiwa kwenda mpaka chumbani kwake bila kuonekana, akaenda kuoga na alipotoka, alianza kujipamba ili hata mumewe akija asigundue kitu chochote kwamba ametoka kufanya mapenzi na mwanaume mwingine wala asigundue kama ametumia madawa ya kulevya.
Baada ya kumaliza kujipodoa na kujipamba, Arianna alitoka hadi sebuleni alikowakuta watoto wakicheza huku wafanyakazi wa ndani wakiendelea na maandalizi ya chakula. Ujio wake sebuleni hapo ulisababisha amani kutoweka kabisa kwani kila mara alikuwa akifokafoka bila hata sababu ya msingi, mwisho akawaamuru watoto wote kwenda kulala mpaka chakula cha usiku kitakapokuwa tayari.
Watoto walipoenda kulala, aliwageukia wafanyakazi, nao akaanza kuwafokea bila sababu na kuwafanya wakose kabisa amani. Kwa bahati nzuri, muda mfupi baadaye mumewe alirejea kutoka kazini, ikawa ahueni kwa watu wote ndani ya nyumba hiyo kwani angalau Arianna alikuwa akipunguza ukali wake mumewe anapokuwepo.
Siku hiyo alijitahidi kumchangamkia mumewe kwani kuna jambo lake alilokuwa nalo kichwani kama walivyokubaliana na Diego. Baadaye walikula chakula cha usiku pamoja kisha Arianna na mumewe wakaelekea chumbani kwao ambapo msichana huyo aliutumia usiku huo kumlainisha mumewe.
Kwa jinsi Msuya alivyokuwa akimpenda mkewe, alijikuta akitoa siri zake zote kuhusu utajiri wake, hakuwa na wasiwasi na Arianna hata kidogo kwani tayari alikuwa ni mke wake halali na kama hiyo haitoshi, alikuwa anaamini kwamba ujauzito aliokuwa nao msichana huyo ulikuwa ni wake.
Tofauti na siku nyingine zote, siku hiyo walizungumza mpaka saa sita za usiku, mpaka kila mmoja anapitiwa na usingizi, tayari Arianna alikuwa ameshapata alichokuwa anakihitaji. Kesho yake asubuhi, Msuya aliwahi kuondoka kuelekea kwenye shughuli zake kama kawaida.
Alipoondoka tu, Arianna naye aliamka na kumfuata Diego, mkononi akiwa na funguo za gari moja la kifahari la Msuya. Kwenye mkoba wake mdogo, alikuwa amebeba kadi za benki (ATM) karibu tano, zote akiwa tayari anajua namba zake za siri.
Akamuamsha Diego na kumpa funguo za gari, wakawadanganya wafanyakazi kwamba wanaenda kliniki kwa sababu Arianna hakuwa anajisikia vizuri. Wakatoka Diego akiwa ndiyo dereva.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/